Misingi ya Kidijitali

Somo 2: Siri na Wewe

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Soma

Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Mchezo wa Kukisia

Sehemu ya 1

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Sambaza vitini vya “Mchezo wa Kukisia” na uombe wanafunzi wote wavijaze. Waombe wanafunzi wachague taarifa nne ambazo watasambaza na uwajulishe kwamba utasambaza taarifa watakazoandika na kundi zima. Waambie wabaki na karatasi ya pili.
Wape wanafunzi dakika 10 ili kukamilisha kitini hiki. Baadaye, kusanya vitini hivyo.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa nitazisoma baadhi ya taarifa zilizo katika kila kitini. Tumia sehemu ya Makisio ili kuandika kisio lako kuhusu ni mwanafunzi gani aliyejaza kitini gani.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Baada ya kupitia vitini hivyo, anzisha mjadala wa kundi.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kuna taarifa ambazo hukumshirikisha mtu yeyote? Ni zipi? Kwa nini?
  • Je, kila mtu alifanya maamuzi sawa kuhusu taarifa ambazo alisambaza? Kwa nini/kwa nini siyo?
  • Kulingana na mtu unayemshirikisha taarifa, Je, kwa nini huenda ukasambaza taarifa zaidi au za kiwango kidogo za aina hii? Unaweza kuzisambaza wakati gani?
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ilikuwa rahisi vipi kuhusisha kila taarifa na mtu aliyeiandika/aliyeisema?
  • Je, kulikuwa na nyakati ambapo jibu lililotolewa huenda lilitoa taarifa zaidi kimakosa kuliko jibu halisi lililotolewa (mfano, pengine mtu alisema chakula anachokipenda zaidi na hilo huenda liliashiria utamaduni/kabila la mtu huyo)?
  • Je, ni mambo gani unayodhani watu wengine watafikiria kuhusu wewe ikiwa utazisambaza taarifa ulizoandika ulimwenguni kote kama sehemu ya Mchezo wa Kukisia na watu usiokuwa na mahusiano nao ya karibu?

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Siri ni uwezo wa kudhibiti mambo ambayo watu wengine wanafahamu kuhusu wewe. Unaweza kufanya hivi kwa kusema mambo fulani kuhusu wewe (kama vile kuwaambia watu wengine anwani yako au mambo unayopenda kufanya ili kujiburudisha) au kufanya mambo ukiwa miongoni mwa watu wengine (kama vile kwenda dukani na marafiki zako na kununua kitu unachopenda zaidi). Siri ni muhimu uwapo chumbani na watu wengine au unazungumza nao kwenye mtandao.

Siri inategemea na maamuzi yako binafsi. Maana ya siri kwako na familia yako huenda ikawa tofauti sana na maana ya siri kwa watu wengine walio katika kundi hili na familia zao. Ikiwa tutafahamu zaidi kuhusu tunachochukulia kuwa kitu cha binafsi na jinsi tabia zetu katika mtandao zinavyoweza kuchangia hali ya siri zetu, tutaweza kufanya maamuzi mazuri zaidi kuhusu aina za siri tunazotaka. Siri pia hubadilika kulingana na aina ya taarifa zinazosambazwa na pia mtu ambaye unampa taarifa hizo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO

Kwa mfano, unaweza kusambaza mtaa na namba ya nyumba unapoishi na:

  • Wazazi/walezi wako au watu wengine wazima ambao ni muhimu wa familia yako?
  • Marafiki zako?
  • Mwalimu wako?
  • Mtu mgeni kwako au mtu usiyemfahamu vizuri?
  • Rafiki wa rafiki yako?
  • Shirika au kampuni?

Muhtasari

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Unaposambaza taarifa mtandaoni, ni muhimu kuzingatia ni nani anayeweza kuona taarifa hizo na ikiwa wewe au mtu ambaye taarifa zake zinasambazwa anahisi sio tatizo kwake kusambaza taarifa hizo na watu fulani. Baadhi ya taarifa huenda zikasababisha mambo mabaya baadaye ikiwa zitasambazwa kwa watu wasiofaa.
Ikiwa mtu mgeni kwako/mtu usiyemfahamu vizuri anajua pahali hasa unapoishi, basi anaweza kuja nyumbani kwako na hilo linaweza kuhatarisha usalama wako. Ingawa hili ni jambo linaloweza kutokea katika maeneo tofauti ya ulimwengu, hatari (na uwezekano wa kudhurika) huenda ikazidi uwezekano wa kiwango kidogo kwamba jambo hilo litafanyika. Ili kuelewa machaguo ya siri ambayo yatahakikisha usalama wako, unahitaji kuelewa ni zipi athari za kusambaza taarifa.

Mjadala Kuhusu Kutofikisha Taarifa Ipasavyo

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hebu tuzungumzie mambo tunayosema katika ujumbe, jinsi tunavyoyasema na jinsi inavyoweza kuwa tofauti na kuzungumza na mtu ana kwa ana.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kumwambia mtu kwa njia ya ujumbe kunaweza kuwa vipi tofauti na kumwambia ana kwa ana?
  • Jibu linaloweza kutolewa: Ikiwa huwezi kuona jinsi mtu huyo alivyochukulia ujumbe wako, huenda usijue jinsi alivyohisi kuhusu ulichosema. Huenda ukamuumiza mtu bila kufahamu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Unapozungumza na mtu ana kwa ana, unaweza kuona jinsi anavyochukulia unachomwambia, pamoja na ishara za mwili na toni ya sauti. Sehemu za muktadha huo hupotea watu wanapozungumza mtandaoni.

Hata hivyo, kuzungumza mtandaoni kunaweza kukupa muktadha fulani wa taarifa ambazo zinaweza kukusaidia katika mawasiliano (mfano, tovuti huenda zikawa na kanuni mahususi zinazokupa uelewa mzuri zaidi kuhusu jinsi taarifa zinavyoeleweka)

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ikiwa Utakosa baadhi ya vidokezo vya muktadha (mfano, ishara za mwili, toni ya sauti), hii inaweza kusababisha vipi maandishi yako au ujumbe mwingine wa mtandaoni kueleweka vibaya na mpokezi (mfano, kichekesho kinaweza kueleweka vibaya na kuumiza hisia za mtu)?
  • Ikiwa ulieleweka vibaya katika mazungumzo ya ana kwa ana, unaweza kufanya nini ili kuondoa hali hiyo ya kutoelewana (mfano, unaweza kuomba msamaha au kuelezea ulichokuwa unajaribu kusema)? Kufanya hivyo kunaweza kuwa tofauti vipi (yaani, kuwa vigumu au rahisi zaidi) iwapo ulitumia ujumbe wa maandishi?

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Ingawa hatuwezi kuepuka kuacha alama za shughuli zetu za mtandaoni, kuna njia tunazoweza kutumia kuzidhibiti siri zetu na kusimamia sifa zetu za mtandaoni. Katika muktadha wa mitandao ya kijamii mara nyingi kuna mipangilio iliyo katika mitandao hii inayoturuhusu kuchagua ni nani anayeweza kuona tunachochapisha. Ingawa kubadilisha mipangilio hii hakuzuii uchanganuzi — ikiwa ni pamoja na uchanganuzi wa metadata — kwa mfano, kutoka kwa wahusika wa tatu (mfano, watangazaji, watafiti au makampuni) na vile vile na tovuti hizo zenyewe, mara nyingi kunaweza kudhibiti mambo ambayo watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wanaweza kuona au taarifa ambazo makampuni au watangazaji wanaweza kuyaona.

Kwa wanaotaka kujua, kimsingi metadata ni data kuhusu data. Metadata inaweza kujumuisha, lakini sio tu mambo kama vile wakati ambapo uliingia katika mtandao wa kijamii, eneo ulilokuwa ulipoingia na taarifa kuhusu watu unaowasiliana nao mtandaoni. Mipangilio ya uslama inaweza kuwa tofauti katika kila mtandao wa kijamii, lakini inatusaidia kuwajua watu watakaoona machapisho yetu. Kwa mfano, mipangilio inaweza kuruhusu machapisho yetu yaonekane kwa watu wote, kwa marafiki wa marafiki zetu tu, kwa marafiki zetu tu, na wakati mwingine kwa marafiki walioteuliwa tu. Aina nyingine za utendaji zinazoweza kuathiriwa na mipangilio hii ni pamoja na sehemu ya eneo la data na ya kusambaza taarifa. Vidakuzi vinavyonuia kuboresha matangazo, na kipengele cha kukamilisha utafutaji vinaweza kusitishwa katika huduma nyingi kupitia kubadilisha machaguo/mipangilio katika kila huduma.

Pia kuna viongezeo vya vivinjari pamoja na huduma nyingine za kidijitali zinazoweza kuimarisha usalama wa siri zako unapotoka katika tovuti moja kwenda nyingine (mfano, kivinjari cha Privacy Badger cha “Usinifuatilie” cha kutoka kwa shirika la Electronic Frontier Foundation).

Sehemu ya 2

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wagawe wanafunzi katika makundi ya watu wawili.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Tumia dakika moja kutafakari kuhusu mitandao yote ya kijamii ambayo kila mmoja wenu ana akaunti. Je, mnafahamu mipangilio yenu ya usalama ya sasa katika kila jukwaa la mitandao hiyo ya kijamii?

Zoezi la Kundi

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hebu tuangalie uwezo tunaopata kutoka kwenye mipangilio hii na kubaini ni ipi inayofaa zaidi, katika hali gani na ni kwenye mitandao gani ya kijamii. Ukiwa peke yako, ingia kwenye mtandao wa kijamii unaotumia na uangalie mipangilio yako ya usalama. Kwa kawaida, mipangilio ya usalama inaweza kupatikana katika mipangilio yako ya akaunti na baadhi ya tovuti pia hujumuisha vipengele vya kipekee vya kukagua usalama wako.

Baada ya kuangalia mipangilio yako ya usalama, zungumza na mwenzako kuhusu mipangilio hii. Je, kwa nini kila mmoja wenu ameweka mipangilio yake jinsi ilivyo? Je, mipangilio ya usalama wakati mwingine huendana na mazingira. Mfano; mipangilio mingine hufaa katika hali moja lakini haifai katika hali nyingine?, Je Umewahi kubadilisha mipangilio yako? Unaibadilisha baada ya muda gani na kwa nini?

Hakikisha kwamba mnaangalia mipangilio ya usalama inayohusiana na kusambaza taarifa na watu wengine kwenye tovuti hiyo, pamoja na ile inayoashiria kiasi cha data ambacho tovuti hiyo na wahusika wake wa tatu (kama watangazaji) wanaweza kupokea. Vyote hivyo ni vipengele muhimu vya kudhibiti mipangilio binafsi ya kidijitali — kwa ajili ya watu wageni kwako/watu usiowafahamu vizuri, marafiki, jamaa na makampuni.

Mjadala

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kwa jumla, je, mipangilio ya akaunti yako inaruhusu taarifa zako kuonwa na umma, mtu binafsi au chaguo lingine?
  • Uliamua vipi kuweka mpangilio huu?
  • Je, mipangilio yako binafsi ya sasa imewekwa jinsi ambavyo unataka iwe?
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ni wakati gani ambapo ni busara kuruhusu taarifa kuonwa na umma, na ni wakati gani ambapo mipangilio ya kuweka taarifa binafsi itafaa?
  • Je, unahisi sio tatizo kusambaza taarifa zako katika mitandao ya kijamii unayotumia au na makampuni yanayoweka matangazo kwenye mitandao hiyo ya kijamii? Kwa nini au kwa nini siyo?
  • Je, mjadala huu unakupa mtazamo tofauti kuhusu mipangilio yako binafsi? Kwa nini au kwa nini siyo?

Zoezi

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa kwa kuwa tumezungumzia siri, yale ambayo watu wanaweza kugundua kwa mujibu wa maudhui tunayosambaza, jinsi ujumbe unavyoweza kueleweka kwa namna tofauti na watu tofauti na kwa nini mipangilio inaweza kuwa zana muhimu katika kuamua yale unayotaka kusambaza na kundi mahususi la watu, basi tutumie ujuzi ambao umepata.

Katika muda wa dakika 30 zijazo, ukiwa peke yako tafakari kuhusu visa vitatu vifuatavyo na uandike jibu la mistari michache kwa kila kisa.

Amina ana umri wa miaka 13 na ameanza kujaribu kuimba hivi karibuni. Anahisi kwamba yeye bado sio mwimbaji mzuri, lakini angependa kuwaonesha marafiki zake jambo hili jipya analopenda sana ili apate maoni yao. Anafikiria kuhusu kuweka baadhi ya video zake akiimba baadhi ya nyimbo anazopenda sana katika mtandao wa kijamii. Je, unapendekeza atumie mtandao upi wa kijamii? Je, anahitaji ruhusa ya wazazi wake? Je, unadhani mipangilio ipi binafsi ni mizuri kwa mtandao huo wa kijamii? Tafadhali eleza kwa nini.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Anna ana miaka 16 na anapenda sana kupika na kubuni vyakula vipya. Ametengeneza vyakula vingi vinavyoliwa katika eneo lake kama vile Supu ya samaki na Mayai ya Kukaangwa na Viazi ambavyo anapenda sana kuvipika. Anna angependa kuwapa marafiki zake na watu wengine wanaopenda kupika viung na kuwafundisha namna ya kuvitumia kupata chakula kitamu kama chake.

Je, unapendekeza atumie mtandao upi wa kijamii? Je, anahitaji ruhusa ya wazazi wake? Je, unadhani mipangilio ipi binafsi ni mizuri kwa mtandao huo wa kijamii? Tafadhali eleza kwa nini.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Fatuma ni msichana wa miaka 18 ambaye amehitimu shule ya sekondari hivi karibuni na anataka kuanza kutafuta kazi mwezi ujao. Anapenda kompyuta na angetaka kupataka kazi katika sekta ya habari na teknolojia. Hata hivyo, hafahamu ni nafasi gani za kazi anazoweza kupata. Anajua kwamba waajiri watataka kuona wasifuwake lakini hajui jinsi ya kuandika wasifuwake vizuri. Angependa kukutana na watu walio na mipango sawa ili apate ushauri na mapendekezo kuhusu jinsi ya kuendelea na mchakato huo. Je, unapendekeza Fatuma atumie mtandao upi wa kijamii? Je, anahitaji ruhusa ya wazazi wake? Je, unadhani ni mipangilio ipi mizuri ya binafsi kwenye mtandao huo wa kijamii itakayomsaidia kutimiza lengo lake? Tafadhali eleza kwa nini.

DONDOO KWA MWALIMU

Lengo la mifano hii ni kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kutambua mitandao tofauti ya kijamii na mipangilio binafsi inayofaa ili kuhakikisha kwamba wahusika wanatimiza malengo yao. Majina na mifano hii inaweza kuwa ya kawaida ili kuendana na majina ya watu yanayotumika sana na hali za kawaida katika eneo unalofundisha. Kwa mfano:

  • Ethiopia: Tsehay, Meskerem na Michael
  • Kenya: Amani, Onyango na Fatuma
  • Nigeria: Obinna, Akpan na Babatunde
  • Zambia: Twaambo, Walusungu na Kayla

Zoezi

Kama inawezekana, wakati mwingine mtakapokutana kama kundi, waombe wanafunzi wajigawe katika makundi yanayofanana ya watu wawili na uombe kila kundi lizungumzie matokeo ya zoezi lao. Wape wanafunzi dakika 30 ili wakamilishe zoezi hili. Zoezi hili linaweza kufanyika darasani au kama kazi ya nyumbani.

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo

Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy