Somo 5: Unataka Kuwa Nani?
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Wanafunzi watatathmini utambulisho wao mtandaoni na maudhui wanayotengeneza na kuyasambaza yanayohusiana na malengo yao (mfano, yanayohusiana na kazi, masomo au mambo yanayowavutia maishani ambayo wangependa kujishughulisha nayo). Wataangalia jinsi ya kuthibiti utambulisho wa mtandaoni kwa kuzingatia mada, wavuti, jina, mwonekano na mipangilio binafsi.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
MASWALI MUHIMU
- Teknolojia za kidijitali zinaathiri vipi mambo yanayokuvutia maishani na malengo yako?
- Unayawasilisha vipi mambo yanayokuvutia maishani na malengo yako kupitia mtandao?
VIFAA
- Kitini cha "Utambulisho Wangu wa Mtandaoni"
MATAYARISHO
- Chapisha kitini kimoja kwa kila mwanafunzi.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yaendane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizo zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu." Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- JUMUISHI: Niko tayari kusikiliza na kutambua mitazamo tofauti kwa heshima na ninazungumza na watu wengine mtandaoni kwa heshima na kwa kuelewa hisia zao.
Utambulisho Wangu wa Mtandaoni
Mjadala
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Hebu tuchukue muda mfupi kutafakari kuhusu jinsi tunavyo aminiana na watu wengine kulingana na hali zao. Huenda ukafanya mambo tofauti ukiwa na marafiki zako ikilinganishwa na utakavyoyafanya ukiwa na wanafamilia au walimu wako shuleni.
Pia huenda ukawa mtu tofauti kulingana na mazingira au hali iliyopo — ukiwa shuleni na marafiki zako, wewe ni mtu tofauti na unapokuwa na marafiki hao hao nje ya shule.
Sote huenda tukawa watu tofauti kidogo kulingana na mahali tulipo na watu tulio nao. Una uwezo sawa wa kudhibiti jinsi wewe na maudhui yako yatakavyoonekana kwa umma kwenye mtandao na inaweza kuwa vyema ukianza kufikiria kuhusu jinsi ambavyo ungetaka wengine wakuone kwenye intaneti.
Watu mashuhuri (mfano; walio katika tasnia ya muziki, filamu, televisheni, wanasiasa, viongozi wa kibiashara) hufanya hivyo kila wakati. Kwa kuwa makini katika utengenezaji wa kila sehemu ya chapa yao na taswira yao mbele ya umma, kuanzia maudhui ya mitandao ya kijamii (mfano; picha, video, machapisho ya maandishi) hadi mahojiano, wanajaribu kuwavutia mashabiki wengi kadiri wanavyoweza. Sio lazima uwe mtu mashuhuri mwenye mkakati wa utangazaji wa mabilioni ya pesa. Lakini ni muhimu kufikiria kuhusu watu ambao huenda wanaangalia shughuli na utambulisho wako mtandaoni na jinsi utakavyoonekana mtandaoni katika siku zijazo.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili wawili.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Hivi sasa mnatengeneza na/au kuchapisha maudhui ya aina gani mtandaoni (mfano; video, muziki, kuchanganya nyimbo/video, blogu, vielelezo, katuni)?
- Ni nini kinakupa motisha ya kutengeneza au kuchapisha maudhui haya?
- Kwa nini unafanya kazi hiyo? Ni maudhui gani ambayo unayahusisha na jina na picha yako halisi?
- Kuna maudhui yoyote ambayo usingependa yahusishwe nawe katika umma? Kwa nini siyo?
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wape wanafunzi dakika saba za kujadiliana. Kisha omba makundi yazungumzie majibu yaliyotolewa.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
Kabla ya kuzungumzia shughuli na maudhui yako ya mtandaoni katika siku zijazo, hebu tuzungumzie malengo yake kwanza. Jadiliana na mwenzako:
- Ungetaka kuwa nani na wapi katika miaka michache ijayo, na ulipata wazo hilo vipi kwa mara ya kwanza? Ni sawa ikiwa una zaidi ya wazo moja au kazi zaidi ya moja ambazo kwa wakati huu unazipenda.
- Una malengo gani mengine binafsi ambayo hayahusiani na malengo yako ya kazi?
- Ni nini unachoweza kufanya mtandaoni ambacho kinaweza kusaidia kutimiza malengo yako ya kazi au binafsi ya siku zijazo?
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wape wanafunzi hati za "Utambulisho Wangu wa Mtandaoni".
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Mnachofanya mtandaoni kinaweza kuwasaidia kuangalia mambo yanayowavutia hivi sasa na pia kuwasaidia kutambua mambo ambayo mngependa kufanya katika siku zijazo.
Tumieni dakika chache kujaza hati hii na mfikirie kuhusu ndoto zenu mkizingatia shughuli na maudhui yenu mtandaoni. Kumbuka kwamba utambulisho wa mtandaoni wa kila mtu huenda ukawa tofauti na utambulisho wako na huenda ukabadilika kulingana na jinsi malengo na mambo unayopendelea yatakavyobadilika katika siku zijazo.
Zoezi
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sasa kwa kuwa tumefikiria kuhusu unavyojiona wewe na mambo unayopendelea, tufikirie kuhusu jinsi ambavyo ungependa kuonesha watu wengine vipengele vya utambulisho wako.
Chukulia kwamba unaanzisha shughuli na maudhui mapya kwenye mitandao ya kijamii yanayojikita katika kipengele maalum cha utambulisho wako. Utaanza upya na utakuwa na uhuru kamili wa kubadilisha mipangilio yote binafsi na kubuni maudhui kwa namna unayotaka. Kwa kutumia aya fupi, eleza jinsi unavyoweza kupanga shughuli na maudhui haya mapya kwenye mitandao ya kijamii ili kuonesha taswira unayotaka marafiki na wafuasi wako waione. Zungumzia dhana zifuatazo:
- Aina ya akaunti na tovuti (mfano; mitandao ya kijamii, blogu)
- Aina ya maudhui (mfano; picha, video, machapisho ya maandishi)
- Unaweza kuandika nini katika sehemu ya "Kuhusu Mimi"?
- Unaweza kutumia picha za aina gani?
- Ungeiweka vipi mipangilio yako binafsi? Je, mipangilio hii ingetegemea aina ya maudhui unayosambaza?
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.