Somo 3: Kutengeneza Wasifu
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Washiriki watajifunza kuhusu mitindo tofauti ya wasifu na kufanya mazoezi ya kuandika wasifu wakizingatia mambo wanayopendelea, mambo waliyopitia, mbinu mbalimbali na malengo. Washiriki pia watajifunza kuhusu maana ya wasifu na kwa nini ni muhimu katika kufanikisha malengo ya muda mrefu.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
SWALI MUHIMU
- Kwa kuangalia fursa ambazo ungependa kufanya katika siku zijazo, unaweza kusimulia vipi kuhusu historia na ubora wako kupitia wasifu?
VIFAA
- Mfano wa Wasifu
- Kompyuta iliyounganishwa na Intaneti
- Projekta na Skrini ya Maonesho
- Chati mgeuzo au Kipeperushi (Ikiwa hakuna ubao)
- Kalamu nafidhi
- Kompyuta au Kifaa cha Mkononi Kilichounganishwa na Intaneti
- Karatasi
- Kalamu za Wino au Penseli
MATAYARISHO
- Chapisha kitini kimoja kwa kila mwanafunzi.
- Wanafunzi watahitaji intaneti kwa ajili ya somo hili.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yalingane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizi zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu" katika hati nzima. Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- USAWA: Ninafanya maamuzi sahihi kuhusu namna ya kuupa kipaumbele muda na kazi zangu nikiwa na nisipokuwepo mtandaoni.
Kuanza Kutayarisha Rasimu
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Tuanze siku ya leo huku kila mmoja wenu akifikiria kuhusu mwigizaji mmoja anayempenda kutoka katika filamu au kipindi cha televisheni. Anaweza kuwa Harry Potter, The Avengers, au mwingine. Sasa, fikiria kuhusu sifa au mbinu nzuri ambazo mtu huyo anazo. Kama ni Harry Potter inaweza kuwa uaminifu wa juu wa Hermione au katika The Avengers, inaweza kuwa ustahimilivu wa Tony Stark/Iron Man.
Kisha, ningependa ufikirie kuhusu wakati ambapo mtu huyo alionesha mbinu hiyo.
Huku ukizingatia mambo hayo, ningependa uandike mambo matatu katika karatasi nitakayowapa.
Kwanza, ni ipi asili/muktadha wa hali mahususi ambapo mtu huyo alionesha mbinu hiyo? Ni nini kilichokuwa kinafanyika katika kipindi hicho cha televisheni au filamu wakati huo?
Pili, mtu huyo alifanya nini ili kuonesha mbinu hiyo? Alichukua hatua gani?
Tatu, matokeo ya hatua alizochukua yalikuwa yapi? Yaliathiri vipi mambo yaliyokuwa yakifanyika katika shoo ya televisheni au filamu hiyo? Yalikuwa na athari gani kwa waigizaji wengine?
DONDOO KWA MWALIMU
Mifano iliyoko hapo juu inaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Lengo la mifano hii ni kuwaonesha wanafunzi kwamba mbinu zetu zinaweza kutumiwa kuleta mabadiliko kwa kuwaomba wanafunzi watathmini jinsi shujaa au nyota wa filamu anavyotumia mbinu zake ili kuleta mabadiliko.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Unaweza kufikiria kuhusu vipengele hivi vitatu kama 1) Muktadha 2) Hatua Alizochukua, na 3) Matokeo. Njia rahisi ya kukumbuka vipengele hivi ni kwa kutumia kifupisho cha "M.H.M."
Una dakika tano za kuandika M.H.M. ya muigizaji unayempenda.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Andika vipengele hivi vitatu vinavyobadilika — Muktadha, Hatua na Matokeo (M.H.M.)
— na maana yake kwenye chati mgeuzo/kipeperushi au ubao.
Mpe kila mshiriki karatasi na kalamu ya wino au penseli. Wape dakika tano za kushiriki katika zoezi hili.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna mtu anayetaka kuzungumzia mfano wa M.H.M. wa muigizaji aliyechagua?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Kwa kutoa kila moja ya vipengele hivi — muktadha wa hali fulani, hatua zilizochukuliwa na matokeo yaliyopatikana — tunasimulia tukio lenye mwanzo (yaani muktadha), sehemu ya kati (yaani hatua zilizochukuliwa) na mwisho (yaani matokeo).
Kwa fursa tofauti tunazotaka kufanya, mbinu ya M.H.M. ni zana nzuri tunayoweza kutumia kuonesha mbinu zetu na kusimulia visa vyetu kuhusu mambo tunayoweza kufanya vyema, iwe ni kushirikiana na wengine katika kazi za kundi, uchanganuzi wa data au historia ya sanaa.
Fikiria kuhusu fursa uliyo na ari nayo — kazi ya kujitolea, chuo kikuu mahususi, tarajali, mpango wa mustakabali wa kazi yako — na mbinu moja uliyo nayo ambayo huenda inahusiana na shughuli hiyo. Sasa, tumia dakika 10 zijazo kuandika M.H.M. yako mwenyewe kwenye upande wa nyuma wa karatasi yako!
Wape washiriki dakika 10 ili waandike mfano wao wa M.H.M.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Kuna mtu anayetaka kuzungumzia kisa chake cha M.H.M.?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Hili zoezi fupi limewawezesha kuanza kufikiria kuhusu mbinu zinazohusiana na mambo mliyo na ari nayo na jinsi ambavyo mnaweza kusimulia visa kuhusu mbinu hizi.
Njia nyingine ya kuonesha mambo tuliyofanikiwa kufanya pamoja na tajriba inayohusiana na kazi na kusimulia visa vyetu ni kwa kutengeneza wasifu.
Wasifu unatakiwa kuwa wa kurasa 2 na kwa kawaida huwa na taarifa muhimu binafsi kama vile taarifa za mawasiliano, taarifa binafsi, muhtasari wa uzoefu wako na pia historia ya elimu. Pia ni muhimu kwamba uweke maelezo kuhusu ujuzi, weledi wa kitaaluma na wadhamini wako wakuu wanaoweza kuthibitisha kwamba una ujuzi huo.
Nchi na mashirika mbalimbali huwa na mitazamo tofauti kuhusu taarifa ambazo ni muhimu kuwekwa katika wasifu. Kwa mfano, kuweka picha katika wasifu ni jambo la kawaida katika sehemu za Asia, Afrika na Mashariki ya Kati, ilhali sio kawaida nchini Marekani.
Kimataifa, kuna taratibu nzuri zinazoweza kukusaidia, ambazo unafaa kuzikumbuka unapotengeneza wasifu:
- Kuweka taarifa za mawasiliano (mfano anuani yako ya barua pepe)
- Kuhakikisha urefu wa wasifu hauzidi kurasa mbili
- Kuweka maelezo ya elimu (masomo ya chuo na ya shule ya sekondari)
- Kuweka hoja chini ya kila kazi uliyofanya hapo awali, ukiandika majukumu yako na mambo uliyofanikiwa kufanya
- Tuzo na wadhamini (Angalau wasipungue watatu)
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Wasifu ni muhtasari mfupi (kwa kawaida huwa na ukurasa mmoja au mbili) wa tajiriba na ujuzi wako. Kwa kawaida watu hubadilisha wasifu zao kulingana na kazi wanayoomba. Wasifu ni nyaraka yenye taarifa za kina kuhusu historia yako ya kazi (mara nyingi hujumuisha sehemu inayoeleza kuhusu ujuzi wa mtu) na lugha anazozungumza (ukieleza bayana lugha yako ya asili) katika kurasa mbili (ikitegemea urefu wa muda wa kazi wa mtu) ambayo hubaki hivyo wakati mtu anapoomba kazi tofauti.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna yeyote ambaye amewahi kutengeneza wasifu? Kama ndiyo, ni jambo gani alilofurahia zaidi? Ni sehemu ipi iliyokuwa na changamoto kubwa?
- Je, umefikiria kuhusu njia nyingine za kuonesha tajiriba yako na mambo unayoweza kuyafanya vizuri? Kama ndiyo, unaweza kulishirikisha kundi baadhi ya mifano hiyo?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Mbali na wasifu, kuna njia nyingine za kina zaidi na zisizokuwa za kina zinazonijia akilini kuhusu kuonesha tajiriba zetu zinazohusiana na uzoefu.
Njia ya kina zaidi inaweza kuwa kutengeneza hati ya kidijitali inayo onesha kazi ulizofanya. Hati ya kidijitali inayoonesha kazi ulizofanya inaweza kuwa mkusanyiko wa nyenzo za kidijitali (mfano, michoro, picha, matini, faili zenye maudhui tofauti, machapisho ya blogu).
Mkusanyiko wa nyenzo kama huo hauwezi tu kusaidia kuonesha uwezo wako, bali pia unaweza kuwa namna ya kusimulia kisa chako. Mfano wa wasifu unaoangazia kuonesha kazi alizofanya mtu ni ule wa Euan Brown, ambaye ni mwanachama wa Youth and Media, http://portfolios.massart.edu/ebrownart.
Pia unaweza kufikiria kuhusu kuandika biografia. Biografia ni muhtasari mfupi (kwa kawaida usiozidi ukurasa mmoja) wa mambo muhimu ambayo mtu amepitia na aliyofanikiwa kufanya. Badala ya kuorodhesha tarehe zilizowekwa za kazi tofauti au shughuli mahususi kama sehemu ya kazi (kama katika wasifu), biografia hutoa picha pana ya mambo makuu zaidi ambayo mtu amefanikiwa kufanya. Biografia, ambazo huandikwa katika mtu wa tatu (yaani, "Sara sasa hivi hufanya kazi katika..."), mara nyingi huwa na picha ya mtu huyo, vyeo vya kazi vya nyuma/sasa, hati (mfano, shahada za chuo kikuu, vyeti vya kozi za mtandaoni) na tuzo. Angalia mifano ya biografia katika https://cyber.harvard.edu/people, kama vile https://cyber.harvard.edu/people/ahasse.
Pia unaweza kuwa na wasifu wa kawaida kuhusu wewe ambao utaelekeza watu kuangalia. Wasifu ni muhtasari mfupi sana (takriban sentensi tatu) kuhusu pahali ambapo mtu anasomea/anafanya kazi hivi sasa, miradi mikuu, na pengine mambo aliyo na ari nayo. Sawia na biografia, wasifu mara nyingi huandikwa katika nafsi ya tatu. Angalia baadhi ya mifano kwenye tovuti ya Youth and Media kupitia http://youthandmedia.org/team/core/.
DONDOO KWA MWALIMU
Mifano iliyoko hapo juu inaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Tafadhali tumia viungo vya wasifu wa watu ambao wanatumika katika muktadha wa eneo lenu badala ya viungo vilivyo hapo juu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sasa kwa kifupi tumeangalia njia tofauti mnazoweza kuzitumia kuonesha historia zenu na mambo mliyofanikiwa kufanya.
Hata hivyo, leo tutajikita katika njia moja mahususi — wasifu — kwa kukusaidia kutengeneza wasifu wako mwenyewe! Ikiwa tayari una wasifu, jisikie huru kuitumia kama sehemu ya kuanzia.
DONDOO KWA MWALIMU
Toa mfano wa wasifu kwa wanafunzi wako ambao unaendana na muktadha wa kawaida wa wanafunzi wako. Lengo la zoezi hili ni kuwafundisha wanafunzi kuhusu mambo wanayotakiwa kuyaweka katika wasifu kwa kutazama mifano inayotumika.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Mnaweza kutumia wasifu huu kuwaelekeza — ikiwa tayari una wasifu au unautengeneza kwa mara ya kwanza. Kwa kuanza, ningependa mtembelee tovuti ya "Jinsi ya Kuanza Kutengeneza Wasifu—Chati Mtiririko."
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Onesha tovuti ya "Jinsi ya Kuanza Kutengeneza Wasifu—Chati Mtiririko" kwenye skrini ya maonesho. Tafadhali kumbuka tovuti hii ni ya Kiingereza na inazingatia muktadha wa Marekani. Unaweza kuwaonesha mfano unaoambatana na muktadha wa eneo lako au la washiriki wako. Kwa mfano, Monster.com ni tovuti ya kimataifa ya nafasi za ajira ambayo hutoa zana za utafutaji wa kazi na ushauri kuhusu kutengeneza wasifu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Kisha, tumieni takriban dakika 10 kusoma yaliyo katika tovuti hii.
Kwa kutumia mambo uliyojifunza, anza kutengeneza wasifu wako au kuufanyia marekebisho ule ulio nao — ukitumia kompyuta au kifaa cha mkononi — ukitumia mtindo wa wasifu unaofaa kwa kazi unayotaka.
Ikiwa tayari una wasifu, jisikie huru kuufungua kwenye kompyuta au kifaa chako cha mkononi. Ikiwa huna wasifu wako hivi sasa, jaribu kadri unavyoweza kuukumbuka vizuri kuuandika kwenye karatasi au katika kifaa chako.
Unapotengeneza au kuurekebisha wasifu wako, hakikisha umejumuisha tajiriba na ujuzi wako wote!
Kupata Mrejesho
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Omba kila mshiriki achapishe nakala mbili za wasifu wake au atoe nakala za wasifu au uwatolee nakala.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Kila siku, tunazingatia mazingira tuliyomo ili kuamua mambo tutakayoshiriki na wengine. Kwa mfano, pengine sisi huzungumza na walimu au wazazi/walezi wetu kwa njia tofauti na tunavyozungumza na marafiki zetu. Kufikiria kuhusu sifa za walengwa wetu ni njia muhimu ya kuelewa jinsi ya kuwasiliana na watu tunaojaribu kuwafikia kwa njia nzuri zaidi. Ingawa tuna mawazo mengi yanayotujia akilini kila siku, sharti tutambue ni mawazo gani yanayofaa kushirikisha, na tutawashirikisha akina nani. Katika muktadha wa wasifu, hali hii sio tofauti. Ingawa pengine tumejihusisha katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na kazi, ni muhimu kufikiria kutambua mambo yanayoendana vizuri na vigezo vya waamuzi wanaokagua wasifu.
Sasa, tutaangalia kielelezo cha wasifu ambacho kila mmoja wenu alitengeneza (kwa mitazamo yenu binafsi) ili kutambua vipengele vilivyo vizuri zaidi na pia vipengele ambavyo vinaweza kuboreshwa kwa ajili ya watu watakaotazama wasifu huo.
Kwanza, juu ya wasifu wako, andika kazi mahususi ambayo unaitengenezea wasifu huo. Kwa maneno mengine, fikiria kuhusu: Ni nani unayemsimulia kisa chako? Kisha, badilishana wasifu wako na mshiriki mwingine (yaani, umpe wasifu wako, naye akupe wake).
Kwa kutumia kompyuta au kifaa cha mkononi, kila mmoja wenu anatakiwa kutumia muda wa dakika 10 ili kutafuta baadhi ya ujuzi na mambo yanayohitajika kwa ajili ya nafasi hiyo. Mnaweza kufanya hivyo kwa kutumia kanzi data za mtandaoni, kama LinkedIn, au kutafuta mchanganyiko wa "[cheo]" + "ujuzi" + "sifa zinazotakiwa."
Baada ya kutafuta, tumia dakika 10 kupitia wasifu wa mwenzako kisha umpe maoni ya kumsaidia. Kwenye upande wa nyuma wa wasifu wako, andika angalau mambo mawili ambayo umeyapenda sana kuhusu wasifu wake (mtindo au jinsi alivyoangazia ujuzi fulani) na mambo mawili uliyopenda lakini unadhani kuwa yanaweza kurekebishwa ili kuboresha vizuri wasifu wake.
Kisha, rudia mchakato huu kwa kubadilishana na wenzenu, kutafuta ujuzi na sifa zinazotakiwa ambazo mwenzake anazitaka, kisha upitie wasifu wake.
Baada ya kukamilika kwa zoezi hili, unatakiwa kuwa umepitia wasifu wa watu wawili na kupokea maoni kuhusu wasifui wako kutoka kwa watu wawili.
Zoezi
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Angalia mrejesho uliopata kutoka kwa hao washiriki wengine wawili. Pita wasifu wako na uufanyie marekebisho kama inavyotakiwa.
Ikiwa utapata nafasi, onesha wasifu wako kwa mtu kama mwalimu, mkutubi, mwanafamilia au rafiki. Baada ya kupata mrejesho, hariri wasifu wako ili upate nakala ya mwisho.
Mwisho, katika aya utakayoandika, linganisha nakala ya kwanza na ya pili ya wasifu wako na ueleze mambo uliyojifunza wakati wa kufanyia wasifu wako marekebisho.
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.