Kuchangamana Kidijitali

Somo 8: Metadata

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo

Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika somo la nyuma, mlijifunza jinsi nakala na picha za vichekesho zinavyotengenezwa kirahisi, kufanyiwa mabadiliko na kusambazwa katika mitandao ya kijamii. Sasa fikiria kwamba wewe ni mwanahabari anayeripoti kuhusu habari za hivi punde. Unaandika makala kuhusu tukio hilo na unaanza kutafuta picha zinazohusiana na tukio hilo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Je, mnadhani kwa nini ni muhimu kwa mwanahabari kupata picha halisi au mtu aliyeipiga picha hiyo?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Ni muhimu kwa wanahabari kutaja vyanzo halisi, mara nyingi iwezekanavyo, wanaporipoti habari ili kuonesha umma kwamba wamefanya uchunguzi mzuri wa habari zao. Kutumia vyanzo halisi na kufuata maadili mema kama kutaja mtu aliyetengeneza picha hiyo husaidia kuhakikisha kwamba wanaopokea habari wanaelewa muktadha halisi wa picha. Picha pia huenda zikawa chini ya sheria mbalimbali za kunakili wakati zinaponakiliwa, kuoneshwa katika chapisho au kutumika na mashirika mbalimbali ya kibiashara au yasiyokuwa ya kibiashara.

Kuthibitisha maudhui halisi na chanzo chake pia huwezesha wanahabari kubaini ikiwa habari fulani ni za kweli au za uongo. Picha za kidijitali, sauti zilizorekodiwa, video, vitabu na midia zingine za kidijitali huwa na metadata, ambayo ni "data kuhusu data." Kila faili la kidijitali lina metadata; metadata ni maelezo ambayo yameambatanishwa kwenye midia yenyewe, na yanaweza kutumika kutafuta, kupanga na kuchuja taarifa katika ulimwengu wa kidijitali.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Unapopiga picha kwa simu yako ya mkononi, unadhani ni maelezo gani ambayo kifaa chako hunasa kuhusu picha hiyo?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Metadata inaweza kuwa na tarehe na wakati ambapo faili lilipigwa picha, maelezo ya eneo ya GPS na pia muundo na/au mipangilio ya kamera iliyotumika kupiga faili hilo.

Data za EXIF, mojawapo ya aina muhimu sana za metadata za picha, inaweza kukujulisha picha ilipigwa na kupakiwa lini na wapi (ikiwa mipangilio ya eneo ya kifaa cha mkononi cha mtu huyo ilikuwa imewezeshwa) (First Draft).

Kuna vitazamaji vya EXIF vya mtandaoni visivyolipiwa kama vile Metapicz, ExtractMetadata.com na Jeffrey’s EXIF Viewer.

PICHA YA MAZUNGUMZO YA DARASANI

Tuangalie metadata ya sampuli ya picha ya papa wa Afrika Kusini.

Bofya kiunganishi hiki. Kisha bofya picha ya papa na mwendeshaji kayaki. Picha hiyo itafunguka katika ukurasa mpya. Angazia kiunganishi cha picha hiyo kisha ukiweke katika Mtazamaji wa Metadata ya Picha ya Jeffrey. BVofya "Mimi sio roboti" kisha chagua kitufe cha "Tazama Data za Picha."

Kagua metadata utakazoona hapa.

DONDOO KWA MWALIMU

Mfano huu unalenga kuwawezesha wanafunzi kufikiria kwa makini kuhusu picha wanazoona na kujifunza jinsi ya kuangalia metadata za picha hizo zinazopatikana. Ingawa mfano wa papa kutoka Afrika Kusini unafaa sana kwa kuonesha mfano wa nakala, tunakuhimiza utumie picha au video ambayo inatambulika na wanafunzi wako. Ikiwa kuna mfano wa eneo lenu ambao wanafunzi wako wanautambua zaidi, tunapendekeza kwamba utumie mfano huo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ni maelezo gani ambayo yamenaswa kutoka kwenye picha hii?
 • Unadhani kwa nini Tarehe ya Kufanyiwa Marekebisho katika jedwali la EXIF ni tofauti na Tarehe ya Kutengenezwa kwenye jedwali la IPTC?
DONDOO KWA MWALIMU

Hiari: Waombe washiriki wawageukie watu waliokaa karibu yao ili kujadili maswali haya katika makundi ya watu wawili wawili.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Je, hii ndiyo picha halisi iliyonaswa na mpiga picha? Tunaweza vipi kuthibitisha maelezo haya?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hatuwezi kuwa na uhakika kamili kwamba picha hii ndiyo halisi ambayo ilinaswa na mpiga picha. Kama ilivyotajwa hapo nyuma, metadata zinaweza kubadilishwa kwa urahisi. Ili kuthibitisha kwamba kweli picha hii ndiyo halisi, mwanahabari anaweza kujaribu kuwasiliana na Thomas Peschak ili kuthibitisha kwamba picha hii ndiyo halisi; mwanahabari huyo pia anaweza kuithibitisha kwa kumuomba Peschak athibitishe metadata tofauti za picha hiyo kama vile tarehe na pahali ambapo picha hiyo ilipigiwa.

Ingawa inaweza kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa uthibitishaji, metadata huwa na mapungufu mengi:

 • Mitandao ya kijamii huondoa metadata, kwa hiyo sharti watu wajaribu kupata faili halisi wanapojaribu kuthibitisha maudhui ya habari fulani. Unapoweka picha zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii katika mtazamaji wa data za EXIF, hutapata matokeo yoyote. Hata hivyo, unapoweka picha halisi uliyopiga kwa simu yako ya mkononi kwenye mtazamaji wa data za EXIF, utapata matokeo.
 • "Metadata hubadilishwa kwa urahisi. Hata unaweza kubadilisha data za EXIF za picha ukitumia simu yako." (First Draft)
 • Video hazina data ya EXIF. Mtazamaji wa data wa EXIF hutumika tu kwa picha halisi.

Jambo la msingi ni kwamba kuangalia metadata ya picha kunaweza kukusaidia kupata maelezo ya ziada, lakini sio mbinu inayokuhakikishia kupata matokeo kamili ya uthibitishaji. Ikiwa sio picha halisi unayotazama, metadata za picha unayotumia hazitakuwa sahihi. Hivyo basi, unapothibitisha uhalisia wa picha za tukio fulani, ni muhimu kutambua chanzo cha picha kwanza kabla ya kuangalia metadata zake.

Zoezi

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa tutazame jinsi sehemu ya mtazamaji wa EXIF inavyofanya kazi kwa picha halisi. Katika zoezi hili, unaweza kutumia picha uliyopiga kwa simu yako au utumie picha kutoka Commons Gallery ya Flickr (flickr.com/commons). Picha kutoka Commons Gallery ya Flickr zinatoka katika mkusanyiko wa picha zilizo wazi kwa umma ambazo hazina makatazo ya haki za kunakili. Ikiwa washiriki wanachagua picha ambayo walipiga wenyewe, wafahamishe wazingatie masuala ya siri. Kwa mfano, washiriki wanaweza kuchagua kutotumia picha zinazoonesha watu.

Pakia picha hiyo katika mojawapo ya sehemu tatu za mtazamaji wa EXIF tulizozungumzia hapo nyuma: Metapicz, ExtractMetadata.com, au Jeffrey’s EXIF Viewer.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Mnaona maelezo gani?

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa chukua picha hiyo hiyo na uifanyie mabadiliko fulani (mfano, kuikata, kuipindua, kubadilisha mwanga au rangi za picha hiyo, n.k.). Pia unaweza kuchukua picha ya picha hiyo. Kisha pakia picha hii mpya kwenye mtazamaji huyo huyo wa EXIF.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Metadata zinabadilika kwa namna yoyote?

Sehemu ya 3

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa pakia picha hii kwenye akaunti yako moja ya mitandao ya kijamii. Kisha chukua picha ya chapisho hili. Pakia picha hiyo kwenye sehemu hiyo hiyo ya mtazamaji ya EXIF.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Metadata zinabadilika kwa namna yoyote? Vipi?

Mjadala

WAULIZE WANAFUNZI WAKO

Fikiria kuhusu metadata mlizoona katika zoezi hili:

 • Ni kwa vipi metadata zinaweza kuwa muhimu kwa wanahabari na wapokezi wa habari?
 • Ni zipi changamoto za kupata metadata sahihi?
 • Je, unadhani kwa nini simu za mkononi/kompyuta hutengenezwa ili ziweze kunasa maelezo haya ya picha? Fikiria kuhusu ni nani anayeweza kufaidika kutokana na maelezo haya.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kama tulivyojifunza, metadata zinaweza kutupatia maelezo muhimu kuhusu picha na chanzo chake, tarehe ya kupigwa kwa picha hiyo, na hata pahali ambapo ilipigiwa. Hata hivyo, metadata zinaweza kubadilishwa kwa urahisi katika simu ya mkononi / kompyuta au kila wakati picha inapopakiwa katika mfumo mpya. Hivyo basi, kuangalia metadata za picha ni hatua moja tu katika mchakato wa uthibitishaji — hatua ambayo kila wakati inafaa kutekelezwa baada ya kutambua maudhui ya asili.

NYENZO

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy