Somo 4: Hatua za Uthibitishaji
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Wanafunzi watajifunza kuhusu orodha ya ukaguzi ya hatua tano wanazoweza kutumia kuthibitisha asili, chanzo, tarehe, eneo na nia ya picha au video. Watatambua matatizo yaliyo katika mchakato wa uthibitishaji na kuanza kufikiria kuhusu zana mbalimbali za mtandaoni na zisizo za mtandaoni wanazoweza kutumia ili kuchunguza uhalisia wa maudhui ya mtandaoni. Wanafunzi watafikiria kuhusu jinsi nia ya chanzo cha taarifa inaweza kuathiri namna ambavyo kisa fulani kitaonekana.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
SWALI MUHIMU
- Je, unawezaje kuhakikisha kama maudhui ya mtandaoni ni ya kweli au la?
- Nia ya mtu fulani (aliyebuni au kusambaza maudhui tena) inaweza kuchangia vipi katika mchakato wa kuthibitisha uhalisia wa maudhui ya mtandaoni?
VIFAA
- Kitini cha "Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji"
- Kitini cha "Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji" - Nakala ya Mkufunzi
- Upatikanaji wa Intaneti
- Nyenzo za Ziada za Mwalimu Zilizoorodheshwa
MATAYARISHO
- Wanafunzi watahitaji intaneti kwa ajili ya somo hili.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yaendane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizo zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu." Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- NINA UFAHAMU: Ninatathmini usahihi, mtazamo na uhalisia wa midia za kidijitali na machapisho katika mitandao ya kijamii.
Hatua za Uthibitishaji
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Uthibitishaji ni mchakato unaotumika sana katika sekta ya habari. Kwa kweli, mashirika kama vile First Draft hutengeneza nyenzo zinazowasaidia wanahabari kuhakiki uhalisia wa taarifa na kupambana vyema zaidi na taarifa za kupotosha. Visa vya mafunzo yaliyo kwenye masomo ya uthibitishaji ni maudhui ambayo yalibuniwa na First Draft.
Leo hii, mtajifunza kuhusu jinsi ya kuthibitisha uhalisia wa taarifa mtandaoni kupitia mchakato wa hatua kwa hatua unaotumiwa na wanahabari katika kazi zao. Unapothibitisha uhalisia wa picha au video mtandaoni, anza kwa kuhakikisha kwamba kisa husika kweli kilitokea. Ukithibitisha kwamba kisa hicho kweli kilitokea, sasa unaweza kufuata Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji ili kuthibitisha uhalisia wa picha au video yako.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji
- Asili: Je, unaangalia chanzo cha maudhui?
- Chanzo: Ni nani aliyetengeneza maudhui hayo?
- Tarehe: Maudhui hayo yalichukuliwa/yalirekodiwa lini?
- Eneo: Maudhui hayo yalichukuliwa/yalirekodiwa wapi?
- Ari: Maudhui hayo yalichukuliwa/yalirekodiwa kwa sababu gani?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Asili:
Fanya ukaguzi huu kwanza ili kubaini ikiwa unaangalia maudhui halisi na sio nakala yake. Kama mtakavyojifunza baadaye katika somo hili, picha au video halisi huwa na maelezo muhimu yanayotumika katika mchakato wa uthibitishaji ambayo nakala au picha za skrini hazina. Hii inaweza kuwa changamoto wakati mwingine, hasa wakati unapochanganua picha za kuchekesha ambazo huwa ni vigumu sana kupata nakala halisi.
Chanzo:
Kama mlivyojifunza kwenye somo la nyuma, kila habari huwa na chanzo, ambacho kinaweza kubainishwa kama mtu, chapisho au wakala iliyonasa picha au yenye taarifa kuhusu kisa halisi. Wakati wa kubaini chanzo, hakikisha kwamba umetofautisha kati ya mtu aliyechukua picha au video halisi na mtu aliyepakia maudhui hayo. Watu wengi hivi sasa wameacha taarifa nyingi za kidijitali mtandaoni na mara nyingi wanahabari hujaribu kuunganisha taarifa wanazopata katika akaunti tofauti za watu kwenye mitandao ya kijamii ili kupata taarifa kama maelezo ya mawasiliano ya mtu fulani au eneo ambalo mtu alikuwa wakati tukio fulani lilifanyika.
Tarehe:
Ingawa inaweza kuwa vigumu kutambua tarehe ambayo picha au video ilichukuliwa (ikilinganishwa na tarehe ya kupakiwa), mashirika ya habari yamekosolewa hapo nyuma kwa kuchanganya tarehe hizi mbili. Kutokana na uvumbuzi wa simu janja, watu wanaweza kuchapisha picha punde tu baada ya kuipiga, lakini hilo halifanyiki kila wakati.
Eneo:
Mitandao ya kijamii huwapa watu uwezo wa kushirikisha eneo fulani kwenye chapisho, lakini taarifa hizi zinaweza kubadilishwa kwa urahisi. Njia bora zaidi ya kuthibitisha eneo la chapisho ni kuendesha mchakato huru wa kulitafuta kwenye ramani au picha ya setilaiti.
Nia:
Kama mnavyofanya katika somo la historia, jitahidi kuelewa mtazamo na nia ya chanzo. Chanzo cha picha au video hiyo ni mtu aliyeshuhudia kisa hicho bila kukusudia? Afisa anayefanya kazi na Umoja wa Kimataifa? Mwanaharakati? Jibu lako la swali hili linaweza kuathiri mtazamo wako kuhusu kisa hicho kwa ujumla.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
- Kwa nini ni muhimu kutambua nia ambayo huenda chanzo cha habari kinayo?
- Ni hali gani zinazoweza kutokea ambazo zitakusababisha kutilia shaka nia za chanzo cha habari?
DONDOO KWA MWALIMU
Kwa wanafunzi wa umri wa chini, unaweza kuwapa mojawapo ya mifano iliyo hapa chini kabla ya kuwaomba wafikirie kuhusu mifano zaidi.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Watu wanaopokea habari huenda wasitake kujua nia ya mwanahabari, lakini ni muhimu kufikiria ni kwa nini huenda waliandika makala hiyo kabla ya kuichukulia kama taarifa ya kweli. Kwa mfano, je, mwanahabari huyo anamsifu mtu anayewania kiti fulani na pia ni jamaa yake na mtu huyo? Je, hilo linaweza kubadilisha jinsi unavyochukulia makala waliyoandika?
Baada ya kumaliza kutumia orodha hiyo ya ukaguzi, mtapata uelewa mzuri kuhusu kiwango cha uhakika wenu mnaposambaza maudhui mtandaoni. Huenda ikawa kwamba una uhakika wa asilimia 100 kuhusu eneo ambapo video ilirekodiwa, lakini huna uhakika wa asilimia 100 kwamba video uliyo nayo ndiyo halisi. Huenda ukawa na shaka kwamba mtu aliyepakia picha fulani siye mtu aliyeipiga. Mchakato wa uthibitishaji wa uhalisia huenda usikupe uhakika kila wakati. Badala yake, ni mchakato ambapo unatafuta vidokezo na mahusiano ya mambo tofauti na ambapo unatumia zana mbalimbali zinazoweza kukusaidia kukusanya ithibati ya kuonesha kwa nini maudhui fulani yanaweza kuaminika.
Zoezi
MAZUNGUMZO YA DARASANI YA VIDEO
Pitia makala iliyo hapa chini na wanafunzi wako. Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili au watatu kisha uwape kitini cha "Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji".
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Rejea "Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji".
Pamoja na mwenzako au kundi lako, jaza kitini cha "Orodha ya Ukaguzi ya Uthibitishaji" kisha ujiulize jinsi unavyoweza kupata jibu la kila swali. Ni zana zipi za mtandaoni au zisizo za mtandaoni zinazoweza kukusaidia? Unaweza kuzungumza na nani? Kuna vidokezo gani kwenye video vinavyoweza kukusaidia?
Hebu tuzumgumzie majibu yetu. Inua mkono wako ikiwa unaamini kwamba kikundi chako kilipata video halisi.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Mnadhani ni tovuti gani iliyo na video halisi?
- Unawezaje kubaini ikiwa video hii ndiyo au siyo halisi?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Picha ya papa kutoka Afrika Kusini ilisambazwa sana katika mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.
DONDOO ZA MWALIMU
Mfano huu unalenga kuwasaidia wanafunzi kuelewa jinsi ya kuthibitisha nakala za picha kwa kufuata hatua za uthibitishaji. Ingawa mfano wa papa kutoka Afrika Kusini unafaa sana kwa kuonesha umuhimu wa kuthibitisha uhalisia wa picha/video, tunakuhimiza utumie picha au video ambayo inatambulika na wanafunzi wako. Ikiwa kuna mfano wa eneo lenu ambao wanafunzi wako wanautambua zaidi, tunapendekeza kwamba utumie mfano huo.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Wakati tukio linatokea, picha na video zinaweza kuongezeka kwa urahisi, huku mtu mmoja akipigwa picha na watu wengi kutoka pande tofauti. Kila mtu anayenasa na kusambaza maudhui fulani huenda akafanya hivyo kwa sababu tofauti. Kwa mfano, picha za tukio hilo hilo zinaweza kupigwa na mwanahabari, mwanaharakati, mtu anayefanya kazi katika eneo hilo au mtu anayesafiri akapita katika eneo hilo wakati wa likizo. Kila picha inayoibuka inaweza kuashiria nia, maoni na pia miegemeo tofauti ya chanzo chake.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Facebook imejitolea kupambana na uenezaji wa habari za uongo katika Facebook.
Facebook inafanya ukaguzi kwa kutumia teknolojia pamoja na binadamu ili kuondoa akaunti za uongo, kuhimiza watu kuchanganua habari kwa makini na kukomesha mapato ya watu wanaotuma ujumbe taka.
Katika baadhi ya nchi, Facebook pia inashirikiana na wahakiki wa nje wa uhalisia ambao wameidhinishwa kupitia shirika huru la Mtandao wa Kimataifa wa Uhakiki wa Uhalisia ili kusaidia kutambua na kukagua habari za uongo.
Kuwa na uelewa wa habari ni kama kuweza kusoma. Lakini mtu aliye na uelewa wa vyombo vya habari anaweza 'kusoma' aina zote za habari — pamoja na vyombo vya habari vya kawaida kama vile televisheni na redio, vyombo vya kuchapishwa kama magazeti, na taarifa zilizo katika intaneti.
Mtu mwenye uelewa wa vyombo vya habari hana uwezo wa kufikia vyombo tu. Pia anaweza kuielewa, kuichanganua, na kufikiria kuihusu kwa makini — na kubuni midia yeye mwenyewe.
Ili kuwa na uelewa wa midia tunahitaji kuweza kufikiria kwa makini kuhusu taarifa hizo ni zipi, zimetoka wapi na kwa nini zimetengenezwa.
Taarifa za kidijitali wakati mwingine zinaweza kufanyiwa mabadiliko ili kubadilisha maana ya taarifa hizo. Hivyo basi, tunahitaji kujifunza jinsi ya kutambua taarifa za uongo na jinsi ya kutofautisha ukweli na maoni ya mtu binafsi.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Ni jinsi gani ya kuripoti taarifa za uongo katika Facebook?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
- Chukua simu yako.
- Angalia chapisho fulani.
- Bofya chini ya chaguo lililo kwenye kona ya juu kulia ya chapisho hilo — huenda ni mshale au nukta tatu.
- Chagua chaguo la 'Pata Msaada au Ripoti Chapisho.'
- Bofya 'Taarifa za Uongo.'
- Ripoti hizi hutusaidia kutambua habari ambazo huenda ni za uongo katika Facebook.
Jambo lingine la kuangalia unapoangalia taarifa ni ikiwa ni chapisho ambalo halijalipiwa au ni tangazo la biashara.
Tangazo ambalo halijalipiwa ni lile lililochapishwa bila malipo na sio tangazo lililolipiwa.
Wakati chapisho lina neno 'imedhaminiwa' katika sehemu yake ya juu, inamaanisha kwamba mtu aliyelichapisha alilipa pesa ili lichapishwe na pia chapisho hilo limepitia ukaguzi wa ziada ili kuhakikisha kuwa sio Taarifa za Uongo.
DONDOO ZA MWALIMU
Jisikie huru kubadilisha mifano iliyo katika slaidi hii ili kuonesha mifano ya machapisho ambayo hayajalipiwa, na matangazo kutoka eneo lenu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Hebu tuone kwa ufupi jinsi unavyoweza kuripoti matangazo au machapisho ya watu kwa kupotosha au kuwa na habari za uongo n.k. katika Instagram.
Kwenye skrini, mnaona chapisho binafsi na chapisho lililolipiwa.
Ili kuripoti chapisho, anza kwa kubofya nukta tatu zilizo kwenye upande wa juu wa kulia wa chapisho hilo.
Sasa unaweza kuona machaguo yaliyopo kwa aina zote mbili za machapisho kwa ajili ya kuripoti.
DONDOO ZA MWALIMU
Jisikie huru kubadilisha mifano iliyo katika slaidi hii ili kuonesha mifano ya machapisho binafsi na machapisho yaliyolipiwa kutoka eneo lenu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Facebook inajitahidi kupunguza uenezaji wa habari za uongo kwa:
- Kutambua habari zauongo: Facebook hutambua habari ambazo huenda ni za uongo kwa kutumia viashirio kama ripoti kutoka kwa watu walio katika Facebook. Wahakiki wa uhalisia huenda pia wakatambua taarifa za kukagua wao wenyewe.
- Kukagua machapisho: Wahakiki wa uhalisia watakagua machapisho, kukagua ikiwa ni ya kweli, na kukadiria usahihi wake.
- Kuonesha taarifa za uongo katika sehemu ya chini ya Mlisho: Ikiwa mhakiki wa uhalisia atakadiria chapisho fulani kwamba ni za uongo, litaonekana chini zaidi kwenye Mlisho. Hii hupunguza idadi ya watu watakaoliona kwa kiasi kikubwa.
- Kuchukua hatua dhidi ya wanaorudia kuchapisha taarifa za uongo: Kurasa na tovuti zinazorudia kusambaza habari za uongo zitapunguziwa idadi ya watu zinaowafikia na pia uwezo wake wa kuweka matangazo utaondolewa.
Sasa tuangazie jinsi tunavyoweza kutambua ujumbe ambao umesambazwa katika WhatsApp.
Wakati ujumbe umesambazwa mara nyingi, huenda chanzo chake kisijulikane. Wakati hujui chanzo chake, unafaa kuthibitisha uhalisia wa taarifa hiyo.
Kama mnavyoona, ujumbe huo huonesha kama ujumbe umesambazwa.
Facebook pia imeongeza vipengele vya ziada vya kutambua taarifa za Uongo.
Mtu anapochapisha taarifa za uongo, inaweza kutambuliwa kisha mtu atakayeiona ataarifiwa wakati atakapoiona kwenye Mlisho.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Facebook pia imeongeza vipengele vya ziada vya kutambua taarifa za Uongo.
Mtu anapochapisha taarifa za uongo, inaweza kutambuliwa kisha mtu atakayeiona ataarifiwa wakati atakapoiona kwenye Mlisho.
Nyenzo
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.