Somo 4: Alama za Reli
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Wanafunzi watajifunza jinsi ambavyo alama za reli zimekuwa ni njia nzuri za kuendesha harakati za kupigania masuala ya kijamii. Wanafunzi pia watafahamu jinsi ambavyo alama za reli katika mitandao ya kijamii zinavyoweza kusaidia kuhamasisha watu kuhusu suala la utetezi na watabuni alama zao za reli na mbinu za kukuza uhamasishaji kuhusu masuala yaliyo muhimu kwao.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
MASWALI MUHIMU
- Watu wengine wametumia vipi alama za reli katika kuhamasishana kuhusu suala fulani?
- Unaweza kutumia vipi alama za reli ili kukuza uhamasishaji kuhusu suala fulani?
MATAYARISHO
- Tambua video itakayoonesha jinsi ambavyo vyombo vya habari vinavyoweza kutumika kuhamasisha na kutetea masuala yanayoihusu jamii yako.
- Wanafunzi wanahitaji intaneti ili kukamilisha somo hili.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yaendane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizi zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu" katika hati nzima. Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- KUSHIRIKISHWA: Ninatumia teknolojia na mifumo ya kidijitali ili kushiriki katika masuala ya kiraia, kutatua shida na kuleta mabadiliko chanya katika jamii halisi na za mtandaoni.
Kufanya Utetezi kwa Kutumia Alama za Reli
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Wakati mara nyingi watu binafsi hutumia mitandao mahususi ya kijamii katika kampeni za utetezi kwa sababu mahususi, mitandao hii ya kijamii huwa na vipengele vingine vinavyofanana. Kipengele kimoja muhimu kinachotumika sana ni alama ya reli (#). Alama za reli hutuwezesha kuwavutia watu kwa mawazo yetu kwa kuunganisha machapisho yetu na machapisho mengine yanayozungumzia mada hiyo hiyo. Kwa mfano, kama tungetaka kusambaza video za mechi yetu ya kandanda ya hivi sasa ambapo mshambuliaji wetu alifunga mabao matatu, tunaweza kuweka "#football, "#footballinYourStateorCountry" (mfano, "#footballinGhana" au "FootballinLagos") na "#hattrick" kwenye maelezo ya video ili kuwezesha watu wengine wanaotafuta video za kandanda wazione. Kwa njia hii, tunaweza kuongeza uwezekano kwamba huenda video zetu zitaonekana na wataalamu wa michezo wanaotafuta wachezaji bora.
Alama za reli ni muhimu sana katika jitihada za utetezi. Kwa mfano, habari kuhusu kifo cha Iniobong Hiny Umoren, mwanamke aliyetoweka alipokuwa akitafuta ajira katika mji wa Uyo, ulio katika Jimbo la Akwa Ibom, nchini Nigeria, ziliibua hamasa huku raia wa Nigeria wakilalamika kuhusu ukosefu wa usalama nchini humo. Kutoweka kwake kulisababisha watu kuchukua hatua baada ya rafiki yake kuzungumzia kutoweka kwake katika Twitter. Alama ya reli ya #FindHinyHumoren ilisambaa sana na kuziamsha mamlaka ambazo zilifanya uchunguzi na kusaidia kumkamata mhalifu aliyehusika.
Alama ya reli ni aina ya alama katika mitandao ya kijamii yenye uwezo mkubwa wa kufikia ulimwengu mzima. Wakati kundi la kigaidi la Boko Haram lilipowateka nyara wasichana 276 kutoka shule yao ya sekondari katika mji wa Chibok nchini Nigeria, watu nchini humo walijaribu kueneza habari kuhusu suala hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa kuchapisha taarifa mtandaoni zilizokuwa na alama ya reli ya “#BringBackOurGirls.” Suala hilo lilipata uungwaji mkono kwa kasi kutoka ulimwenguni kote, huku watu mashuhuri na wanaojulikana kwa umma wakiunga mkono jitihada hiyo.
Kuna mifano mingine mingi ya matumizi ya alama za reli katika jitihada za utetezi kote ulimwenguni. Kwa mfano, vijana nchini Uganda walitumia “#FreeBobiWine” ili kupinga kunyanyaswa na kutiwa nguvuni kwa mwanasiasa mchanga nchini Uganda. Mgogoro wa Anglofoni nchini Kameruni (na alama ya reli ya #EndAnglophoneCrisis) ulirejea katika habari za dunia mnamo Oktoba 2020 baada ya wanaume wasiojulikana waliokuwa na bunduki kuvamia kampasi ya Mother Francisca International Bilingual Academy mjini Kumba na kuanza kuwafyatulia watoto risasi. Tukio hili lilikashifiwa na kushutumiwa katika mitandao ya kijamii kwa alama ya reli.
DONDOO KWA MWALIMU
Toa mifano zaidi ya alama za reli katika eneo lenu ambazo zinatumiwa kusambaza ujumbe muhimu katika mifumo ya kidijitali. Lengo la mfano huu ni kuwaelimisha wanafunzi kuhusu alama za reli na jinsi zinavyoweza kutumika katika jitihada za utetezi wa suala fulani. Mifano ni kama:
- Kenya: Chuo Kikuu cha Nairobi hutumia #Jiactivate ili kuwahimiza vijana wafuate ndoto zao na kujenga maisha yao kwa njia nzuri zaidi.
- Zambia: Alama ya reli ya #DukuChallenge ilizinduliwa nchini Zambia hivi majuzi ili kuonesha kuunga mkono waathiriwa wa kansa ya matiti, wale ambao wamepona na wale waliofariki kutokana na ugonjwa huo. Kampeni hii ilikua sana kiasi kwamba pia ikajumuisha kansa ya mlango wa kizazi.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Unapofanya utetezi wa suala fulani, kutumia alama za reli ni njia nzuri ya kuhakikisha mawazo yako yanawafikia watu wengi. Katika zoezi lifuatalo, tutaangalia matumizi ya alama za reli katika mitandao ya kijamii.
Zoezi
Sehemu ya 1
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Katika makundi ya watu wawili, tafuteni alama ya reli ambayo imetumiwa hivi sasa katika uhamasishaji kuhusu suala fulani. Baada ya kupata alama ya reli, pitia mazungumzo yaliyo na alama hiyo ya reli, kisha katika timu yako, andikeni muhtasari mfupi wa suala linalojadiliwa. Mtauwasilisha muhtasari huu kwa njia ya mazungumzo kwa kundi zima. Mtakuwa na dakika 15 za kutafuta alama ya reli na kandaa muhtasari.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wape wanafunzi dakika 15 za kukamilisha zoezi hili. Baada ya kumaliza, toa dakika 15 ili kila kundi la watu wawili wawili liwasilishe muhtasari wake kwa kundi zima.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Ni maudhui ya aina gani yanayosambazwa kwa kutumia alama hizi za reli?
- Kuna mazungumzo yanayofanana yanayoendelea ambayo yanatumia alama hizi tofauti za reli? Je, mnadhani kwa nini hili linafanyika/halifanyiki?
- Je, baadhi ya alama nyingine za reli zinazoonekana kuwa na ufanisi mkubwa (mfano., zina uwezekano mkubwa wa kuchapishwa tena) kuliko zingine? Ni zipi? Kwa nini?
Sehemu ya 2
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sasa, njooni na suala ambalo ni muhimu kwa kundi lenu na:
- Mtengeneze alama ya reli ya suala hilo.
- Tengeneza picha, picha yenye taarifa/data, picha ya kuchekesha, chati au grafu ili kutangaza matumizi ya alama yako ya reli.
- Pamoja na mwenzako, jadili njia tofauti mnazoweza kutumia kusambaza alama yenu ya reli mkitumia mtandao wa watu. Ni zipi baadhi ya mbinu nzuri ambazo tumezisoma katika uchunguzaji wa alama nyingine za reli?
Mtakuwa na dakika 30 ili kukamilisha zoezi hili.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wape wanafunzi dakika 30 ili kushiriki katika zoezi hili na wenzao. Baadaye, wape wanafunzi katika makundi yao ya watu wawili wawili dakika 20, ili wajadili alama yao ya reli pamoja na kundi zima, wakitumia picha na michoro, pamoja na mawazo ya kusambaza alama hiyo ya reli.
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa
Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.