KIFAA CHA MUUNGANISHO: Hiki ni kifaa chochote kinachosambaza mawimbi ya Wi-Fi na kuwezesha upatikanaji wa Intaneti.
AKILI BANDIA: Uwezo wa kuelewa algorithimu zinazotumika katika mifumo ya akili bandia ambayo mtu huingiliana nayo pamoja na mazungumzo ya kimaadili kuhusu ukuzaji wa teknolojia hizi.
KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII NA KISIASA: Uwezo wa kushiriki katika masuala ya kiraia (mfano, haki za jamii ya LGBTQ, kuleta amani, kushughulikia hotuba za chuki) na kupigania mambo ambayo mtu anajali — kutumia zana zilizo na zisizo za kidijitali — ili kuboresha hali ya maisha ya mtu katika jamii kutoka katika viwango vya chini hadi vya juu vya uchumi (Levine, 2007).
KUSAHILISHA MATATIZO YA KOMPYUTA: Uwezo wa kuelewa na kutumia dhana, taratibu na mitazamo katika matumizi ya kompyuta. Dhana katika matumizi ya kompyuta ni pamoja na dhana ambazo watu hutumia wanapotengeneza programu (mfano, kutambua msururu wa hatua za shughuli fulani, au kuendesha misururu mara nyingi inayofanana). Taratibu katika matumizi ya kompyuta ni zile ambazo watu hupata huku wakitengeneza programu (mfano, kufanya majaribio na kurudiarudia maagizo, kutumia upya na kuchanganya, au kutengneza kitu fulani kwa kutumia mawazo au kazi ambazo tayari zipo). Mwisho, mitazamo katika matumizi ya kompyuta ni mitazamo ambayo watu hutengeneza kuhusu wao, mahusiano yao na watu wengine (kama katika jamii za mtandaoni zenye ushirikiano), na ulimwengu wa teknolojia kwa jumla (mfano, kuelewa uwezo unaotokana na kutengeneza maudhui pamoja na watu wengine na kwa ajili ya watu wengine) (Brennan & Resnick, 2012).
KUTENGENEZA MAUDHUI: Uwezo wa kutengeneza maudhui (ya kidijitali) kwa kutumia zana (za kidijitali).
MUKTADHA: Uwezo wa kufahamu, kuelewa na kufafanua vipengele vinavyotumika katika muktadha fulani (kwa mfano, kitamaduni, kijamii, kiwilaya/kimkoa/kimataifa) katika hali fulani — huku mkazo ukitiliwa kwa mambo ambayo watu kutoka makundi yenye uwakilishi mdogo wamepitia pamoja na mitazamo yao, haijalishi kama yanahusiana na umri, kabila, rangi, jinsia na mwegemeo wa kijinsia, dini, taifa la asili, eneo, kiwango cha ujuzi au elimu, na/au hali ya masuala ya kijamii na kiuchumi — na kuweza kushiriki kikamilifu katika hali hiyo.
DATA: Uwezo wa kufahamu, kuunda, kukusanya, kuwakilisha, kutathmini, kutafsiri na kuchanganua data kutoka kwenye vyanzo vya kidijitali na visivyo vya kidijitali.
UPATIKANAJI WA KIDIJITALI: Uwezo wa kuunganisha na kuipata intaneti, kwa mtu binafsi au watu wengi (mfano, teknolojia zinazounganisha watumiaji wengi).
UCHUMI WA KIDIJITALI: Uwezo wa kutekeleza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mtandao ili kuchuma rasilimali za aina tofauti za kiuchumi, kijamii, na/au kitamaduni (mfano, kupata pesa, kuongeza mitandao ya watu, kutengeneza jina binafsi).
UELEWA WA MASUALA YA KIDIJITALI: Uwezo wa kutumia intaneti pamoja na zana na mifumo mingine ya kidijitali ili kupata, kuingiliana, kutathmini, kutengeneza na kutumia taarifa upya kwa njia nzuri (Palfrey & Gasser, 2016). Uwezo wa kuelewa na kutatua matatizo katika dhana za kidijitali (Carretero, Vuorikari & Punie, 2017).
KUANGALIA NA KUBUNI UTAMBULISHO: Uwezo wa kutumia zana (za kidijitali) ili kuchunguza vipengele vya utambulisho wa mtu, na kuelewa jinsi jamii inavyochangia kutengeneza utambulisho wa mtu.
UBORA WA TAARIFA: Uwezo wa kupata,kuingiliana, kutathmini, kubuni, na kutumia taarifa upya (kwa jumla; mfano; habari, taarifa za afya, taarifa binafsi) kwa namna nzuri (Palfrey & Gasser, 2016).
INTANETI: Mtandao mkubwa wa kompyuta unaounganisha mitandao midogo ya kompyuta kote ulimwenguni. Intaneti ina mitandao ya biashara, elimu, serikali, na mitandao mingine.
SHERIA: Uwezo wa kuchangamana na mifumo, dhana, na mawazo ya kisheria kuhusu intaneti na zana zingine za kidijitali (mfano, haki za kunakili, matumizi yenye usawa) na uwezo wa kutumia mifumo hii katika shughuli zako.
UELEWA WA VYOMBO VYA HABARI: Uwezo wa kuchanganua, kutathmini, kusambaza na kutengeneza maudhui ya muundo wowote wa vyombo vya habari (mfano, yaliyochapishwa, ya kutazama, yanayoshirikisha watumiaji, ya sauti) na kushirikisha katika jamii na mitandao. Uelewa wa vyombo vya habari (Hobbs, 2010), unajumuisha mambo ambayo watafiti wengine wanachukulia kuwa "uelewa mpya" (Lankshear & Knobel, 2007), na “uelewa mpya wa vyombo vya habari” (Jenkins, Clinton, Purushotma, Robison & Weigel, 2006). Yaani, zinajumuisha mitazamo ya uelewa ambayo haijikiti tu katika kuchangamana kwa watu na vyombo vya habari (uelewa wa vyombo vya habari) ila pia una stadi zinazoangazia uhusishwaji wa jamii na desturi za ushirikishaji. "Uelewa wa vyombo vya habari" pia unajumuisha ufahamu wa kusoma na kuandika.
MODEMU: Modemu ni kifaa kinachotengeneza na kudumisha muunganisho kwa Mtoa Huduma za Intaneti (ISP) wako ili kukuwezesha kupata intaneti. Modemu hubadilisha mawimbi kutoka nje ya eneo lako mahususi kuwa mawimbi yanayoweza kusomwa na kompyuta yako pamoja na vifaa vingine vya kidijitali.
MTANDAO: Mtandao ni mkusanyiko wa mifumo ya kompyuta na vifaa vilivyounganishwa pamoja kutoka kote ulimwenguni.
TABIA NZURI/ZA HESHIMA: Uwezo wa kuingiliana na watu wengine (watu binafsi pamoja na umma kwa jumla) mtandaoni kwa namna yenye heshima, maadili mema, uwajibikaji wa kijamii na kuelewa hisia za wengine.
SIRI NA SIFA: Uwezo wa kulinda taarifa zako binafsi na za wengine katika mtandao. Ufahamu wa "alama" za kidijitali zinazoachwa baada ya shughuli ambazo mtu hufanya mtandaoni, matokeo ya muda mfupi na mrefu ya alama hizi, jinsi ya kusimamia alama za mtandaoni ipasavyo, pamoja na kuwa na ufahamu kuhusu data zilizotokana na taarifa zingine (yaani, data mpya zilizopatikana kwa kunasa na kuchanganua data zingine, ambazo huenda zikatoa maelezo mapya kuhusu mtu (van der Hof, 2016)).
RUTA: Ruta ni kifaa ambacho hutengeneza mtandao kati ya vifaa vyote (mfano kompyuta, vishikwambi, simu za mkononi) katika eneo fulani (kama vile shule, maktaba au nyumbani kwako).
USALAMA NA USTAWI: Uwezo wa kuzikabili hatari ambazo huenda zikaletwa na ulimwengu wa kidijitali ili kulinda afya yako ya mwili na akili (mfano kujilinda dhidi ya uraibu wa intaneti na majeraha yanayotokana na matumizi ya viungo kupita kiasi). Hatari za mtandaoni zinaweza kuwekwa katika kategoria kubwa tatu: matendo (unyanyasaji wa mtandaoni, unyanyasaji wa kimapenzi au kutumia mtu jumbe za kingono ambazo hataki), mawasiliano (mfano, kukutana ana kwa ana baada ya kuwasiliana mtandaoni, kuwasiliana na watu wanaojifanya mtu mwingine), na maudhui (mfano, kutazama ponografia, maudhui yenye vurugu au ghasia, maneno ya chuki, maudhui kuhusu dawa za kulevya, maudhui ya ubaguzi wa rangi) (Livingstone, Kirwall, Ponte & Staksrud, 2013).
USALAMA: Uwezo wa kulinda taarifa binafsi, vifaa vya kidijitali na rasilimali zako (mfano, taarifa za kuingia kama vile nywila, wasifu, na tovuti).