Somo 3: Uthibitishaji ni Nini?
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Wanafunzi watajifunza kuhusu maana ya uthibitishaji wa taarifa na kwa nini ni muhimu kwa wapokeaji wa habari kuthibitisha habari wanazosoma au kutazama. Pia watazingatia wajibu wa mashirika ya habari, walengwa wa habari na makampuni ya mitandao ya kijamii katika kukuza mazingira ya usambazaji wa taarifa za kweli.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
MASWALI MUHIMU
- Je, unahisi kwamba, kwa jumla, mfumo wako wa habari za mtandaoni una taarifa za kweli?
- Kwa nini au kwa nini siyo?
VIFAA
- Picha ya Samaki Aina ya Pigfish (inayooneshwa kwenye skrini au iliyochapishwa)
- Vipakatalishi
- Nyenzo za Ziada za Mwalimu Zilizoorodheshwa
MATAYARISHO
- Wanafunzi watahitaji intaneti kwa ajili ya somo hili.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yaendane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizo zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu." Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- NINA UFAHAMU: Ninatathmini usahihi, mtazamo na uhalisia wa midia za kidijitali na machapisho katika mitandao ya kijamii.
Uthibitishaji ni Nini?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Mwaka 2016, tovuti ya World News Daily Report ilichapisha makala kuhusu mpiga picha wa National Geographic ambaye aliliwa akiwa hai na samaki mkubwa wa aina ya sunfish nchini Peru. Kulingana na makala hiyo, Joaquín Álvarez Santos mwenye umri wa miaka 29 alikuwa anapiga picha ndani ya maji pamoja na wapiga mbizi wengine wanne alipomezwa mzima mzima na samaki huyo, aliyekuwa na uzani wa zaidi ya kilo 2000 (tani mbili).
Mmoja wa wapiga mbizi katika shughuli hiyo ya kupiga picha, James C. Wyatt, alisemekana kupiga picha hii kabla ya kisa hicho kutokea. Kabla ya somo letu lijalo, tumieni dakika mbili kutatufa taarifa za tukio hili katika Google ili kuona mambo mtakayopata.
DONDOO ZA MWALIMU
Ikiwa wanafunzi hawana intaneti, wape mfano huo kisha uendelee na zoezi.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Pengine katika utafutaji wenu, mmegundua kwamba makala haya ni ya kubuniwa tu. Kila habari huwa na chanzo, ambacho kinaweza kubainishwa kama mtu, chapisho au wakala iliyonasa picha au yenye taarifa kuhusu kisa cha asili.
Chanzo cha taarifa hii ni tovuti ya World News Daily Report, ambayo ina kanusho linalosema kuwa "inawajibikia kabisa sifa ya tashtiti ya makala zake" na kwamba "wahusika wote walio katika makala za tovuti hii—hata wale ambao msingi wao ni watu halisi—ni wa kubuniwa tu." Hata hivyo, huenda mmegundua kwamba picha hii ni halisi. Ilipigwa na mpiga picha Miguel Pereira, aliyeona samaki mkubwa wa aina ya sunfish kwenye pwani ya nchi ya Ureno (na akaponea chupu chupu) mwaka 2013.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Kwa nini mnadhani tovuti hiyo ilichapisha makala hii?
- Je, mnadhani inafaa kuwe na tovuti inayochapisha maudhui ya kubuniwa tu?
- Je, mnadhani kwamba wasomaji wote watatambua kwamba makala zinazochapishwa na World News Daily Report ni za kubuniwa? Kwa nini/kwa nini siyo?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Je, ni wangapi kati yenu wamesambaza habari katika mitandao ya kijamii hapo kabla? Sasa hivi, watu kutoka kote ulimwenguni wanatoa habari kuhusu matukio katika Facebook, Twitter, YouTube na programu za kutuma ujumbe kama Snapchat na WhatsApp.
Mamilioni ya watu wametumia mitandao ya kijamii kama njia muhimu ya kupanga maandamano na kushirikishana habari (kwa kuchapisha picha/video/taarifa, kusambaza na kutoa maoni). Kufahamu jinsi ya kuchuja na kuelewa taarifa hizi zote ni ujuzi muhimu kwa mtu yeyote anayetaka kutumia habari siku hizi. Ujuzi huu huwa muhimu zaidi kwa sababu watu wanaweza kubuni, kusoma au hata kusambaza taarifa za kupotosha au taarifa bandia bila kukusudia.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, "Mnaweza kufikiria kuhusu matukio (yoyote) ya habari ambapo mlidanganywa na uvumi au picha au video bandia?" (First Draft)
- Lilikuwa ni tukio gani?
- Je, ulijuaje kwamba habari hizo zilikuwa bandia?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Ingawa watu wengine hujaribu kimakusudi kuvidanganya vyombo vya habari, kwa mfano, kuchapisha taarifa katika Twitter kwamba Soko la Hisa la New York lilifurika wakati wa Kimbunga Sandy. Watu wengine huenda wakasambaza taarifa hizo hizo kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na nia njema ya kuwasaidia au kuwajulisha wengine. "Mara nyingi kuna uvumi mwingi wa uongo wakati wa habari za hivi punde kwamba vyumba vya habari vimeanza kutengeneza orodha za taarifa hizo za uongo” (First Draft).
Wanahabari wamefundishwa kutilia shaka kila kitu wanachosikia na kuona — kama ni habari za hivi punde au maudhui yanayoenea sana — hadi watakapothibitisha au kukanusha chanzo.
Katika mkusanyiko huu wa mafunzo, utajifunza jinsi ya kuthibitisha uhalisia wa taarifa kama video, picha, na habari zingine ili uweze kutofautisha ukweli na uongo katika mazingira ya sasa.
Uthibitishaji ni mchakato ambapo shirika la habari au mtu binafsi hukusanya na kutathmini ushahidi ili kupeleleza ikiwa taarifa ni sahihi au la. Ingawa mchakato wa uthibitishaji ulikuwa unatekelezwa husasani na wanahabari na mashirika ya habari, imekuwa mchakato muhimu kwa kila mtu anayetaka kupata habari za kweli za matukio ya sasa. Katika mazingira ambayo kila mtu anaweza kubuni na kusambaza taarifa mtandaoni, hasa katika mitandao ya kijamii, kuweza kuthibitisha uhalisia wa maudhui tunayopokea na kusambaza ni muhimu katika kujenga jamii bora za mtandaoni na kujenga sifa ya uaminifu katika mitandao ya kijamii.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna yeyote aliyesikia kuhusu kuhakiki ukweli au wahakiki wa ukweli hapo kabla?
- Je, mnafikiria wahakiki wa ukweli hufanya nini?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Wahakiki wa ukweli ni watu wanaotambua na kisha kuthibitisha au kukanusha ukweli wa maandishi fulani. Wahakiki wa ukweli wa taarifa kwa kawaida wamekuwa wakifanya kazi katika mashirika ya magazeti, majarida, waandishi au wachapishaji wa vitabu, lakini katika miongo ya hivi karibuni, wamejishughulisha zaidi na uthibitishaji wa maudhui ya kisiasa.
Kama unavyoona katika Makala ya First Draft, wataalamu wanaamini kwamba idadi ya wahakiki wa ukweli ulimwenguni kote itaongezeka katika siku zijazo kwa sababu ya kuongezeka kwa habari zinazobuniwa katika mitandao ya kijamii na watumiaji.
Uthibitishaji ni kutathmini vyanzo visivyo rasmi katika mtandao, ambavyo pia hujulikana kama "maudhui yaliyobuniwa na watumiaji," kwa mfano mtu anapokuwa katika tukio fulani kisha anapakia video ya tukio hilo.
Wahakiki wa ukweli wa taarifa pia huangalia vyanzo rasmi: sera, hati za serikali, hotuba za wanasiasa, n.k. Wahakiki wote wa ukweli hutumia kipengele fulani cha mchakato wa uthibitishaji. Hata hivyo, kama ilivyotajwa hapo kabla, mtu yeyote anaweza kutumia mchakato wa uthibitishaji anaposoma au kutazama habari. Unaweza kutumia tovuti maarufu kama vile Snopes.com, FactCheck.AFP.com, AfricaCheck.org, BBC.com au Aljazeera.com ili kukusaidia kuthibitisha ukweli wa habari utakazoona mtandaoni.
Zoezi
PICHA YA MAZUNGUMZO YA DARASANI
Onesha picha ya samaki wa aina ya pigfish kwenye skrini ya projekta mbele ya darasa. Unapouliza maswali, waulize wanafunzi kwa nini kutambua kwamba picha hii ni ya uongo kuna manufaa kwa machapisho na wanaopokea habari.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Picha hii imesambazwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook na YouTube huku ujumbe unaosema kuwa kiumbe hicho ni “samaki wa pigfish” au “aina isiyo ya kawaida ya hogfish.” Tembelea tovuti ya kuhakiki uhalisia ya Snopes na utazame jinsi wahakiki wa uhalisia walivyothibitisha kuwa picha hii si ya kweli.
Andika kwa ufupi ukieleza kwa nini kutambua kwamba picha hii ni ya uongo kuna manufaa kwa machapisho na wanaopokea habari. Je, baadhi ya matokeo ya kuchapisha taarifa ambazo hazijathibitishwa yanaweza kuwa yapi? Je, unadhani kwamba kuna hali ambapo ni sawa kwa watu kuchapisha taarifa ambazo hazijathibitishwa?
DONDOO ZA MWALIMU
Mfano huu unalenga kuwawezesha wanafunzi kufikiria kwa makini kuhusu picha wanazoona na kujifunza kuhusu jinsi ya kuthibitisha kama ni za kweli au la. Ingawa picha ya samaki wa aina ya pigfish ni mfano mzuri wa picha ya utapeli, tunakuhimiza uchague picha inayotambulika na wanafunzi wako. Ikiwa kuna mfano wa eneo lenu ambao wanafunzi wako wanautambua zaidi, tunapendekeza kwamba utumie mfano huo.
Nyenzo
Tovuti za Kuhakiki Uhalisia
DONDOO KWA MWALIMU
Ikiwa kuna tovuti zingine za uhakiki wa uhalisia ambazo zinatumika katika eneo la wanafunzi wako, tafadhali toa mifano hiyo kwa darasa.
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.