Fursa za Kidijitali

Somo 5: Mitandao ya Kijamii na Algorithimu

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Mlisho Wenye Kasoro

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Pengine wengi wenu mna akaunti katika angalau aina moja ya mitandao ya kijamii — iwe Instagram, Twitter, Facebook, YouTube au mitandao mingine mbalimbali ya kijamii.

Baadhi yenu pengine mna akaunti nyingi katika mitandao tofauti ya kijamii kwa sababu tofauti. Pengine unatumia mtandao mmoja wa kijamii kuangalia habari, unatumia mwingine kuwasiliana na marafiki, na mwingine unautumia kutazama video maarufu sana sasa hivi.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, ni mtandao/mitandao gani ya kijamii unayoitumia sana?
  • Je, kuna mtu aliye na akaunti nyingi katika mtandao mmoja wa kijamii?
  • Kwa kawaida huwa unaona nini kwenye akaunti zako za mitandao ya kijamii? Ikiwa una akaunti nyingi katika mtandao mmoja wa kijamii, huwa unaona maudhui tofauti (mfano, picha, video, machapisho yenye matini, matangazo) katika kila akaunti?
  • Je, unadhani ni nini kinachobaini unayoona (yaani, maudhui kama vile picha, video, machapisho yenye matini, matangazo n.k.)?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika mitandao ya kijamii, algorithimu zinaendelea kubuniwa ili kuamua mambo utakayoona. Kwa mfano, algorithimu zinaweza kubaini kiasi cha maudhui utakachoona kutoka kwa marafiki, jamaa, na makundi dhidi ya maudhui kutoka kwa biashara, chapa, na vyombo vya habari.

Algorithimu pia zinaweza kubaini muundo wa maudhui utakaopewa kipaumbele, kama vile video, machapisho yenye matini au picha.

Mitandao mingi ya kijamii hufuatilia jinsi unavyoingiliana na machapisho ya marafiki, jamaa, na makundi, pamoja na maingiliano yako na machapisho yaliyo wazi kwa watu wote kutoka kwa biashara, chapa na vyombo vya habari.

Algorithimu za mitandao hii ya kijamii zinaweza kubashiri mambo unayotaka kuona kulingana na maingiliano hayo.

Lengo kuu ni kukuletea maudhui ambayo kuna uwezekano kwamba utaingiliana nayo kwa kuweka machapisho kwenye mlisho wako ambayo yanatoka kwa watu na kurasa sawa au zinazofanana na zile ambazo umeingiliana nazo hapo kabla.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, ni kwa namna gani mnahisi kwamba milisho ya mitandao yenu ya kijamii inaonesha mambo mnayopendelea?
  • Je, umewahi kupata chapisho katika mlisho/milisho yako ambalo uliona kuwa halilingani na muktadha na historia yako kwa kuwa halikuhusu/halifai/haliendani na mawazo yako? Je, utajisikia huru kusambaza kwenye kundi kwa nini ulijisikia hivi? Kwa nini unadhani algorithimu zilionesha maudhui hayo?
  • Je, kuna mifano ya machapisho ya mitandao ya kijamii ambayo ilionekana kuendana sana na muktadha na historia yako kwa namna hakika/ya wakati unaofaa/iliyo sawa na mawazo yako? Je, utajisikia huru kusambaza kwenye kundi kwa nini ulijisikia hivi?
  • Hebu tuchukulie kwamba algorithimu huhakikisha kwamba itakuonesha maudhui ambayo unapendelea kwa asilimia 100. Je, kuna uwezo wa kuwepo kwa hatari au mapungufu gani? Unadhani kuwa algorithimu inafaa kutengenezwa kwa namna kwamba, wakati mwingine, inaonesha maudhui yasiyotarajiwa (yaani, kwa kubahatisha tu)?
  • Je, umewahi kuona machapisho kwenye mlisho/milisho yako ambapo maudhui (mfano, chapisho linalozungumzia siasa au masuala ya kiraia) yalionekana kuwa ya kutiliwa shaka/kana kwamba yalinuia kukuhadaa? Kama ndiyo, ni mara ngapi? Je, kuna mtu anayeweza kutoa mfano wa chapisho la aina hii? Je, ulifanya nini baada ya kuliona? [Washiriki wengine, kwa mfano, huenda walilipuuza chapisho hilo, wakaliripoti au kulizungumzia na rafiki au jamaa.]
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Ili kutusaidia kufikiria kwa kina zaidi kuhusu jinsi algorithimu inavyobaini jinsi milisho ya mitandao yetu ya kijamii itakavyokuwa, tufanye zoezi la kundi zima!

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wagawe washiriki katika makundi manne kisha ulipatie kila kundi moja ya vitini vinne vya "Kutana na Beldine" na mkusanyiko wa machapisho 24-32 ya mitandao ya kijamii katika bahasha. Kunatakiwa kuwa na bahasha nne — moja ya kila kundi.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Katika makundi yenu, kwanza, angalieni mkusanyiko wa machapisho hayo, kisha taarifa kuhusu Beldine zilizo katika kitini chenu. Kisha, chagua hadi machapisho 18 na myapange kwa mpangilio mnaofikiria utatengeneza mlisho unaolingana na sifa ya Beldine. Fikiria kuhusu aina ya maudhui ambayo Beldine angefurahia zaidi kuingiliana nayo (mfano, muda ambao angetumia kutazama, kupenda, kubofya, kusambaza au kusambaza tena machapisho ya wengine).

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape washiriki dakika 15 ili kushiriki katika zoezi hili la kundi.

DONDOO ZA MWALIMU

Jina lililoko hapo juu linaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lao. Lengo la kitini hiki ni kuwaonesha wanafunzi jinsi taarifa, kwa mfano, kuhusu mambo anayopenda na asiyopenda mtu, zinaweza kusaidia algorithimu kuonesha maudhui ya mitandao ya kijamii yanayoambatana na mapendeleo ya mtu huyo.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Waombe washiriki wote wakusanyike pamoja, huku washiriki wakikaa katika makundi yao. Omba makundi yateue mtu atakayetoa wasilisho kuhusu mlisho uliotengenezwa. Omba kila kundi lieleze kwa kifupi 1) taarifa ambazo walipata kuhusu Beldine, 2) machapisho ambayo walichagua na kwa sababu gani 3) kati ya aina tatu tofauti za taarifa kuhusu

Beldine zilizotolewa kwenye kitini, ni madhui gani waliyotilia maanani ili kutengeneza mlisho.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, kulikuwa na taarifa zozote kuhusu Beldine ambazo mnahisi zilikuwa na umuhimu wa kipekee katika kutengeneza mlisho?
  • Je, kulikuwa na taarifa kuhusu Beldine ambazo mlihisi zilikuwa na umuhimu mdogo?
  • Ni taarifa gani kuhusu Beldine ambazo mlizipa kipaumbele kuliko zingine?
  • Ni taarifa gani kuhusu Beldine ambazo mngetaka kupata — ili kufanya algorithimu itengeneze mlisho ambao unaendana na Beldine — ambazo hamkuwa nazo? Kwa nini mngetaka taarifa hizo? 
    • Jibu ambalo huenda litatolewa: Beldine anajali sana kuhusu haki za binadamu. Hata hivyo, kwa kuwa washiriki walikuwa na wazo moja tu kuhusu haki za binadamu (yaani, kipeperushi kuhusu usawa wa kijinsia), huenda ilikuwa vigumu kuutengeneza mlisho ili kuangazia masuala mahususi ya haki za binadamu. Inaonekana kwamba Beldine ana ari kuhusu usawa wa kijinsia, lakini je, ana ari kuhusu masuala mengine ya haki za binadamu, na kama ndiyo, ni yapi?

Taswira Kamili

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kila kundi lilipokea taarifa kuhusu Beldine. Sasa hebu tulete taarifa yote kuhusu Beldine pamoja na tufikirie kuhusu vipi (kama inatumika) uelewa wetu kuhusu jinsi mlisho na algorithimu iliyopo inayoendana na Beldine huenda ikabadilika.
Unaweza kuonesha mkusanyiko kamili wa taarifa kuhusu Beldine ("Kutana na Beldine—Taswira Kamili Zaidi: Nakala ya Mkufunzi") kwenye skrini ya maonesho au uchapishe nakala na kumpa kila mshiriki.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kulingana na taarifa zote mnazojua sasa kuhusu Beldine, je, ni ipi kati ya milisho iliyopo na algorithimu zilizopo (zilizobuniwa na yale makundi manne) ndizo mnadhani kwamba Beldine angefikiria zingemsisimua zaidi? Kwa nini?
  • Kwa kufahamu jumla ya taarifa zote, utadumisha mojawapo ya milisho iliyopo (iliyotengenezwa na vile vikundi vinne) na algorithimu zilizopo au utatengeneza mlisho mpya?
DONDOO ZA MWALIMU

Jina lililoko hapo juu linaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lao. Lengo la kitini hiki ni kuwaonesha wanafunzi jinsi taarifa, kwa mfano, kuhusu mambo anayopenda na asiyopenda mtu, zinaweza kusaidia algorithimu kuonesha maudhui ya mitandao ya kijamii yanayoambatana na mtu huyo anachokipenda.

Zoezi

CHAGUO LA 1 kwa washiriki wenye miaka 11–13
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa, hebu tutumie maarifa tuliyojifunza leo kuhusu mitandao ya kijamii na algorithimu katika milisho yenu ya mitandao ya kijamii. Chagua akaunti kutoka kwa mitandao mahususi ya kijamii kisha uchague machapisho 18 ya kwanza yatakayotokea. Tambua vipengele 10 vinavyobadilika unavyofikiria kwamba algorithimu iliyopo inajikita (mfano, maingiliano yako na machapisho ya rafiki yako, ya duka la nguo au ya timu ya michezo).

CHAGUO LA 2 kwa washiriki wenye miaka 14–18
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kwa wale wanaotaka kupata data zinazobaini utendakazi wa algorithimu za milisho yenu ya mitandao ya kijamii, mnaweza kupata na kupakua nakala ya taarifa zenu ambazo mitandao ya kijamii inazo.

Kwa wale walio na akaunti ya Facebook, ingia katika Facebook ukitumia kompyuta na kwenye upande wa juu wa kulia wa ukurasa wako mwanzo, bofya mshale wa bluu unaoelekea chini. Kutoka hapo, bofya Mipangilio kisha ubofye Taarifa Zako za Facebook. Kisha bofya Pakua Taarifa Zako. Hapa, unaweza kuchagua ni taarifa gani unazotaka kupakua (mfano, matangazo, eneo, machapisho).

Kwa wale walio na akaunti ya Instagram, ingia katika Instagram kwa kutumia kompyuta ya mezani kisha ubofye kitufe cha Wasifu kilicho kwenye kona ya juu upande wa kulia, iliyo na umbo kama la mtu, kisha ubofye kitufe cha Mipangilio, inayofanana na gurudumu. Kutoka hapo, bofya kitufe cha Faragha na Usalama na ubiringishe chini hadi Data ya Akaunti ili ubofye Tazama Data ya Akaunti. Ili kuangalia aina mahususi ya data (mfano, maombi ya sasa ya wafuasi, alama za reli unazofuatilia, akaunti ulizozuia, n.k.) bofya Tazama Zote.

Ikiwa una akaunti ya Facebook na Instagram pia, unaweza kujaribu kufanya zoezi hili katika akaunti zote mbili!
Kwa mujibu wa taarifa hizi, ningependa utoe maoni yako, kwa maandishi, ukizingatia maswali yafuatayo:

  • Faili hizi zinawakilisha baadhi ya data ambazo tovuti ya Facebook na/au Instagram imekusanya kukuhusu. Je, unajihisi vipi kwamba tovuti za Facebook na/au Instagram zina taarifa hizi zote? Je, ungependa tovuti hizi ziwe au zisiwe na taarifa hizi?
  • Je, taarifa hizi zinaonekana kuonesha taswira sahihi kukuhusu/kuhusu kile unachokipenda? Kwa nini au kwa nini siyo?
  • Mlisho wako unaonekana kuashiria au kutoashiria mambo unayopendelea kwa kiasi gani?
  • Je, kuna taarifa zingine kuhusu mambo unayopendelea na uliyo na ari nayo ambayo ungependa tovuti za Facebook na/au Instagram zifahamu kukuhusu ili mlisho wako ukufae zaidi?
  • Ni vipengele gani vya taarifa ulizopakua unafikiria vinachangia muundo wa algorithimu inayobaini jinsi mlisho wako utakavyokuwa?
  • Je, kuna tovuti au huduma gani zingine za mtandaoni unazoingiliana nazo ambazo huenda zikaathiri jinsi mlisho wako ulivyo? Kwa mfano, ukinunua tiketi za ndege mtandaoni kutoka kwa tovuti mahususi ya usafiri, kama vile Expedia*, huenda utaona matangazo kutoka kwa tovuti hiyo katika milisho yako ya mitandao ya kijamii.
DONDOO ZA MWALIMU

Mfano ulioko hapo juu unaweza kurekebishwa ili uendane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lao. Lengo la kitini hiki ni kuwaonesha wanafunzi jinsi taarifa, kwa mfano, kuhusu mambo anayopenda na asiyopenda mtu, zinaweza kusaidia algorithimu kuonesha maudhui ya mitandao ya kijamii yanayoambatana na mtu huyo anachokipenda.


End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy