Kuchangamana Kidijitali

Somo 2: Mahusiano Mazuri ya Mtandaoni

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Msamiati wa Mahusiano

Sehemu ya 1

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wakusanye wanafunzi katika duara.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Leo, nataka kuzungumza kuhusu jinsi mambo tunayoyafanya mtandaoni yanavyoathiri mahusiano yetu. Pia tutazungumza kuhusu yale mnayoweza kufanya ili kuwa "mtetezi" wa wengine na kutambua wakati marafiki zetu wanahitaji usaidizi ili kusuluhisha matatizo yao katika mahusiano.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO

Ni nani ambaye amewahi kusikia kuhusu maneno "mtazamaji" au "mtetezi"? Maneno haya yana maana gani kwako?

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Sikiliza majibu mawili au matatu.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kama mlivyosema, mtazamaji ni mtu anayetazama tukio fulani likifanyika. Kwa ajili ya zoezi la leo, tutazungumzia kuhusu matendo yanayohusiana na mahusiano mabaya/yasiyo na ukarimu. Mtetezi ni mtu anayefanya jambo zuri kwa kujibu tukio fulani — pengine kwa kumsaidia mwathiriwa, kusaidia kukomesha kitendo hicho, au kusaidia kwa namna nyingine, kulingana na hali iliyopo.

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa hebu tuzungumze kuhusu mahusiano.

Kwanza, ni vyema kuelewa kwamba "mahusiano" ni neno pana sana. Kwa ajili ya malengo yetu, tutasema kuwa maana ya "uhusiano" ni namna yoyote ambayo watu wenye umri, vyeo au majukumu sawa wanahusiana. Kwa mfano, huenda ukawa na uhusiano na wenzako kwa njia ya kuwa marafiki, wanafunzi wenza, au wanachama wa kazi moja ya nje ya shule (mfano, klabu ya filamu). Kila tunapozungumza kuhusu mahusiano mazuri, kuna swali tata linaloibuka kila wakati: "Uhusiano mzuri ni nini hasa?" Kila mtu ana maoni tofauti kuhusu mada hii na kuna majibu mengi mazuri.

Ili kuhakikisha kwamba sote tunakubaliana, basi tutafakari kwa kina kuhusu maneno yanayoweza kueleza kuhusu mahusiano mazuri — mahusiano ya kirafiki, wanafunzi wenza na mahusiano ya aina tofauti. Tunafahamu kwamba wakati mwingine mambo yanaweza kuwa mabaya katika mahusiano ya aina zote, kwa hiyo hebu tuzungumze kuhusu tabia nzuri zinazohusiana kwa namna ya kipekee na mahusiano ya aina tofauti.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hebu tucheze mchezo mdogo. Huku tukizunguka katika duara, hebu kila mmoja wetu aseme neno moja linaloelezea mahusiano mazuri. Nitaanza. Nadhani mahusiano yanaweza kuwa (ya kusaidiana, ya kujali, yenye ukarimu n.k.).

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Unafanya nini ili kumsaidia mtu ambaye una mahusiano mazuri naye?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Andika mambo ambayo wanafunzi watasema kwenye chati ya mtiririko wa hatua.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Vizuri sana! Asanteni kwa kuchangia! Hebu sasa tuangalie maneno haya.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Mnakubaliana nayo?
 • Mna maneno mengine ya kuongezea?
 • Kwa mujibu wa maneno haya, kuna mtu anayeweza kutunga maana ya sentensi moja ya mahusiano mazuri?

Ongoza kundi katika kutafuta maana ya pamoja kuhusu mahusiano mazuri.

Kuzunguka darasani na kushiriki

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wagawe wanafunzi katika makundi ya watu wawili wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa kwa kuwa tuna orodha nzuri ya mambo tunayofikiria wakati tunapozungumzia "mahusiano mazuri," ni wakati wa kujikita na kuangalia mambo ya mahusiano ambayo tuliyopitia sisi wenyewe kwenye intaneti.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Andika swali moja kutoka kwenye orodha ya maswali yanayoweza kuibuka iliyo hapa chini kwenye kipeperushi kisha ubandike vipeperushi hivyo kwenye kuta za darasa.

Maswali Yanayoweza Kuibuka:

 • Unamuunga mono nani kupitia teknolojia?
 • Ni mifumo, huduma au tovuti gani unazotumia ili kuwasiliana na watu?
 • Ni kwa vipi intaneti na teknolojia za simu (kama vile vishikwambi au simu za mkononi) zimekupa fursa za kutengeneza au kudumisha mahusiano mazuri?
 • Unaweza kudumisha vipi mawasiliano na watu kwa kutumia vifaa vya mkononi na kompyuta?
 • Kuna changamoto gani zinazotokana na intaneti na teknolojia za simu katika kutengeneza/kudumisha mahusiano mazuri?
 • Kuna mchezo gani wa kirafiki ambao umeuona au kuushuhudia kwa sababu ya mambo yaliyochapishwa mtandaoni?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Nitalipa kila kundi la watu wawili vikaratasi vinavyoweza kubandikwa na kalamu ya wino. Katika vipeperushi vilivyo kwenye kuta za darasa kuna maswali tofauti. Nitakapowapa vifaa vyenu, mnaweza kwenda kwenye vipeperushi hivyo. Andikeni majibu yenu kwenye vikaratasi hivyo vidogo kisha mvibandike kwenye vipeperushi. Ikiwa una zaidi ya jibu moja la swali, andika kila jibu kwenye kikaratasi tofauti kisha mvibandike kwenye vipeperushi. Mna muda wa dakika nane. Ili kufikia vipeperushi vyote, tumia dakika 1-2 kwa kila kipeperushi. Furahieni!

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Kusanya vipeperushi baada ya zoezi hili kisha uombe kundi hilo likusanyike tena.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ni majibu gani yaliyokuwa sawa kwa kila moja ya maswali haya?
 • Kuna mambo yoyote mnayodhani yamekosekana?
 • Kuna mienendo mnayoiona?
 • Teknolojia imeathiri vipi mahusiano yako na marafiki zako?
 • Teknolojia imerahisisha mambo au kuyafanya magumu zaidi? Kwa nini?

Mjadala wa Tukio

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa tutajadili tukio linalohusiana na teknolojia na mahusiano ambalo ni "kutuma ujumbe mwingi kupita kiasi." Kuna mtu anayejua maana ya "kutuma ujumbe mwingi kupita kiasi?"

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Sikiliza majibu mawili au matatu.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kutuma ujumbe mwingi kupita kiasi ni hali ambapo mtu anamtumia mtu mwingine ujumbe mwingi sana kiasi kwamba unamuelemea mtu huyo mwingine.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Kuna mtu ambaye amewahi kutumiwa ujumbe mwingi kupita kiasi?
 • Ikiwa wewe ndiye unapokea ujumbe huo, utafanya nini? Kwa nini?
 • Ikiwa mmoja wa marafiki zako angekujia na kukwambia kuwa anapitia hali hii, ungempa ushauri gani? Ungechukua hatua? Ni hatua zipi tofauti ambazo ungechukua?

Kufuatilia: Kuchukua hatua hizi ili kumsaidia rafiki yako kunaitwa "kumtetea."

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ni nini kinachoweza kumzuia mtu kumtetea rafiki yake?
 • Hebu tuchukulie kwamba mmoja wa marafiki zako anamwambia rafiki yake aache kutuma ujumbe mwingi sana. Ni nini kitakachofanyika ikiwa rafiki huyo ataanza kuja nyumbani kwa mtu huyo kila wakati, huku akiomba kuonana naye wakati wote? Tatizo hilo linaonekana kuendelea kuwa baya zaidi, hali ambayo inaweza kuitwa "kukithiri kwa tatizo." Ni ushauri gani unaoweza kumpa rafiki yako ikiwa tatizo hilo litaendelea kukithiri?
 • Ikiwa tatizo hilo litakithiri, bado utaingilia kati kama mtetezi kwa njia sawa na uliyotumia hapo kabla? Hivi sasa utachukua hatua gani ili kuwa mtetezi?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kumtumia mtu ujumbe mwingi kupita kiasi ni mfano mmoja wa hali ambapo teknolojia inaweza kuleta mahusiano mazuri.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Kuna mifano gani mingine?
 • Baadhi ya masuluhisho ya matatizo haya ni yapi?
 • Mjadala wetu umetufahamisha nini kuhusu jukumu la teknolojia katika mahusiano kufikia sasa?
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Endesha mjadala kuhusu athari chanya na hasi za teknolojia katika mahusiano.

Zoezi la Spektra

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Angalieni tabia mahususi katika mahusiano mazuri na mabaya na pahali ambapo yatakuwa kwenye spektra, kuanzia mahusiano mazuri hadi mabaya. Nitampa kila mmoja wenu kikaratasi kinachoweza kubandikwa. Kwenye kikaratasi hicho kuna jambo linalofanyika katika mahusiano, kama vile "kumtumia mwenzako ujumbe kwa muda wa saa 24/7" au "kubadilishana nywila za mitandao ya kijamii." Baada ya kukupa kikaratasi hicho, ningependa usimame kisha uende mbele ya darasa. Kwenye upande mmoja wa darasa kuna tabia nzuri zaidi katika mahusiano (iliyoandikwa "1") na katika upande wa pili kuna tabia mbaya zaidi katika mahusiano (iliyoandikwa "10").

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Utakapokuja hapa mbele, fikiria kuhusu jinsi tabia iliyo kwenye kikaratasi hicho ni nzuri au mbaya. Kisha fikiriajinsi ambavyo ungekadiria uzuri au ubaya wa tabia hiyo kwa kiwango cha 1 hadi 10. Kwa mfano, ikiwa unaamini kwamba "kumtumia mwenzako ujumbe saa 24/7" ni tabia mbaya kuliko "kuunga na kusambaza kila kitu ambacho marafiki zako huchapisha," basi simama karibu na upande wa "10" au ule wa tabia mbaya.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Mada zinazopendekezwa zilizo kwenye vikaratasi:

 • Kumtumia mwenzako meseji saa 24/7
 • Kubadilishana nywila za mitandao ya kijamii
 • Kusoma ujumbe wa rafiki yako bila ruhusa yake
 • Kuzungumza mtandaoni na watu wageni kwako/watu usiowafahamu vizuri
 • Kuchapisha maoni ya kufedhehesha kwenye chapisho la mtu katika mitandao ya kijamii
 • Kutuma ujumbe wa "usiku mwema" au "asubuhi njema" (pengine kila siku) kwa mtu unayemjali
 • Kuzungumza kuhusu mabishano kati yako na rafiki yako hadharani kwenye mitandao ya kijamii
 • Kuunga na kusambaza tena machapisho yote ya marafiki zako
 • Kuchapisha maudhui katika mitandao ya kijamii ukitumia akaunti ya rafiki yako (yenye jina lake)
 • Kushirikisha marafiki zako kwenye picha za sherehe
 • Kueneza uvumi kuhusu mwanafunzi mwenza katika mitandao ya kijamii
 • Kuchapisha sehemu za mazungumzo ya siri bila kuomba ruhusa

Huku wanafunzi wakija mbele na kujipanga, waulize kuhusu sababu zao za kusimama pahali walipo na uwahimize wanafunzi wazunguke hadi maeneo mengine ikiwa watahitaji kufanya hivyo. Baada ya wanafunzi kumaliza kusimama katika mpangilio wa spektra, waombe wavibandike vikaratasi vidogo kwenye ukuta ulio mbele ya darasa kisha warudi nyuma ili waweze kuona spektra nzima.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Ikiwa wataamua kufanya hivyo, wanafunzi wanaweza kujibu maswali mawili ya kwanza yaliyo hapa chini kwa kujadiliana, baada ya kuandika majibu kwenye vikaratasi na kuvibandika kwenye ukuta ulio mbele ya darasa.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Kuna tabia zozote mbaya mnazoweza kufikiria? Kuna tabia zozote nzuri mnazoweza kufikiria?
 • Je, spektra hii inaweza kupangwa kwa namna moja tu iliyo sahihi? Kwa nini/kwa nini siyo? Nyote mnakubali?
 • Tunaziweka tabia hizi mahususi kwenye spektra, tukianza na zile nzuri hadi zile mbaya. Lakini je, kunaweza kuwa na hali ambapo tabia nzuri zitabadilika na kuwa mbaya? Au tabia mbaya iwe nzuri? Hilo linaweza kufanyika lini?
 • Ikiwa X ni tabia mbaya (chagua tabia maalum ambayo wanafunzi walibandika karibu na upande wa spektra wa tabia mbaya), unaweza kufanya nini ili kuitatua?
 • Unaweza kumzungumzia mtu vipi ikiwa huridhishwi na kitu anachokifanya?

Zoezi

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Leo tumezungumza sana kuhusu teknolojia na mahusiano. Sasa kwa kuwa tumewafanya mtafakari, je, mnaweza kuwaambia wengine yale mliyojifunza? Kuna shughuli za aina gani mnazoweza kubuni ili kuwahimiza wenzenu wawe watetezi iwapo watashuhudia aina yoyote ya tabia mbaya katika mahusiano?

Wagawe wanafunzi katika makundi ya watu watatu au wanne.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Tuna mapendekezo mawili hivi sasa, lakini kama mna mawazo tofauti, mnaweza kuyatoa! Mna dakika 30.
Pendekezo #1: Buni mpango wa tukio linaloweza kufanyika katika shule au jamii yako kuhusu jukumu la teknolojia katika mahusiano. Tukio hili linaweza kuwa onesho la filamu ya matukio halisia/mjadala, kampeni kama vile #EndCyberbullying au hata wasilisho! Toa mifano ya jinsi unavyoweza kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook au Twitter, kutangaza tukio hilo. Una uhuru wa kutumia picha pamoja na mpango wako (mfano, kutumia michoro, picha ya kuchekesha).

DONDOO ZA MWALIMU

Mnapojadili hoja za matukio, zungumzia mifano ya kampeni iliyofanya vizuri katika eneo lenu ili kuwapa wanafunzi ufahamu mzuri wa jinsi ya kukamilisha zoezi hilo. Zoezi hili linalenga kuwafundisha wanafunzi jinsi wanavyoweza kutumia teknolojia kuleta mabadiliko katika jamii yao. Chagua mifano ya kampeni za kidijitali zilizofanya vizuri ambazo wanafunzi wanaweza kurejelea.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Pendekezo #2: Buni kisa kuhusu uhusiano (mfano, uhusiano kati ya ndugu au uhusiano kati ya marafiki shuleni) na jinsi unavyoweza kuathiriwa na mitandao ya kijamii. Mnaweza kuigiza mchezo mfupi, kubuni picha (mfano, mfululizo wa michoro yenye hadithi nzuri) au kuandika Mlisho wa Facebook au gumzo la kubuniwa katika Twitter. Tuwe wabunifu!

Zoezi

Sehemu ya 2

Baada ya muda wa dakika 30 kuisha, yaombe makundi yazungumzie vitu walivyobuni kisha uanzishe mjadala unaozingatia maswali yafuatayo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ni mada gani mnayoshughulikia?
 • Mnataka watu wajifunze nini kutokana na wazo lenu? Wazo hilo litaleta vipi faida kwa shule/jamii/marafiki zenu?
 • Mnawalenga akina nani?
 • Mtalitangaza vipi wazo lenu kwa watu mnaowalenga?
 • Mnadhani watu mnaowalenga watalichukulia vipi?

Wazo la Mwisho

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Tunatumaini kwamba nyote mmefikiria kuhusu mahusiano mazuri kwa kina zaidi, hasa kwa kuzingatia jinsi ambavyo teknolojia imebadilisha mambo. Pia tulikuwa tunataka mtafakari kuhusu njia za kuwahimiza marafiki zenu wawe "watetezi" au wajitetee wao wenyewe pamoja na wengine wanapoona jambo lisilowapendeza au jambo linalowaumiza wengine.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ni yapi baadhi ya mambo mliyojifunza?
 • Ni zoezi gani mlilofurahia zaidi? Kwa nini?
 • Ni zoezi gani ambalo hamkulifurahia? Kwa nini?
 • Mnawezaje kutumia mambo mliyojifunza au kuyafanya na kuyafanyia kazi maishani mwenu? Utawaeleza vipi rafiki zako yale uliyoyafanya?
 • Ni nini kilichokuwa kitu kipya au cha kushangaza?
 • Mna maswali mengine kuhusu mahusiano mazuri au mabaya?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Facebook ni mahali ambapo unaunganishwa na watu na mambo ambayo unajali. Katika Facebook, wewe ndiye unayeamua utakubali nani awe "Rafiki" yako. Kabla ya kukubali mtu awe "Rafiki" yako ni vizuri kutazama wasifu wa mtu huyo.

Una marafiki ambao ni marafiki zake pia? Mnatoka katika mji mmoja? Unamjua mtu huyo vizuri kiasi kwamba sio tatizo kwako kukubali ombi lake la urafiki?

Chaguo ni lako — unaweza kukubali au kukataa maombi ya urafiki.

Kuondoa rafiki: Ili kuondoa mtu kama rafiki yako, nenda kwenye wasifu wa mtu huyo, gusa kitufe cha Marafiki kilicho katika sehemu ya juu ya wasifu wake, kisha chagua 'Ondoa rafiki'.

Unapochagua kuondoa mtu kama rafiki yako, Facebook haitamjulisha mtu huyo lakini utaondolewa kwenye orodha ya marafiki wa mtu huyo. Ikiwa unataka kuwa rafiki wa mtu huyo tena, utahitajika kumtumia ombi jipya la urafiki.

Ili kufahamu zaidi kuhusu kuondoa marafiki, tembelea fb.me/Unfriending

Kuacha kufuata: Unapoacha kumfuata mtu, hutaona machapisho yake kwenye Mlisho wako, lakini utaendelea kuwa rafiki yake. Ili kuacha kumfuata mtu, Ukurasa, au kikundi moja kwa moja, zungusha mshale wa kipanya juu ya 'Unafuata' (katika wasifu), 'Umependa' (katika Ukurasa), au 'Umejiunga' (katika kikundi) karibu na picha ya jalada kisha chagua 'Acha kufuata'.

Kuzuia: Facebook pia humpa mtu yeyote uwezo wa kuzuia watu wengine. Unapomzuia mtu, anaondolewa kama rafiki yako ili usiendelee kuona wasifu au machapisho yake.

Pia, mtu huyo hataweza tena kuchapisha chochote kwenye wasifu wako, kukushirikisha katika machapisho, kukualika kwenye matukio au vikundi, kuanzisha mawasiliano nawe, au kukuongeza kama rafiki. Kwa kumzuia mtu, pia nawe hutaweza kufanya hayo yote kwa hiyo hutaweza kufanya mambo kama vile kuanzisha mawasiliano naye, au kumuongeza kama rafiki.

Unapomzuia mtu, hatutamjulisha kwamba umemzuia. Ili kumzuia mtu:

 • Bofya kwenye sehemu ya juu ya kulia ya ukurasa wowote wa Facebook.
 • Bofya Nitamzuia vipi mtu anayenisumbua?
 • Weka jina au anwani ya barua pepe ya mtu unayetaka kuzuia kisha bofya Zuia.
 • Ikiwa umeweka jina, chagua mtu maaalum unayetaka kumzuia kutoka katika orodha itakayotokea.

Ili kufahamu zaidi, tembelea fb.me/Blocking

Kwa wale ambao mnatumia Instagram kati yenu, kuna namna rahisi za kuripoti, kudhibiti na kuzuia watumiaji katika Instagram. Unaweza kuripoti maudhui, maoni au akaunti.

Ni nini kinachotokea unaporipoti?

Kuna timu kutoka ulimwengu mzima inayopitia ripoti hizo na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuondoa maudhui yasiyoambatana na Miongozo yetu.

Mbali na programu ya kuripoti, Instagram ina sehemu za ziada za Kituo cha Usaidizi za kukusaidia kuripoti:

 • Akaunti ya Mtu Anayeiga Mwingine
 • Akaunti ya Mtoto Ambaye Hajafikisha Umri Unaohitajika
 • Akaunti Inayoeneza Chuki
 • Akaunti Iliyodukuliwa
 • Ukiukaji wa Haki za Miliki Ubunifu

Instagram pia hukuwezesha kuripoti ndani ya programu, pahali popote katika huduma hiyo. Ukiona chochote ambacho unadhani hakifai kuwa katika Instagram, unaweza kukiripoti, kukidhibiti au kukizuia. Ikiwa maudhui yaliyoripotiwa yanakiuka masharti yetu, yanaondolewa.

Ripoti moja ni sababu tosha ya kuondoa maudhui yanayokiuka masharti hayo. Ripoti nyingi kuhusu jambo ambalo halikiuki masharti hazitasababisha kuondolewa kwake.

Kudhibiti: Hatua ya kudhibiti imewekwa ili kukupa uwezo wa kulinda akaunti yako kisiri huku ukiendelea kufuatilia akaunti ambayo imechangia kutatizika kwako. Wakati mwingine, kwa sababu ya kuwa na maingiliano yasiyokupendeza, au sababu yoyote ile uliyo nayo, ni vizuri kuweka nafasi zaidi kati ya akaunti mbalimbali.

Kuzuia: Kuzuia akaunti kunamaanisha kwamba mwenye akaunti hiyo hataona maudhui yako na kwamba wewe hutaona maoni atakayotoa kwenye machapisho ya watu wengine.

Katika WhatsApp unaweza kuzuia namba yoyote au kuondoka katika kundi lolote unalotaka. Tumia vipengele hivi ili kudhibiti matumizi yako ya WhatsApp.

Sawa na unapotumia Facebook na Instagram, unaweza kuziripoti jumbe taka zinazokutatiza au Kuondoka katika Kundi hilo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Umewekwa katika makundi yoyote ambayo hukuwa unataka kujiunga nayo?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Pia unaweza kukomesha arifa/kuondoka kwenye kundi mara moja.

Vyovyote vile, wewe ndiye utakayeamua kama Utakomesha Arifa au Kuondoka.

Kwa hiyo kumbukeni kwamba, iwe mko katika Facebook, Instagram, WhatsApp, au Messenger, mnaweza kuzuia au kuripoti maudhui au watu wanaosambaza taarifa mnazodhani kuwa hazifai.

Iwe ni kwa sababu ya dhuluma, unyanyasaji au masuala mengine, karibu kila aina ya maudhui yanaweza kuripotiwa au kuzuiwa.
Wakati mtu anaporipotiwa kwa kampuni ya Facebook, ripoti hiyo inakaguliwa na maudhui au mtu huyo anaondolewa ikiwa amekiuka Viwango vya Jumuiya facebook.com/communitystandards.

Katika hali zote, utambulisho wa mtu aliyeripoti au kuzuia mtu aliyekiuka masharti haufichuliwi.

Timu kubwa ya Facebook hufanya kazi katika ofisi zilizoko kote duniani, saa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki. Timu hizo hutumia zaidi ya lugha ishirini na nne ili kukagua masuala unayoripoti na kuhakikisha kuwa huduma za Facebook, Instagram, WhatsApp na Messenger zinabaki salama.

Njia nzuri zaidi za kuripoti maudhui yanayokera au jumbe taka ni kutumia kiunganishi cha Ripoti kinachoonekana karibu na maudhui hayo.
Kwa mfano, ili kuripoti chapisho:

 • Bofya sehemu ya juu ya kulia ya chapisho unalotaka kuripoti kisha chagua sitaki kuona chapisho hili.
 • Bofya Kwa nini hutaki kuona chapisho hili?
 • Chagua chaguo ambalo linaeleza vizuri zaidi suala linalokutatiza kisha ufuate maelekezo yaliyo kwenye skrini.

Ikiwa umeripoti kitu fulani, unaweza kuangalia hali ya ripoti yako kwenye Kikasha cha Usaidizi.
Tafadhali kumbuka kwamba ni wewe tu unayeweza kutazama Kikasha chako cha Usaidizi: fb.me/supportInbox

Ili kufahamu zaidi, tembelea: fb.me/Reporting

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy