Misingi ya Kidijitali

Somo 3: Nywila

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Maelezo ya Msingi Kuhusu Nywila/Nenosiri

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Mara nyingi hatutilii maanani sana Nywila/Nenosiri tunazotumia katika tovuti, programu na huduma. Hata hivyo, kiwango cha ubora wa Nywila/Nenosiri yako huonesha jinsi taarifa zako zitakavyokuwa salama.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Anzisha mjadala wa wanafunzi kwa kutumia maswali yafuatayo. Tafadhali wakumbushe wanafunzi kwamba ni muhimu kutowapa wanafunzi wengine Nywila/Nenosiri halisi wanayotumia katika zoezi hili au lingine lolote.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Una Nywila/Nenosiri ngapi?
  • Je, una Nywila/Nenosiri tofauti kwa kila akaunti zako za barua pepe na za mitandao ya kijamii?
  • Je, Nywila/Nenosiri hizo ni tofauti sana au zote zina Nywila/Nenosiri zinazofanana?
  • Ikiwa una zaidi ya Nywila/Nenosiri moja, je, unakumbuka vipi kwamba hii Nywila/Nenosiri ni ya akaunti fulani?
  • Ni mara ngapi umesahau Nywila/Nenosiri muhimu?
  • Ulifanya nini baada ya kusahau Nywila/Nenosiri yako?
  • Unafanya nini kuhakikisha kwamba Nywila/Nenosiri yako ni rahisi kuikumbuka?
  • Je, kuna Nywila/Nenosiri unayoitumia kila siku?
  • Ni nini kitatokea iwapo — mtu mwingine — ataijua Nywila/Nenosiri yako bila wewe kujua?
  • Je, itategemea mtu huyo ni nani?
  • Ni aina gani za taarifa ambazo mtu anaweza kuzifahamu kuhusu wewe akitumia Nywila/Nenosiri yako kuingia kwenye akaunti yako?

Sehemu ya 2

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Pamoja na mwenzako, jadilini mambo yanayoweza kufanyika iwapo mtu mwenye nia mbaya ataifahamu nywila ya akaunti ya mtandao wa kijamii uupendao zaidi.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi dakika tano za kujadiliana, kisha uombe makundi yote yazungumzie waliyojadili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa zungumza na mwenzako kuhusu kile ambacho kinaweza kufanyika iwapo mdukuzi ataijua nywila ya akaunti ya benki ya mtandaoni ya mzazi/mlezi wako.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi dakika 5 za kujadiliana. Kisha, yaombe makundi yote yazungumzie mambo yaliyojadiliwa.

Sehemu ya 3

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Huenda unajiuliza jinsi mdukuzi anavyoweza kuijua nywila yako. Kuna njia kadhaa zinazoweza kutumika; njia moja ni kupitia kutumia hila — au kuhadaa mtu ili atoe nywila yake. Mdukuzi anaweza kufanya hivyo kwa kutuma barua pepe ambayo utadhani kwamba kweli imetoka katika mtandao wa kijamii au tovuti ambapo una akaunti. Barua pepe hiyo huenda ikamwomba mtu abofye kiunganishi fulani na kuingia akitumia jina lake la mtumiaji na nywila; baada ya mtu kuingia, maelezo hayo sasa yatamfikia mdukuzi.

Wadukuzi wakati mwingine hujaribu kubuni nywila kwa kutumia mafungu yanayotumika sana sana kama “nywila123,” “jaribu,” au jina lako la kwanza au la mwisho. Njia nyingine ambayo wadukuzi huitumia kupata nywila ya mtu ni kupitia kubuni nywila nyingi tofauti huku wakitumaini kuipata nywila sahihi. Hii hutokea wakati mdukuzi anapojaribu kuingia katika akaunti yako kwa kuzijaribu mara nyingi nywila tofauti. Ingawa mdukuzi anaweza kujaribu nywila nyingi tofauti kwa mikono yake, mara nyingi udukuzi huu hufanywa kwa kuendesha programu ya kompyuta ambayo kwa kasi na kwa njia ya kawaida hujaribu kila mchanganyiko wa nywila unaoweza kufikiria — kwa mfano, orodha ya nywila ambazo huenda unatumia au msururu wa nywila zenye mchanganyiko wa herufi na namba tofauti — hadi atakapopata nywila sahihi.

Bila shaka, namna nyingine za kubuni nywila tofauti hadi kuipata nywila sahihi ni ya juu zaidi. Ikiwa nywila yako ipo katika orodha ya nywila ambazo huenda unazitumia, kama vile “QWERTY” au “12345,” basi programu zingine zinaweza kulikisia haraka zaidi kwa kujaribu machaguo hayo kabla ya yale ambayo uwezekano wa kuyatumia ni mdogo au ambayo ni ya kubahatisha tu. Udukuzi huu unaweza kuwa ni wa juu zaidi ikiwa mdukuzi anajua taarifa fulani kuhusu wewe. Ikiwa, kwa mfano, wadukuzi wanajua jina lako, wanaweza kutumia jina lako pamoja na namba nyingi tofauti mwishoni (k.m., "Adamu2005," au "Adamu3020").

DONDOO KWA MWALIMU

Lengo la mfano huu ni kuwaonesha wanafunzi nywila ambazo ni rahisi kuzidukua, ili waelewe umuhimu wa kutumia nywila ngumu. Mifano ya nywila inaweza kuwa ya kawaida ili iendane na nywila zinazotumika sana katika eneo unalofundisha. Kwa mfano:

  • Ethiopia: hiwot123
  • Kenya: Godslove222
  • Nigeria: QWERTY
  • Zambia: John123

Kanuni za Kutengeneza

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, ni nani kati yenu anayefahamu maana ya kuwa na nywila/nenosiri "ngumu" au "ngumu zaidi"? Kwa nini hili ni wazo zuri?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Nywila/nenosiri ngumu husaidia kulinda taarifa zako. Ingawa kuwa na nywila/nenosiri ngumu hakukuhakikishii kwamba akaunti yako haitadukuliwa, kuwa na nywila/nenosiri dhaifu huifanya iwe rahisi zaidi kwa mtu kuzipata taarifa zako.

Zoezi Kuhusu Nywila

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kuna mifano gani ya nywila/nenosiri dhaifu? Baadhi ya mifano ni kama Nywila/nenosiri; 12345, Hello!, tarehe ya kuzaliwa, jina la utani.
  • Kwa nini unadhani nywila/nenosiri hizi ni dhaifu? Jibu: Zinaweza kubuniwa kwa urahisi na mtu mwingine na/au kompyuta inayoendesha programu ya kubuni nywila/nenosiri hadi kuipata iliyo sahihi.
  • Ni zipi baadhi ya njia ambazo unazoweza kuzitumia kutengeneza nywila/nenosiri ngumu zaidi? Baadhi ya mifano ni kama vile kuongeza namba, herufi kubwa na ndogo, alama, kurefusha nywila/nenosiri, na kuepuka kutumia maneno na mafungu ya maneno yanayotumika sana peke yake.
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Baada ya wanafunzi kuchangia, andika maelekezo haya ubaoni:

  • Weka angalau namba moja.
  • Weka angalau alama moja.
  • Weka angalau herufi moja kubwa na herufi moja ndogo.
  • Nywila/nenosiri zinatakiwa kuwa na angalau herufi 7.
  • Nywila/nenosiri zinatakiwa kuwa rahisi kukumbukwa (isipokuwa kama unatumia mfumo wa usimamizi wa nywila/nenosiri).
  • Mfumo wa usimamizi wa nywila/nenosiri ni tovuti/programu inayosaidia watumiaji kuhifadhi na kuzipanga nywila/nenosiri zao.
  • Nywila/nenosiri hazitakiwi kuwa neno moja tu linalotumika sana au taarifa binafsi (tarehe ya kuzaliwa, jina la mzazi, n.k.).
  • Nywila/nenosiri hazitakiwi kusambazwa katika tovuti.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kuna njia mbili za kutengeneza nywila/nenosiri ngumu. Ya kwanza ni kufuata "menyu ya kutengeza nywila/nenosiri" kama hii iliyo ubaoni. Kutumia mwongozo kama huu hukuhimiza kuweka vipengele vilivyo vigumu zaidi kubuni nywila/nenosiri yenye herufi/nambari, na kuifanya nywila/nenosiri yenyewe kuwa gumu zaidi kuibuni. Tatizo la njia hii ni kwamba inafanya iwe vigumu kukumbuka nywila/nenosiri.

Nywila/nenosiri Ngumu

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Njia nyingine ya kutengeneza nywila/nenosiri ngumu inahusiana na urefu wa nywila/nenosiri. Kwa kuwa ugumu wa nywila/nenosiri unaendana na urefu wa nywila/nenosiri, kutumia msururu wa maneno manne au zaidi yasiyohusiana huifanya nywila/nenosiri iwe ngumu zaidi kubuniwa na watu na hata kompyuta. Njia hii ina manufaa ya ziada kwa kuwa nywila/nenosiri unayobuni kwa njia hii ni rahisi kuikumbuka ikilinganishwa na njia ya kutumia menyu ya kubuni nywila/nenosiri.

Mwisho, mtu anaweza kutumia mchanganyiko wa njia hizi mbili kwa kutafuta msururu wa maneno manne au zaidi yasiyohusiana, na pia kuweka alama na namba. Lengo la njia hizi tofauti ni sawa: kutengeneza nywila/nenosiri ambazo ni za kipekee na ngumu kwa watu wengine kuzibuni.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika makundi ya watu wawili wawili, jaribuni kutengeneza nywila/nenosiri ngumu kwa kutumia maelekezo mliyoyaandika ubaoni hapo kabla. Kumbuka kwamba nywila/nenosiri ambayo ni ngumu kwa kompyuta kuibuni kwa urahisi, huenda ikawa rahisi kubuniwa na binadamu au kompyuta iliyo na orodha ndefu ya nywila/nenosiri zinazotumika mara nyingi. Karatasi yenye nywila/nenosiri yako haitachukuliwa baada ya zoezi hili.

Unahimizwa usitumie nywila/nenosiri hii kwa akaunti yako yoyote, kwa kuwa watu walio kwenye kundi wataifahamu.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi dakika tano za kufanya zoezi hili. Kisha zunguka darasani na uwaulize wanafunzi wanadhani ni ipi mifano ya nywila/nenosiri ngumu zaidi waliyotoa. Waulize wanafunzi ikiwa wanaweza kukumbuka nywila/nenosiri walizobuni bila kuziangalia.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Ingawa tovuti nyingine huhitaji nywila/nenosiri yako ili kutimiza baadhi (au yote) ya masharti haya, nyingine hazina vizuizi vya aina hiyo. Pia unaweza kutengeneza nywila/nenosiri kwa kutumia muunganiko wa maneno yoyote yanayotumika sana.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Katika makundi yale yale ya wanafunzi wawili wawili, tengeneza nywila/nenosiri zinazojumuisha muunganiko wa maneno. Waambie kwamba nywila/nenosiri hiyo inafaa kuwa na angalau maneno manne ili iwe ngumu na pia rahisi kukumbuka. Wape wanafunzi dakika tano za kufanya zoezi hili. Kisha zunguka darasani na uwaulize wanafunzi wametoa mifano ipi ya nywila/nenosiri.

Kwa mara nyingine, wakumbushe wanafunzi kwamba karatasi hazitakusanywa baada ya zoezi hilo, na hawatakiwi kuitumia nywila/nenosiri hiyo katika akaunti zao zozote.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Tovuti nyingine hutumia mfumo wa uthibitishaji wa vipengele vingi (au viwili) ili kuthibitisha utambulisho wako. Tovuti hizi mara nyingi hutumia ujumbe wa maandishi, programu au barua pepe ili kutuma neno au tarakimu zinazotumika mara moja ambazo sharti ziwekwe pamoja na nywila.

Njia hii inaweza kuhakikisha akaunti zako ziko salama zaidi kwa kuongeza safu ya ziada ya usalama ambayo ni ngumu zaidi kupenya. Kwa mfano, ili kuingia katika akaunti yako, sharti mtu awe na nywila yako na pia programu, kifaa au barua pepe inayohusishwa na akaunti hiyo.

Kuweka Usalama wa Nywila/nenosiri

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hata ukitengeneza nywila/nenosiri ambayo ni ngumu sana kwa kompyuta au mtu kuigundua, kuna njia nyingine zinazofanya nywila/nenosiri kuwa dhaifu.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kuna njia zipi nyingine zinazofanya nywila/nenosiri kuwa dhaifu? Baadhi ya mifano ni kama kutumia nywila/nenosiri moja katika akaunti nyingi, kutumia nywila/nenosiri ambayo ina taarifa binafsi, kutumia nywila/nenosiri moja kwa miaka mingi na kuisahau nywila/nenosiri yako.
  • Je, ni mara ngapi unatakiwa uibadilishe nywila/nenosiri yako?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hata nywila/nenosiri ngumu zinaweza kuchukuliwa au kuibiwa, lakini kuna mambo ambayo unaweza kufanya ili kujilinda. Ikiwa kuna data zilizovuja kutoka kwenye tovuti ambapo una akaunti, hakikisha umebadilisha nywila/nenosiri yako kwenye tovuti hiyo pamoja na tovuti nyingine ambazo unatumia nywila/nenosiri hizo. Kukumbuka nywila/nenosiri nyingi ndefu na ngumu zinaweza kuwa ngumu.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, unadhani ni vizuri kuandika nywila yako katika karatasi au kwenye faili la kwenye kompyuta yako?
  • Kwa nini au kwa nini siyo?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Taja hali zinazoweza kutokea kama vile mtu akipata karatasi hiyo au kuliona lile faili kwenye kompyuta yako. Eleza kwamba njia mojawapo ni kutumia mfumo wa usimamizi wa nywila, ambayo ni programu inayowasaidia watumiaji kuzihifadhi na kuzipanga nywila zao.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kila siku, tunatumia akaunti nyingi tofauti katika tovuti tofauti. Kuingia na kuondoka katika kila tovuti kila wakati kunaweza kuwa kazi ngumu.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Umewahi kutumia kipengele cha "hifadhi nywila" katika kivinjari chako ili kuhifadhi nywila kwa ajili ya tovuti fulani? Kwa nini au kwa nini siyo?
  • Je, unaelewa jinsi tovuti inavyokumbuka wewe ni nani?
  • Omba ufafanuzi. Kisha eleza kwamba tovuti zinaweza kukumbuka kwamba uliingia kwa kuhifadhi kidakuzi. Vidakuzi ni faili ndogo zinazohifadhiwa kwenye kompyuta yako ili kusaidia tovuti kufahamu wewe na kompyuta yako ni nani unapotembelea tovuti hizi baadaye, bila kuhitajika kuingia upya. Hata hivyo, vidakuzi vinaweza kutumika kukufuatilia unapotoka katika tovuti moja hadi nyingine. Hii ni moja ya njia inayotumika kukuonesha matangazo yanayoweza kukulenga.
  • Je, ni sawa kuhifadhi nywila ikiwa imo kwenye kompyuta yako?
  • Kompyuta yako ina nywila ya kuingilia? Itakuwaje iwapo unatumia kompyuta hiyo pamoja na watu wengine?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika hali hii, ingawa nywila yako kwenye sehemu ya kuweka nywila huenda ikafichwa kwa nukta au nyota nyeusi, watu wengine wanaotumia kompyuta yako wanaweza kufahamu nywila unayotumia. Kwa kuwa tu huwezi kuona nywila kwenye skrini haimaanishi haijahifadhiwa mahali.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kuna wakati wowote ambao ni sawa kuwapa wengine nywila yako? Lini? Kwa nini? Baadhi ya mifano ni kama wakati ambapo wazazi wao huenda wakataka nywila za simu zao za mkononi au wakati wanatumia nywila moja ili kujiunga kwenye Wi-Fi nyumbani au kwenye huduma kama vile ya Netflix.
  • Je, kuna mtu yeyote unayempa nywila yako? Kama ndivyo, ni nani/kwa nini?
  • Ikiwa wewe ni rafiki wa karibu na mtu mwingine, akisema "ikiwa unanijali..." hilo litakusukuma kumpa nywila yako? Kwa nini au kwa nini siyo?
DONDOO KWA MWALIMU

Mfano huu unakusudia kuwaonesha wanafunzi tovuti zinazotumika sana ambazo watu huenda wakadhani kuwa ni sawa kuwapa wengine nywila za tovuti hizo. Mifano ya nywila inaweza kuwa ya kawaida ili iendane na nywila zinazotumika sana katika eneo unalofundisha. Kwa mfano:

  • Kenya: Showmax, Viusasa
  • Zambia: DSTV

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Unaweza kuchagua kumpa mtu unayemjali nywila yako, lakini kumjali hakumaanishi kwamba ana haki ya kupata namna ya kuingia kwenye akaunti zako za mtandaoni.
Fikiria kwa makini kuhusu uhusiano wako na mtu huyo kabla ya kumpa nywila, ikiwemo namna uhusiano huo unavyoweza kubadilika baada ya muda. Kwa mfano, kumpa mzazi/mlezi nywila yako ni uamuzi tofauti sana na kumpa rafiki yako mkubwa.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ni nini kinachoweza kutokea ukiwapa watu wengine nywila yako? Baadhi ya mifano ni kama mtu anaweza kudukua akaunti zako za benki, kuiga utambulisho wako mtandaoni au kugundua baadhi ya siri zako.
  • Ikiwa unatumia nywila la akaunti fulani na mtu mwingine, je, utaitumia akaunti hiyo kwa njia tofauti?
  • Je, kuna mambo ambayo usingependa kutazama katika Facrebook au kuandika katika ujumbe wa WhatsApp ikiwa mtu mwingine anaweza kuona ulichokuwa unafanya?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wanafunzi wanapaswa kufikiria kuhusu mwenendo wao wenyewe wanapotumia akaunti moja pamoja na watu wengine. Wanapaswa kufahamu kwamba shughuli zao katika mtandao zinaweza kuonwa na watumiaji wengine wa akaunti hiyo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ikiwa akaunti yako inawakilisha taswira yako, kama vile wasifu wa mtandao wa kijamii, je, ni sawa kuwaruhusu watu wengine kutumia akaunti yako?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Jadili uwezekano wa mtu mwingine kujifanya ni wewe na kutuma ujumbe kwa marafiki zako.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, unaruhusu vifaa vyovyote unavyotumia vihifadhi nywila yako? Kwa nini au kwa nini siyo? Je, hiyo inamaanisha kwamba ni salama kuhifadhi nywila yako katika simu au kompyuta yako binafsi? Ni kipi kitatokea ikiwa utaruhusu rafiki yako ataazima simu au kompyuta yako?
  • Je, kuna vifaa vyovyote unavyotumia pamoja na watu wengine, kama vile familia au marafiki? Mnatumia akaunti fulani kwa pamoja katika kifaa hicho au kila mtu ana akaunti yake?
  • Unatumia vifaa vya "umma", kama vile kile kilicho katika maktaba, shuleni au mahali pengine? Katika kifaa hicho, unafanya mambo sawa na yale ambayo huenda ungefanya katika kifaa kingine?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika makundi yenu, jadili iwapo mmewahi kuingia kwenye kompyuta katika shule, maktaba au katika mazingira mengine ya kijamii kisha mkaona kwamba mtu mwingine alikuwa bado hajaondoka katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii au barua pepe. Waulize kama wangefikiria kuangalia ndani ya akaunti hiyo au kufanya kitu kingine.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi dakika tano za kujadiliana, kisha uwaombe wazungumzie waliyojadili. Shiriki mjadala kwenye kundi hilo kuhusu matumizi hayo yasiyo na ruhusa.

Uingiaji wa kwenye Akaunti Bila Ruhusa

Sehemu ya 1

Tafadhali kumbuka: Sehemu ya maelezo ya zoezi hili yamezungumziwa katika “Zoezi #1: Maelezo ya Msingi Kuhusu Nywila.” Tunakuachia ufanye uamuzi mwenyewe kuhusu kama ungependa kupitia maelezo haya tena au utayaruka.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Inawezekana kwa wengine kuingia katika akaunti yako, bila hata ya kuijua nywila yako au kuweza kuibuni kwa bahati. Ikiwa mtu anajua taarifa binafsi za kutosha kuhusu wewe, anaweza kuibuni nywila yako akitumia taarifa hizo, au anaweza kumfanya mtu aliye katika kampuni fulani ampe taarifa zako. Kwa kuwa hatumii teknolojia ili kuingia katika akaunti zako, aina hii ya kuingia katika akaunti inaitwa udukuzi wa kijamii au uhadaifu wa kijamii.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Inua mkono wako kama umewahi kusahau nywila yako kwenye tovuti fulani. Je, nini kinatokea unapobofya "nimesahau nywila yangu?" Baadhi ya mifano ni kama vile: Kwa kawaida tovuti huomba majibu ya maswali ya usalama au itajaribu kuwasiliana nawe kupitia namba ya simu au barua pepe.
  • Je, ni yapi baadhi ya maswali ya usalama ambayo tovuti huomba? Eleza jinsi baadhi ya maswali haya ambayo marafiki au watu unaowafahamu wanaweza kujibu au kubuni, kama mlo wanaopenda zaidi, mahali walipozaliwa, jina la ukoo la mama zao, jina la mwalimu wa Shule ya Msingi au Sekondari wanayempenda zaidi, majina ya marafiki zao wakubwa zaidi, au timu ya michezo wanayopenda zaidi.
  • Ni nani mwingine ambaye huenda anafahamu taarifa za aina hii kuhusu wewe?
  • Tovuti huwasiliana nawe vipi wakati unapokuwa umesahau nywila? Ni nani mwingine ambaye huenda akayapata mawasiliano yako?
  • Mtu usiyemfahamu anawezaje kuzijua taarifa binafsi zinazohusiana na majibu yako ya maswali ya usalama? Baadhi ya mifano ni kama machapisho katika mitandao ya kijamii, kutafuta taarifa za umma mtandaoni, kubuni mara nyingi, kuwasiliana na marafiki zako n.k.
  • Je, kuna mifano gani ya machapisho katika mitandao ya kijamii yenye taarifa binafsi? Kwa mfano, picha iliyo na maelezo ya eneo ulipopigiwa picha hiyo.
  • Unawezaje kutumia Google kujua zaidi kuhusu mtu fulani na kuidukua nywila yake? Baadhi ya mifano ni kama vile: Ikiwa injini ya utafutaji itakuonesha akaunti ya mtandao wa kijamii ya mtu fulani pamoja na maelezo yake yote binafsi kama vile tarehe ya kuzaliwa, jina la rafiki yake mkubwa, majina ya shule zote ambazo alisomea na chapisho kuhusu mwalimu anayempenda zaidi au gazeti la mtandaoni linapochapisha picha ya mtu akishinda tuzo kwa ajili ya shule yao huku mwalimu wake akisimama kando yake katika picha hiyo. Unaweza kufahamu jina la mwalimu ambaye mtu fulani anapenda zaidi pamoja na maelezo zaidi kwa kufanya utafutaji rahisi tu katika mtandao.

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kuchapisha taarifa zilizo na majibu ya maswali yako ya usalama kunaweza kukuhatarisha sana. Hakikisha kwamba unachagua maswali ambayo wewe tu ndiye unayejua majibu yake.

Pia unaweza kubuni majibu ya maswali ya usalama, ilmradi tu utayahifadhi katika mfumo wa usimamizi wa nywila au ni majibu yaliyo rahisi kukumbuka. Tovuti zinaweza kuwasiliana na watumiaji kupitia namba ya simu au barua pepe inayohusishwa na akaunti ya mtumiaji. Iwapo mtumiaji ataisahau nywila yake, mara nyingi tovuti hutoa nywila ya muda mfupi au kiunganishi ambacho mtumiaji anaweza kutumia ili kuweka nywila mpya.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, hii ni njia salama ya kuhakikisha kwamba mtu anayeomba nywila mpya ndiye mtumiaji halisi?
  • Vipi ikiwa unatumia anwani hiyo ya barua pepe inayohusishwa na akaunti hiyo pamoja na mtu mwingine? Baadhi ya mifano ni kama vile: Njia ya kutumia kiunganishi cha kuweka nywila mpya huwa salama mara nyingi, lakini ukiwa unatumia akaunti au nywila kwa pamoja na mtu mwingine, kutumia njia hii kutakuhatarisha.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Udukuzi wa kijamii unaweza kufanikishwa kwa kuwasiliana nawe moja kwa moja na kujaribu kukuhadaa utoe taarifa zako. Wakati mwingine, watu watakutumia barua pepe huku wakijifanya mtu mwingine (kama rafiki, mtu wa familia yako au mhudumu wa benki) na kukuomba umpe taarifa muhimu (kama vile tarehe yako ya kuzaliwa) ili kuthibitisha utambulisho wako.

Udukuzi huu pia unaweza kutumia ujanja zaidi, kama mtu akidukua akaunti ya mtandao wa kijamii ya rafiki yako kisha akutumie ujumbe (pengine pamoja na watu wengine) akikuuliza tarehe yako ya kuzaliwa au pahali ulipolelewa. Ukipokea ujumbe kutoka kwa rafiki yako unaodhani sio wa kawaida, kwanza ni vyema uwasiliane na rafiki yako (bila kutumia mtandao huo wa kijamii) ili kubaini ikiwa kwa hakika yeye ndiye aliyetuma taarifa hizo.

Udukuzi unaotumia barua pepe au tovuti zinazoonekana kuwa halisi unaweza kusababisha wizi wa utambulisho. Kwa mfano, mwizi wa utambulisho anaweza kufungua kadi za mikopo akitumia jina lako na kuzitumia, jambo ambalo linaweza kufanya iwe vigumu kwako kupata kadi ya mikopo baadaye maishani mwako. Udukuzi unaotumia barua pepe au tovuti inayoonekana kuwa halisi ili kupata taarifa unaweza kuruhusu mwizi akuige na apate taarifa zaidi, kumruhusu aangalie barua pepe zako, kutumia marafiki zako ujumbe huku akijifanya ni wewe au kuiba pesa zako. Mchakato huu pia unaweza kumruhusu mwizi huyo akuzuie kuingia kwenye akaunti yako kwa kutengeneza nywila mpya ambayo huifahamu.

Zoezi

Waombe wanafunzi wajibu maswali yafuatayo na waweke majibu yao kwa kutumia maandishi au michoro kwenye kitini cha "Kujifunza Kuhusu Nywila".

  • Ni mifano gani mitatu kutoka kwenye somo hili utakayoitumia wakati mwingine utakapohitaji kutengeneza nywila?
  • Ni katika hali gani moja ambayo unahisi kwamba ni sawa kumpa mtu mwingine nywila yako?
  • Ni mikakati gani mitatu unayoweza kuitumia kuhakikisha unaitumia nywila yako pamoja na ya mtu mwingine katika njia salama?
  • Kuna mifano gani mitatu ya mambo mabaya yanayoweza kutokea iwapo nywila yako itajulikana kwa watu wasiofaa?

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy