Tengeneza Mandhari: Utakapowasha kamera yako, unawasha taa darasani mwako; fikiria kuhusu mandhari unayotaka kuweka. Weka usuli utakaojaliza somo lako na kumakinisha au kuchangamsha wanafunzi wako (kulingana na mahitaji yao). Ukuta wenye rangi moja ulio na ujumbe wa kutia motisha au wito wa kila siku uliondikwa kwenye karatasi na kubandikwa, rafu sahili ya vitabu itakayomakinisha wanafunzi katika mazingira ya masomo, au usuli wa Zoom wa maabara ya kisayansi ni mifano ya jinsi unavyoweza kutengeneza mandhari yako ili kulingana na nia na masomo yako. Pia unaweza kuweka vitu kama mimea/picha kwenye ukuta au usuli ili uwe na mandhari anuwai zaidi. Jaribu usiweke vitu vingi sana kwenye picha. Epuka kuta zilizopigwa ruwaza, samani zisizohitajika, au vitu vingi vilivyotapakaa kwenye chumba. Usuli mtulivu wenye rangi iliyofifia, rangi zisizotofautiana sana na rangi nyororo mara nyingi huwa usuli mzuri zaidi. Hakikisha una nafasi ya kutosha ili uwe umbali mzuri kutoka kwenye kamera.
Waoneshe wanafunzi wako kwamba umejitolea kuwapa kiwango cha umakinifu na kujitolea, sawia na kiwango unachotaka kutoka kwao. Punguza kuvurugika kwa akili kwa kutengeneza sehemu yako ya kazi katika eneo la nyumba yako lisilopitwa na watu wengi na uweke simu za mkononi au vitu vingine vinavyovuruga akili mbali sawia na jinsi ungefanya katika darasa halisi — hata ikiwa vitu hivyo havionekani kwenye skrini.
Onekana: Mawasiliano na masomo huendeshwa kwa njia mbalimbali; kwa kuwa hauko katika eneo moja na wanafunzi wako hakumaanishi kwamba huna mawasiliano halisi na wanafunzi wako. Utataka kuonekana vizuri ili nyote mnufaike kutoka kwa sifa zote za mawasiliano ili kusaidia katika masomo na maamiliano, kutoka kwa ishara za uso katika masomo ya lugha hadi tabasamu la furaha na fahari kwa sababu ya ufanisi wa mwanafunzi. Kaa katika sehemu iliyo mraba kutoka kwa kamera, huku ukihakikisha kwamba uelekeo wa macho yako uko sawa na uelekeo wa kamera kadri inavyowezekana. Unapoweka kifaa chako ili kurekodi, hakikisha kwamba unaacha nafasi katika sehemu ya juu, ili kichwa chake kisiwe juu kabisa kwenye skrini. Fuata agizo la kugawa picha kwa thuluthi ili picha iwe na usawa unaofaa. Epuka kuvaa shati na marinda yenye mistari, alama ndogo au mistari mieusi na mieupe kwa sababu mavazi haya hayatapendeza kwenye video. Mwanga wa asili ndio unaofaa zaidi kwa kurekodi video na kupiga picha. Ikiwa chanzo chako cha mwanga kiko nyuma au juu yako, mwanga utang'aa juu yako na kufanya uwe na duara leusi chini ya macho yako. Hili litakufanya uonekane kama mtu asiyeaminika. Hivi hapa ni vidokezo zaidi vitakavyokusaidia:
- Unatakiwa kuelekea kwenye mwanga, lakini mwanga usiwe mkali sana kiasi kwamba unafunga macho kidogo.
- Chanzo cha mwanga kinafaa kutoka nyuma ya kamera.
- Ikiwa hakuna mwanga wa asili, na unatumia taa zilizo kwenye dari, zitatoa mwanga mzuri kwenye nyumba lakini hakikisha kwamba hujasimama moja kwa moja chini ya taa kwa kuwa hilo litasababisha vivuli.
- Tumia taa ya mezani au tochi isiyo na mwanga mkali inayokumulika ili kuweka sawa mwanga. Kadri taa hiyo itakavyokuwa mbali na wewe, ndivyo mwanga wako utakavyokuwa wa kawaida kwenye uso wako.
- Mwanga mdogo unaomulika uso wako na kamera inafaa kuwa katika kiwango sawa na macho yako.
Sikika: Sauti ya kutegemewa na yenye nguvu ni muhimu katika kumakinisha wanafunzi na kuboresha mafundisho yao. Masomo ya mtandaoni hutegemea mafundisho ambapo mkufunzi hayuko kwenye skrini au haonekani. Hii husasan huonekana unapohakikisha kila mtu anaiona skrini au vitu vilivyomo. Katika nyakati hizi, toni ya sauti imara na changamfu huwa muhimu sana. Ishara za sauti zinaweza kueleza mambo ambayo hapo kabla ungetegemea tu ishara za mwili au mbinu zingine za mazungumzo zisizotumia maneno ili kuelezea, katika hali ya kawaida. Kumbuka kuwatia moyo wanafunzi wako kwa sauti ya juu, kwa kuwa huenda hawataweza kuona ukiamkia kwa kichwa chako au kutabasamu kama njia ya kuwatia moyo.
Wafundishe Wanafunzi Wako Teknolojia: Kumbuka kwamba, kama ulivyo wewe, huenda pia wanafunzi wako ni wageni kwa masomo ya mtandaoni. Baada yako kuwa na fursa ya kubaini na kujifunza mazoea bora ya kujifunza mtandaoni, hakikisha umewapa wanafunzi wako maarifa yako kama somo lako la kwanza la mtandaoni. Ikiwa somo hili ni la kutoa maarifa au ndilo somo la kwanza pamoja, hakikisha kwamba wanafunzi wako wanafahamu jinsi ya kutumia mbinu na zana zote, pahali watakapopata nyenzo na kuelewa matarajio yako kuhusu kuhudhuria na kushiriki kwao. Hakikisha kwamba wazazi/walezi/waangalizi wamealikwa ili kujifunza kuhusu teknolojia hiyo na kufahamu matarajio pia.
Orodha Yako ya Ukaguzi ya Vifaa: Kwa kuwa husafiri, hilo halimaanishi kwamba huendi kazini. Kusanya nyenzo unazohitaji kwa ajili ya shughuli za siku hiyo na uzipeleke kwenye eneo utakalofanyia kazi. Hii ni pamoja na zana na nyenzo zitakazotumika — kama vile chaja, penseli, karatasi na vitabu — pamoja na bidhaa za kujistarehesha kama maji, vitafunwa na shashi.
Sawa na hilo, waandikie wanafunzi wako orodha ya bidhaa ambazo zitawasaidia na/au ni muhimu kwao kuweka karibu na uwape orodha hiyo kabla ya somo. Hii itahakikisha kwamba wanafunzi wako wote wanaweza kupata bidhaa zozote zinazohitajika ili kushiriki katika masomo kikamilifu, kuwa na muda wa kutosha wa kusema ikiwa hawatapata bidhaa hizo ili mipango mbadala ifanywe na kwamba mara baada ya somo kuanza, hakuna wakati utakaopotezwa huku wanafunzi wakikimbia kwenye chumba kingine kuchukua daftari.
Fanya Majaribio ya Maikrofoni: Kuendesha somo linalopeperushwa moja kwa moja au lililorekodiwa hufanyika vizuri zaidi kwa kutumia kisikizi kizuri chenye maikrofoni na katika mazingira yenye ukimya. Ikiwa una nafasi au unapenda kutembeatembea, tumia kifaa cha maikrofoni na kisikizi kisicho na waya ili sauti yako ibaki sawa hata kama umesimama ili kueleza sehemu fulani ya somo. Kabla ya kuanza somo au kuanza kurekodi, fanyia vifaa vyako majaribio katika eneo utakalotumia ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wataweza kukusikia moja kwa moja, kwamba hakutakuwa na miangwi au usumbufu usiotarajiwa na kwamba faili unazorekodi zinasikika vizuri na ni rahisi kuelewa.
Fanya Mazoezi ya Kutumia Mfumo Wako: Tenga muda wa kufanya mazoezi ya kutumia mfumo wa masomo ya mtandaoni na kufanya marekebisho yoyote yanayohitajika. Hakikisha kwamba kimo cha kamera/kompyuta yako kitawezesha kuonekana vizuri kwa sura yako na kwamba maikrofoni yako imewekwa katika pahali ambapo inanasa sauti yako vizuri zaidi. Chukua muda wa kuhakikisha una ufahamu mzuri wa kuzungumza kwenye kamera, kutumia mfumo wa kuwasilisha na kubadilisha kati ya skrini ya mapeperusho ya moja kwa moja na slaidi, video na zana zingine. Pia unaweza kurekodi masomo yako (hata ikiwa unafundisha moja kwa moja) ili uyapitie baadaye na utambue sehemu zinazohitaji kuboreshwa kwa maudhui na uendeshaji wa mafundisho.
Kagua Kabla ya Kuanza: Ikiwa unarekodi somo, hakikisha kwamba una nafasi ya kutosha kwenye simu/ kipakatalishi chako ya kuhifadhi faili hiyo. Hifadhi picha na video zako katika kifaa kingine ili kutengeneza nafasi, kama itahitajika. Ikiwa unapeperusha moja kwa moja, basi inapendekezwa sana kwamba upime kasi ya muunganisho wako wa intaneti. Hakikisha una soketi ya umeme karibu yako utakayotumia.
Ondoa Vizuizi vya Ufikiaji: Mifumo mingi ya mikutano na mafundisho ya video ina mipangilio ya tafsiri ya mazungumzo, kubadilisha matini kuwa sauti au zana zingine zilizo ndani ya mifumo hiyo za kusaidia wanafunzi kwa mahitaji tofauti ya ufikiaji. Angalia machaguo yaliyopo kwenye mfumo wako ili uwasaidie wanafunzi wako kuyawezesha.
Jiandae kwa Ajili ya Hitilafu za Teknolojia: Ikiwa wanafunzi wako watakuwa na tatizo la kuunganishwa, ni vyema kuwa na hifadhi ya shughuli huru na masomo yaliyorekodiwa, au yasiyo ya moja kwa moja yaliyotengenezwa ambayo yanaweza kutumika kwa urahisi ikiwa kutatokea hitilafu za miunganisho au teknolojia. Video fupi zilizorekodiwa kabla, mafundisho au mazoezi ya kasi yanayohusiana na somo hilo, au nyenzo zingine ambazo wanafunzi wanaweza kutumia katika hali ambapo hitilafu itatokea zitahakikisha kwamba hakuna muda wa masomo utakaopotezwa huku wanafunzi wakisubiri hitilafu hiyo itatuliwe na kwamba wanafunzi watamakinika katika somo. Unaweza kufikiria kutengeneza mkusanyiko wa shughuli sahili zisizo za mtandaoni ambazo wanafunzi wanaweza kujishughulisha nazo ikiwa hamuwezi kuwasiliana kupitia mtandao. Tengeneza melekezo mepesi yanayoweza kufuatwa na wanafunzi, kama vile zoezi la kusoma la dakika 20 au mchezo wa kutafuta na kukusanya vifaa vya nyumbani.
Hakikisha kwamba wanafunzi wana orodha ya shughuli na maelekezo hayo kabla ya hitilafu yoyote kutokea; kwa mfano, kwa kuyasambaza kabla kupitia barua pepe pamoja na mpango wa somo wa kila siku au juma na nyenzo zingine. Katika somo lako la kwanza kuhusu teknolojia, wafundishe wanafunzi wako kuhusu wanachotakiwa kufanya ikiwa watapoteza muunganisho kabisa au kwa kiwango fulani, na urudie utaratibu huu mara kwa mara ili wawe tayari, ili usijikute ukijaribu kufikiria jinsi ya kuwapa maelekezo huku ukijaribu kutatua hitilafu hiyo.