Misingi ya Kidijitali

Somo 1: Utangulizi wa Siri

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Soma


Matayarisho ya Soma


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Mchezo wa Siri

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Gawa kitini cha “Mchezo wa Siri".

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Unafanya maamuzi kuhusu siri zako kila siku, hasa wakati unapoingia mtandaoni na kutumia simu yako ya mkononi au vifaa vingine vya kidijitali. Mara nyingi, huenda usitumie muda mwingi kufikiria kuhusu maamuzi haya. Lakini yote kwa yote huwa namna ya kipekee kuhusu jinsi unavyoielewa dhana ya usiri. Siri ni uwezo wa kudhibiti mambo ambayo watu wengine wanafahamu kuhusu wewe. Unaweza kufanya hivi kwa kusema mambo fulani kuhusu wewe (kama vile kuwaambia watu wengine anwani yako au mambo unayopenda kufanya ili kujiburudisha) au kufanya mambo ukiwa miongoni mwa watu wengine (kama kwenda dukani na marafiki zako na kununua kitu unachokipenda zaidi).

Siri ni muhimu iwe uwapo chumbani na watu wengine au unazungumza nao kwenye mtandao. Siri hutegemea maamuzi yako mwenyewe. Maana ya siri kwako na familia yako huenda ikawa tofauti sana na maana ya siri kwa watu wengine walio katika kundi hili na familia zao. Ikiwa tutafahamu zaidi kuhusu tunachochukulia kuwa kitu cha binafsi na jinsi tabia zetu katika mtandao zinavyoweza kuchangia hali ya siri zetu, tutaweza kufanya maamuzi mazuri zaidi kuhusu aina za siri tunazotaka.

Hivi sasa tutafanya mchezo mfupi kuhusu siri (tafadhali rejelea kitini cha “Mchezo wa Siri") ambao utakusaidia kubaini jinsi unavyofikiria na kuhisi kuhusu siri. Kila mmoja wenu atajaza kitini chake, azunguke nacho darasani na kujitambulisha kwa mwanafunzi mwingine. Kisha wewe na huyo mwanafunzi mwingine mtaulizana maswali kuhusu taarifa zilizo kwenye kitini. Msikionyeshe kitini kwa wale wanafunzi wengine! Kitini chako hakitakusanywa baada ya kukamilika kwa shughuli hii; uko huru kwenda nacho nyumbani au kukitupa ukipenda.

Katika kila mazungumzo, kila mwanafunzi sharti atoe angalau majibu matatu ya maswali ambayo mwanafunzi mwingine ameuliza. Wanafunzi wanaweza kutoa zaidi ya majibu matatu. Wanafunzi pia wanaweza kuchagua aina tatu au zaidi za taarifa wanazosambaza. Kila mwanafunzi atasambaza taarifa kiasi gani? Kila mwanafunzi atasambaza taarifa za aina gani? Sasa tuzunguke darasani tukizungumza!

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Waombe wanafunzi wajaze kitini. Wape wanafunzi dakika 15 za kuzunguka darasani na kuzungumza na wengine. Baadaye, fanya mazungumzo na kikundi kizima kwa kutumia maswali yafuatayo. Mwishoni, hakikisha kwamba wanafunzi wanatupa vitini vyao au kuondoka navyo. Kama mkufunzi wao, usikusanye karatasi hizo.

Mjadala

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kuna taarifa zozote ambazo hukumwambia mtu yeyote? Ni zipi? Kwa nini?
  • Ni taarifa gani ulizowaambia washiriki wengine? Kwa nini?
  • Je, kila mtu alifanya maamuzi sawa kuhusu taarifa ambazo alisambaza? Kwa nini/kwa nini siyo?
  • Kulingana na mtu unayemshirikisha katika taarifa, kwa nini huenda ukasambaza taarifa zaidi au za kiwango kidogo za aina hii? Unaweza kuzisambaza wakati gani?
  • Je, kuna taarifa zozote ulizosambaza katika shughuli hii ambazo usingeshiriki na watu wote unaojua? Kwa nini siyo?
  • Je, taarifa za aina hii ni kwa ajili ya watu wote? Ni za siri? Kwa nini? Je, hali iko hivyo kwa kila mtu?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kama mlivyosikia, watu walifanya maamuzi tofauti kuhusu taarifa ambazo wangesambaza na zile ambazo wasingesambaza. Pia walikuwa na sababu tofauti za kufanya maamuzi yao. Kitu tulichokifanya kilikuwa ni mchezo. Lakini tunafanya maamuzi ya aina hii kila siku katika maisha yetu halisi.

Tunaamua kama tutachapisha au hatutachapisha picha fulani katika mitandao ya kijamii. Tunaamua ikiwa tunataka maelezo maalum ya mawasiliano, kama vile anwani zetu za barua pepe, zionekane kwa watu wote katika akaunti zetu za mitandao ya kijamii au la. Maamuzi yetu huenda yakawa tofauti na maamuzi ya marafiki zetu wakubwa au hata tofauti na maamuzi yetu ya mwezi uliopita. Hata ikiwa tunafanya maamuzi sawa katika nyakati mbili tofauti, huenda sababu za kufanya maamuzi hayo zikawa tofauti. Maamuzi na sababu hizi tofauti zinawakilisha jinsi sisi wenyewe tunavyoelewa dhana ya usiri.

Kwa kifupi, usiri ni jinsi tunavyoamua kutunza taarifa zinazo tuhusu. Taarifa hizi zinaweza kujumuisha sehemu za utambulisho wetu, shughuli zetu, mambo tunayopendelea, kaida za kufanya mambo, pamoja na mambo mengine kuhusu maisha yetu. Katika ulimwengu wa leo wa kidijitali, kuna fursa nyingi zaidi kuliko hapo awali za kusambaza taarifa zinazotuhusu na watu wengine. Kwa hiyo ni muhimu kwamba tufahamu kuhusu uelewa wetu wa siri na kwamba tufikirie kuhusu kama tunaridhishwa na uelewa huo au la.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kwa mujibu wa hulka yako wakati wa mchezo kuhusu siri, pamoja na hulka yako katika maisha ya kila siku, unaweza kusema siri ni nini? Kwa nini?
  • Je, taarifa zote binafsi pia ni siri? Jibu linaloweza kutolewa: Sio lazima.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kwa mfano, siku yako ya kuzaliwa huenda isiwe siri kwa namna unavyoandika kwenye shajara lako. Kuna watu wengi duniani wanaojua siku yako ya kuzaliwa na wanaofaa kuijua, kama vile wazazi/walezi au daktari wako. Kwa kuwa jambo fulani sio siri, bado unaweza kulichukulia kuwa la siri.

Wengi wetu tusingependa kila mtu ajue siku yetu ya kuzaliwa kwa sababu tunaichukulia kama taarifa ambayo inafaa kujulikana na watu tulio na mahusiano ya karibu nao au watu wenye sababu maalum ya kujua taarifa hiyo. Aina hizi za maamuzi kuhusu nani anayefaa kufahamu taarifa fulani kutuhusu, lini, na kwa nini ndizo msingi wa siri.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kuna mambo mengine ambayo huenda sio siri ambayo bado ungependa kuyafanya siri kutoka kwa watu usiowajua vizuri/watu ambao unawajua kwa muda mfupi tu? Baadhi ya mifano ni kama vile namba za simu, barua pepe, picha, video, n.k.
  • Je, kuna mambo mengine ambayo usingependa yajulikane na wazazi/walezi au marafiki zako?
  • Vipi kuhusu walimu wako au wakufunzi wengine? Baadhi ya mifano ni kama vile: matokeo yako shuleni, akaunti yako ya Instagram, shajara lako.
  • Je, umejifunza chochote kuhusu uelewa wako binafsi kuhusu siri ambacho kimekushangaza?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Mnaweza kwenda na karatasi za Mchezo wa Siri baada ya kukamilisha shughuli za leo! Sasa kwa kuwa mnafikiria zaidi kuhusu siri, mtaona fursa nyingi sana za kufanya maamuzi kila siku ambapo mtatumia uelewa wenu binafsi kuhusu siri.

Zoezi

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hivi sasa tutaangalia zaidi uelewa wako binafsi wa siri.

1. Tafuta mifano mitatu mtandaoni ambapo mtu alisambaza au kuchapisha kitu fulani ambacho wewe ungekiweka siri. Unaweza kutafuta kutoka kwa watu maarufu, wanasiasa, au viongozi wa kibiashara au unaweza kutafuta ukitumia alama ya reli au kwa utafutaji wa jumla mtandaoni ili kupata mifano yoyote. Jaribu kutafuta vitu vya aina tofauti (mfano, picha, video, meseji za picha, maoni ambayo mtu alitoa kwenye mtandao wa kijamii na/au mfumo wa mtandaoni wa kituo cha habari) kuhusu mada tofauti.

2. Kwa kila mfano, andika maelezo ya aya moja kuhusu sababu yako ya kuchagua kuweka taarifa hizo kuwa za siri.

Katika aya yako, tafadhali pia eleza ikiwa/jinsi ambavyo maoni yako binafsi kuhusu kusambaza taarifa hizi hubadilika ikilingana na muktadha (mfano, watu unaozungumza nao, idadi ya watu walio katika mazungumzo hayo, nia na lengo, mazingira [shuleni ikilinganishwa na nje ya shule]).

Zoezi hili linaweza kufanyika darasani au kama kazi ya nyumbani.

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy