Somo 3: Ununuzi salama mtandaoni
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Washiriki wataelewa hatari za kutuma taarifa binafsi zinazoweza kutambulika kwenye tovuti ambazo hazijasimbwa. Watajifunza jinsi ya kulinda taarifa za benki katika program na tovuti za ununuzi na ni tahadhari gani wanahitaji kuchukua wakati wa kukamilisha miamala ana kwa ana.
Sehemu ya 1
Tovuti zilizosimbwa vs zile ambazo hazijasimbwa
Katika Somo la Usalama, ulijifunza umuhimu wa kutumia vivinjari na tovuti zilizosimbwa kwa njia fiche ili kuwa salama mtandaoni. Hebu tuchunguze dhana ya usimbaji fiche kwa undani.
Je, usimbaji fiche unamaanisha nini hasa?
Tovuti kusimbwa kwa njia fiche inamaanisha kuwa data na maelezo kwenye tovuti yamelindwa na hayawezi kutazamwa na watu wengine.
Unapotuma na kupokea taarifa kutoka kwenye tovuti iliyosimbwa kwa njia fiche, taarifa hizo ni salama na zinaweza tu kutazamwa na wewe pamoja na tovuti hiyo.
Tovuti iliyosimbwa kwa njia fiche haimaanishi kuwa hiyo ni tovuti ya kampuni au shirika linalotambulika, kwa hivyo unapaswa kuwa mwangalifu unapotuma taarifa binafsi hata kama tovuti imesimbwa.
Ukiona https:// mwanzoni mwa anwani ya tovuti (badala ya http://), hii inamaanisha kuwa mawasiliano kati ya kivinjari unachotumia na seva ya tovuti imesimbwa kwa njia fiche. Baadhi ya vivinjari vya tovuti huwa na picha ya kufuli ndogo mwanzoni mwa anwani iliyosimbwa kwa njia fiche.
Je, ninawezaje kuitambua tovuti ambayo haijasimbwa?
Tovuti ambayo haijasimbwa haitumii muunganisho wa faragha (uliofichwa). Kwa kawaida, unaweza kutambua tovuti ambayo haijasimbwa kwa kuona "http://" badala ya "https://" mwanzoni mwa anwani ya tovuti. Hii ina maana kwamba mtu yeyote anaweza kutazama taarifa unayotuma au kupokea kutoka kwa tovuti hiyo. Epuka kutuma maelezo yoyote ya binafsi—ikiwa ni pamoja na fedha—kwenye tovuti ambazo hazijasimbwa.
Baadhi ya vivinjari vya mtandao hukupa taarifa unapotembelea tovuti zinazoweza kuwa za hatari. Kuwa mwangalifu sana na tovuti hizi zilizowekwa alama ya hatari. Usiweke maelezo yoyote binafsi na epuka tovuti hizo kwani kufanya hivyo kunaweza kuambukiza kifaa chako na kupakua programu hasidi.
Majadiliano/tafakari
- Je, umewahi kutumia tovuti ambazo hazijasimbwa hapo awali?
- Ulizitumia kwa ajili gani?
- Je, bado ungependa kutumia tovuti hizo hizo sasa? Kwa nini au kwa nini hutapenda?
Kwanini ni muhimu kutumia tovuti zilizosimbwa?
Kutumia tovuti zilizosimbwa kwa njia fiche ni hatua muhimu kuwa salama mtandaoni. Ni muhimu sana kutumia tovuti zilizosimbwa kwa njia fiche unapotuma taarifa za binafsi au zile za kifedha.
Tovuti zilizosimbwa kwa njia fiche hukusaidia kuwa salama unapofanya ununuzi mtandaoni. Hapa mbele, utajifunza zaidi kuhusu ununuzi salama mtandaoni.
Ununuzi salama mtandaoni
Mbali na kutumia tovuti zilizosimbwa kwa njia fiche, kuna mikakati mingine inayoweza kukusaidia kufanya ununuzi salama mtandaoni:
- Nunua kwenye maduka yenye sifa nzuri tu mtandaoni
Kama hujawahi kumsikia muuzaji, tumia muda zaidi kujua kuchunguza biashara hiyo. Biashara ndogo ndogo haziwezi kutoa taarifa rasmi nyingi kama zile kubwa. Unaweza kuwasiliana na mwenye duka moja kwa moja ili upate maelezo zaidi kuhusu bidhaa na huduma wanazotoa ili kuhakikisha kuwa biashara ni halali. Kabla ya kununua kitu kwenye tovuti mpya, fanya utafiti na usome maoni kutoka kwa wateja wengine ili kuona kama duka linajulikana kwa sifa nzuri. Ikiwa huna uhakika kuhusu tovuti ya muuzaji au tangazo, andika anwani ya tovuti ya biashara moja kwa moja kwenye kivinjari chako.
- Usiwe na pupa kwenye kununua.
Kagua bidhaa zote kwa uangalifu kabla ya kulipia. Baadhi ya tovuti zinakupa nafasi ya kubadili mawazo/uamuzi wa kununua, lakini si mara zote. Hakikisha unakagua kwa uangalifu sera na utaratibu wa kurudisha bidhaa kwa muuzaji na kuelewa gharama zote, ikijumuisha ada zozote zinazoweza kutokea au gharama za usafirishaji.
Fuatilia akaunti zako za fedha ili kuhakikisha kuwa hakuna malipo ya utapeli yanayofanyika bila wewe kujua. Ukiona jambo la kutiliwa shaka, liripoti mara moja ili kujilinda dhidi ya utapeli zaidi na gharama za nyongeza.
Sehemu ya 2
Masoko ya mtandaoni
Mtandaoni ni mahali pazuri pa kuunganisha watu wanao uza na kununua bidhaa mbalimbali. Tovuti nyingi za mitandao ya kijamii pia zinajumuisha soko la mtandao linaloruhusu watumiaji kununua na kuuza vitu na bidhaa zao wenyewe kwa wenyewe.
Mikakati ya ununuzi salama katika soko la mtandaoni
Ifuatayo ni baadhi ya mikakati na vidokezo vya kufanya ununuzi kwa usalama katika soko la mtandaoni:
- Hakikisha unasoma miongozo mahsusi ya kila bidhaa kujua nini kinachoruhusiwa kwenye soko husika.
- Unapouza kitu kwenye soko la mtandaoni, mara nyingi tangazo lako huwa hadharani, hivyo linaweza kutafutwa na kuonwa na watu walio ndani na nje ya tovuti. Linda faragha yako na kumbuka kuwa makini ni taarifa gani binafsi unazoweka katika maelezo ya bidhaa na picha zozote utakazotumia.
- Jihadhari na ulaghai wa kadi za zawadi na ofa zinazoonekana kuwa nzuri sana hasa kwa bidhaa kama magari na nyinginezo, ambazo kwa kawaida bei yake huwa juu.
- Kuwa mnunuzi makini, tafiti kama ni bidhaa feki au zimerudishwa kwa muuzaji na wateja kisha ulinganishe bei kabla ya kununua.
- Kumbuka kwamba ukifanya malipo ya moja kwa moja kutoka akaunti yako ya benki iwe kwa muuzaji au mnunuzi, kuna uwezekano mkubwa pesa hizo haziwezi kurudishwa. Pia, hundi zinaweza kuwa feki, hivyo tunashauri utumie njia za kulipa mtandaoni iwapo zipo.
Usafirishaji wa bidhaa
Kuna wakati ambapo, kuna uwezekano wa bidhaa uliyonunua kusafirishwa. Katika hali nyingine, unaweza kuhitaji kwenda kuchukua bidhaa kutoka kwa muuzaji. Hakikisha unabaki salama unapokutana na mtu ana kwa ana ili kuchukua bidhaa zako. Fuata dondoo hizi:
- Usitoe taarifa binafsi kama vile namba ya nyumba. Badala yake, kutana na muuzaji katika eneo lwenye watu wengi, lenye mwanga wa kutosha na wakati wa mchana.
- Mpe taarifa ndugu, mwanafamilia au rafiki juu ya safari yako, mahali unapoenda na muda utakaotumia.
- Ikiwezekana, nenda na mtu mwingine unayemwamini unapofanya makabidhiano ya bidhaa ana kwa ana.
- Hakikisha simu yako ina chaji ya kutosha na muda wa maongezi au kifurushi ili uweze kuwasiliana na ndugu au rafiki iwapo utapata dharura.
Majadiliano/Tafakari
- Je, umewahi kununua vitu kwenye masoko ya mtandaoni? Ilikwendaje?
- Umewahi kununua au kuuza vitu kwenye maduka ya mtandaoni? Ilikwendaje?
- Je, ungefanya jambo tofauti baada ya somo hili? Kwa nini au kwa nini sio?
MASOMO YA NYONGEZA
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Get Safe Online and Digital Promise chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0.