Somo 2: Njia za Kuepuka Kutapeliwa Mtandaoni
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Washiriki watajifunza kuhusu mitindo tofauti ya wasifu na kufanya mazoezi ya kuandika wasifu wakizingatia mambo wanayopendelea, mambo waliyopitia, mbinu mbalimbali na malengo. Washiriki pia watajifunza kuhusu maana ya wasifu na kwa nini ni muhimu katika kufanikisha malengo ya muda mrefu.
Sehemu ya 1
Utapeli kwenye masoko mtandao
Facebook inatoa ulinzi wa “ulinzi wa ununuzi” kwa bidhaa zinazouzwa kwenye soko la ndani ya Facebook na malipo kufanyika hapo. Hata hivyo, Facebook haitoi ulinzi kwa malipo yanafanyika nje ya mtandao (ana kwa ana). Kuwa makini unapoona tangazo la biashara kwenye mtandao wa Facebook, kwani Facebook hairudishi pesa kwa malipo yoyote yaliyofanyika ana kwa ana. Kuwa mwangalifu kila wakati unapotumia malipo ya ana kwa ana kununua bidhaa za Soko la Facebook, hasa ikiwa bidhaa inahitaji kusafirishwa.
Je, ninawezaje kununua na kuuza kwa usalama?
Unapofanya ununuzi kwenye Facebook, tafadhali hakikisha kuwa umeingia kwenye tovuti halisi ya Facebook.
Dondoo muhimu za kununua na kuuza kwenye Soko la Facebook:
- Jihadhari na ulaghai wa kadi ya zawadi
- Wasiliana na muuzaji ndani ya Facebook
- Zingatia njia za usafirishaji zilizopo kwa bidhaa unayotaka
- Usinunue au kuuza bidhaa zilizorudishwa na wateja wengine.
- Jifunze ni bidhaa zipi haziruhusiwi kwenye Soko la Facebook
- Kutana ana kwa ana na muuzaji
- Linda faragha yako
- Tumia njia za malipo mtandaoni na si malipo ya ana kwa ana.
- Epuka kulipa kwa kuhamisha pesa kutoka benki kwenda benki
- Thibitisha bidhaa unayonunua
- Jihadharini na vitu feki
Kuna njia mbili za kununua na kuuza;
1. Lipa kwa Facebook kutoka kwa muuzaji binafsi : Badala ya kutuma ujumbe kwa muuzaji na kupanga kuuziana bidhaa, wanunuzi wanaweza kununua bidhaa hiyo kwa kubofya ‘Nunua Sasa’ au ‘Nunua Usafirishiwe’ kwenye tangazo. Bidhaa hizi zinauzwa na wauzaji binafsi na zinaweza kulindwa na Ulinzi wa Ununuzi, tofauti na mauziano ya moja kwa moja.
2. Mauziano ya Moja kwa Moja : Wanunuzi wanaweza kutuma ujumbe kwa muuzaji na kupanga mauziano ya bidhaa wenyewe kwa wenyewe bila kupitia Soko la Facebook. Kutuma au kupokea vitu hukusaidia kuepuka kuwasiliana na watu moja kwa moja. Bidhaa zilizonunuliwa kwa kuchukua kwa muuzaji moja kwa moja hazilindwi na Ulinzi wa Ununuzi.
Kuna tofauti gani kati ya kulipia bidhaa kwenye soko la Facebook na Mauziano ya moja kwa moja mahali ulipo?
Unaweza kujifunza zaidi kuhusu tofauti kati ya kulipia bidhaa kwenye soko la Facebook na Mauziano ya moja kwa moja mahali ulipo.
Tunapendekeza ufuate miongozo kutoka kwa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kuhusu jinsi ya kuwa na afya bora na kusaidia kuzuia kuenea kwa Virusi vya Korona (UVIKO-19) unaponunua na kuuza. Hakikisha kuwa umeangalia na kufuata sheria na maagizo ya mahali ulipo yanatotumika.
Ikiwa unakutana na mtu ana kwa ana, tunapendekeza mkutane hadharani, eneo lenye watu wengi na mwanga wa kutosha au karibu na kituo cha polisi. Pia ni vyema kutoa taarifa kwa ndugu au rafiki yako kuhusu mahali unapokwenda. Unaweza kutafuta ulinzi kwenye kampuni binafsi za ulinzi. Soma vidokezo vyetu vya kununua na kuuza kwa usalama kwenye Soko la Facebook na kukutana na mtu kutoka kwenye soko ana kwa ana.
Sehemu ya 2
Utapeli wa mapenzi/mahusiano mtandaoni
Mtandao ni mahali pazuri pa kukutana na watu wengine ambao mnaendana katika mambo yanayokuvutia. Hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kupata mpenzi kwenye mitandao ya kijamii. Utafutaji wa wapenzi mtandaoni umekuwa maarufu kwa watu wa rika mbalimbali. Kupitia huduma hizi watu hufanya mahusiano ambayo yanaweza kutengeneza urafiki, mahusiano ya kimapenzi na wakati mwingine ndoa. Hata hivyo, ukichagua kutumia programu au tovuti za mahusiano mtandaoni, kumbuka kwamba mtu yeyote mtandaoni anaweza kusema kuwa yeye ni mtu ambaye siye.
Kwanini uwe makini na mtu unayekutana naye mtandaoni?:
- Picha zao zinafanana na zile za kwenye matangazo au picha za kiofisa. Aina hii ya picha mara nyingi hutumiwa na "walaghai" na zinaweza kuwa picha za mtu mwingine.
- Wanakukosesha raha kwa kusema wana kupenda au wanataka mapenzi yao mara moja kwa kutumia lugha kali.
- Hukukosesha raha kwa kukushinikiza/kukushawishi mbadilishe aina ya mawasiliano, kutoka kwenye tovuti husika na uwasiliane nao kupitia barua pepe au SMS .
Jinsi ya kuwa salama unapotumia mitandao ya mahusiano
Mnapokutana mtandaoni
- Kuwa makini na taarifa unazotoa
- Usiweke taarifa zinazoweza kukutambulisha kwa urahisi hadharani. Usiweke jina lako la ukoo, barua pepe, anwani ya nyumbani, namba ya simu, anwani ya kazini, taarifa zako za benki au taarifa nyingine yoyote ya kukutambulisha kwenye wasifu wako wa mtandaoni au mnapochati kwa meseji.
- Fanya utafutaji wa picha ya mtu unayechati naye.
- Kwa Uhusiano kwenye Facebook: Ripoti na uzuie mtu yeyote anayekuuliza umpe taarifa hizi binafsi, maelezo ambayo yanaweza kuhatarisha faragha au usalama wako, au mtu yeyote ambaye unahisi ana nia mbaya. Hatutamjulisha mtu huyo kuwa umemripoti.
Jihadharini na utapeli
- Matapeli wanaweza kujaribu kutumia akaunti bandia au zilizodukuliwa ili kukulaghai uwape pesa au taarifa binafsi. Ikiwa umepokea ujumbe ambao unaamini kuwa ni ulaghai, ripoti mtu huyo badala ya kujibu.
- Matapeli wanaweza kuomba pesa za kulipia usafiri (nauli), dharura za matibabu, bili za hoteli, bili za hospitali au visa. Kumbuka kwamba mapenzi yoyote ya mtandaoni ambayo yanaomba pesa yanaweza kuwa ya kitapeli.
Viashiria vya Utapeli
- Anataka kuondoka kwenye programu au tovuti mliyokutana na kutaka muwasiliane kupitia barua pepe, SMS au njia nyingine
- Anakwambia kuwa amekupenda haraka sana ili kukushawishi kuzungumza naye zaidi.
- Anafanya mipango ya haraka kukutembelea, lakini anabadili mawazo ya kuja baada ya kupata dharura fulani.
- Anakuomba umtumie pesa, zawadi au kadi za zawadi
- Anaweza kusema amekutumia zawadi nzuri, lakini inahitajika fedha kidogo ili kuituma au kulipia ushuru ili uipate.
Usitume Fedha
- Kamwe, usijibu maombi ya kutuma pesa, iwe kwa benki ay kielektroniki au kutoa mchango. Acha kuwasiliana na mtu yeyote anayejaribu kukushinikiza au kukulaghai ili umwambie taarifa zako za kifedha.
- Wasiliana na benki yako na polisi mara moja ikiwa unaona kuwa umetuma pesa kwa tapeli, na umripoti mtu yeyote anayetaka/omba umtumie pesa. kwa njia ya mtandao.
Kukutana Ana Kwa Ana
Jipe muda, usiwe na haraka ya kukutana.
- Watu wanaweza kudanganya katika wasifu wao wa mtandao wa mahusiano. Uwongo unaweza kuwa ni katika jinsia zao, mwelekeo wa mahusiano wayatakayo au umri wao. Hii inaweza kusababisha madhara au unyanyasaji kijinsia ikiwa utaamua kukutana nao ana kwa ana.
- Endeleza mawasiliano yenu ndani ya programu au tovuti husika (mliyokutana). Pia, fanya utafiti wako na umfahamu mtu huyo vizuri kabla ya kukutana naye ana kwa ana kwa mara ya kwanza.
Dondoo za kuwa salama mnapokutana ana kwa ana;
- Mwambie mtu kuhusu mipango yako: Kila mara mwambie rafiki au mwanafamilia unayemwamini kuhusu mipango yako kabla ya kwenda kuonana na mtu mpya. Mweleze pia eneo unaloenda na muda unaotarajia kurudi nyumbani. Ikiwezekana, unapokutana kwa mara ya kwanza – nenda na marafiki wachache.
- Ruhusu mipangilio ya GPS: Ruhusu rafiki au mwanafamilia unayemwamini aone na kufuatilia simu yako kupitia mfumo wa GPS.
- Kutana hadharani/mahali penye watu wengi: Unapokutana na mtu kwa mara ya kwanza, chagua mahali pa umma ambapo watu wengine wako karibu au karibu na kituo cha polisi.
- Tembelea mahali pa kukutania: Ikiwezekana, tembelea mahali mtakapokutana kabla ya mkutano wengi kuweza kujua usalama wake.
- Zingatia pombe unayokunywa au vilevi vingine: Pombe na vitu vingine vinaweza kuathiri tabia, kwa hiyo fahamu unachokunywa na wanachokunywa watu wengine. Hakikisha glasi yako iko mkononi mwako au unaiona wakati wote.
- Hakikisha kuwa simu yako ina chaji ya kutosha: Hakikisha simu yako ina chaji ya kutosha na upo nayo, iwapo kuna dharura. Unaweza kupanga na rafiki au mwanafamilia akupigie simu ikiwa utamtumia ujumbe wa dharura.
- Panga usafiri wako mwenyewe: Daima panga usafiri wako mwenyewe kwenda na kutoka sehemu ya kukutania ili kuhakikisha kuwa una udhibiti unapofika na kuondoka. Usikubali kamwe kuchukuliwa au kurudishwa nyumbani kwako na mtu unayekutana naye kwa mara ya kwanza.
- Kuwa mwangalifu na maelezo binafsi unayotoa: Kamwe, usione kuwa unawajibika kutoa maelezo au taarifa zako binafsi zinazoweza kukutambulisha kama vile anwani yako ya nyumbani au eneo unapofanya kazi.
Iwapo unajisikia vibaya au hatarini
Ikiwa wewe au mtu unayemjua ni mhanga wa uhalifu au yuko katika hatari, wasiliana na polisi au mamlaka nyingine husika haraka. Iwapo utajisikia kushinikizwa au kukosa raha, unaweza:
- Kumaliza mazungumzo yenu na utumie usafiri wako mwenyewe kurudi nyumbani.
- Kumzuia mtu yeyote anayekukosesha raha
- Kumripoti mtu yeyote unayehisi anatia mashaka.
Sehemu ya 3
Aina nyingine za utapeli
Aina nyingine za utapeli ni pamoja na utapeli wa usaidizi wa kiufundi na wizi wa vitambulisho vya matibabu.
Kompyuta yenye virusi au utapeli wa usaidizi wa kiteknolojia
Kwa kawaida, aina hii ya utapeli hutokea kupitia simu hasa kutoka namba isiyojulikana au ambayo haijasajiliwa, barua pepe au ujumbe ibukizi. Mtu anayedai kuwa yeye ni mfanyakazi wa kituo cha huduma kwa wateja wa kampuni halisi atasema kuwa virusi vimegunduliwa kwenye kompyuta yako. Kisha atakuomba ufuate maagizo ili kuhifadhi au kuokoa data zako, au umpe ruhusa aitengeneze kompyuta yako kutoka huko waliko. Ukikubali, utakuwa umemruhusu kusakinisha programu hasidi kwenye kompyuta yako. Programu hiyo itamfanya aweze kufikia taarifa zako binafsi kama vile za benki au akaunti nyingine na ataiba taarifa hizo. Katika baadhi ya matukio, anaweza kukuuliza taarifa za fedha au kukuhitaji ununue kadi za zawadi ili kuweza kutumia tena kompyuta yako.
Ili kuepuka utapeli huu, kata simu au upuuze ujumbe kisha uwasiliane na kampuni moja kwa moja kupitia vituo vilivyoorodheshwa kwenye tovuti yao ikiwa una maswali au jambo lolote linalokuhusu. Ikiwa una wasiwasi fulani baada ya kuruhusu programu kwenye kompyuta yako, jaribu kuitoa. Ikiwa huwezi, au una shaka, ondoa kebo ya mtandao na uzime WiFi ili kuzuia Internet. Ikiwa unafikiri kwamba kompyuta yako au kifaa kingine kimeambukizwa na programu hasidi kama vile virusi, chunguza mara moja au utafute usaidizi wa kitaalamu.
Wizi wa vitambulisho vya matibabu
Matapeli wanaweza kutumia taarifa zako binafsi zilizoibwa kujipatia dawa walizoandikiwa na daktari, vipimo vya uchunguzi na hata oparesheni. Iwapo hilo litatokea, unaweza kulazimika kulipia gharama hizo (yaani matibabu) ya wezi wa kitambulisho chako cha matibabu na kutumia maelezo yako ya bima za afya. Wanaweza pia kuitumia kukulazimisha uwalipe pesa ili wakurudishie kitambulisho hicho au waache kukuingiza hasara ya kulipia matibabu yao.
Dondoo kuzuia wizi wa vitambulisho vya matibabu
- Kuwa mwangalifu sana kuhusu kutoa bima yako ya afya au kitambulisho cha taifa kwa kampuni au watu wasiojulikana.
- Ingawa watoa huduma za matibabu wanaweza kutaka kuchukua nakala ya kadi yako ya bima, jitahidi kuzuia watu wengine kunakili kadi yako ya bima au kutia saini kwenye fomu ya kudai bima ambayo bado haijajazwa.
- Mara kwa mara, kagua taarifa zako za bima/maelezo ya mnufaika (EOBs).
- Kuwa mwangalifu unaponunua dawa ulizoandikiwa na daktari au vifaa vingine vya matibabu mtandaoni. Ikiwa bei inaonekana kuwa nzuri sana, inaweza kuwa ni utapeli. Pia kuwa mwangalifu kuhusu mahali unaponunua dawa ulizoandikiwa na daktari au vifaa vingine vya matibabu—unahitaji kuwa na uhakika kwamba unachonunua na kupokea ni bidhaa sahihi na sio bidhaa feki inayoweza kuwa haifai, imeisha muda wa matumizi au hatari kwa afya yako kuitumia. Tafuta orodha rasmi ya maduka ya dawa mtandaoni kwenye nchi yako, ikiwa ipo.
Sehemu ya 4
Nani analengwa kwa Matapeli?
Mtu yeyote anaweza kuwa mlengwa wa matapeli, kwa hivyo ni muhimu zaidi kuwa macho wakati wa kufanya biashara au miamala ya kifedha mtandaoni. Kubofya viungo, viambatisho na picha mara kwa mara ndani ya barua pepe kutoka kwa vyanzo visivyojulikana inaweza kukuweka hatarini zaidi, kwani utakuwa unawafahamisha matapeli kuwa unaweza kuathiriwa zaidi na ujumbe wa ulaghai.
Mikakati ya nyongeza kukabiliana na utapeli
- Iwapo bei ya vitu inaonekana kuwa ndogo sana kuliko kawaida, inaweza kuwa utapeli.
- Iwapo kuna shindano, bahati nasibu, kazi, au masomo yanahitaji ulipe pesa kabla ya kupata, usifanye hivyo kwani unaweza kuwa ni utapeli.
- Kuwa mwangalifu kutoa taarifa binafsi kwa watu au mashirika ambayo huyajui na kuyaamini.
- Wasiliana na mtu huyo, shirika au NGO nje ya mtandao moja kwa moja ili kuthibitisha uhalisia kwa kutumia namba ya simu unayojua kuwa sahihi.
Majadiliano/Tafakari
- Je, umekumbana na utapeli wowote mtandaoni hapo awali?
- Je, ulifanyaje?
- Je, kwa sasa utafanyaje?
Masomo ya Nyongeza
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.