Somo 1: Kuangalia Mambo Tuliyopitia
Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.
Muhtasari wa Somo
Washiriki watajifunza jinsi ya kutambua matukio mahususi yaliyochangia kuwajenga watu namna walivyo hivi sasa. Pia wata tafakari kuhusu namna matukio kama hayo yanavyoweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wao na kufikiria namna wanavyoweza kutengeneza uzoefu mpya utakao wasaidia kutimiza malengo yao.
Matayarisho ya Somo
MUDA UNAOKADIRIWA
SWALI MUHIMU
- Matukio uliyopitia yamechangia vipi kukujenga na kuonekana kama ulivyo hivi sasa na unaweza vipi kutengeneza uzoefu mpya wenye maana?
VIFAA
- Kitini cha "Kukabiliana na Changamoto Mpya"
- Kitini cha "Mpango wa Malengo Yangu"
- Kompyuta iliyounganishwa na Intaneti
- Projekta na Skrini ya Maonesho
- Chati Mgeuzo au Kipeperushi (ikiwa hakuna ubao)
- Kalamu nafidhi
- Karatasi
- Kalamu za Wino au Penseli
MATAYARISHO
- Chapisha kitini kimoja kwa kila mwanafunzi.
- Wanafunzi watahitaji Intaneti kwa ajili ya somo hili.
- Kuna fursa za kubadilisha maudhui yako ili yalingane na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Fursa hizi zimebainishwa kama "Dondoo za Mwalimu" katika hati nzima. Tunapendekeza kwamba ulipitie somo mapema na uandae mifano kabla ya kuanza kwa somo.
HIARI: USTADI WA ISTE DIGCITCOMMIT
- USAWA: Ninafanya maamuzi sahihi kuhusu namna ya kuupa kipaumbele muda na kazi zangu nikiwa na nisipokuwepo mtandaoni.
Jinsi Matukio Tuliyopitia Hutufanya Kuwa Watu wa Kipekee
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Tuanze siku ya leo kwa kutafakari kuhusu matukio tuliyopitia — hasa yale ya wakati uliopita na jinsi ambavyo yanaathiri tunavyo wasiliana na ulimwengu unaotuzunguka.
Matukio tuliyopitia ndiyo yanayofanya kila mmoja wetu kuwa mtu wa kipekee. Sote tumepitia mambo tofauti katika siku zetu za huko nyuma — baadhi ya mambo hayo yana upekee fulani kwetu.
Kumbukumbu hizi muhimu sana tunaweza kuziita "kumbukumbu kuu." Kuna mambo yaliyofanyika huko nyuma ambayo ndiyo kiini cha utambulisho na nafsi yetu.
Kwa mfano, huenda una ari kubwa kuhusu kucheza piano na mojawapo ya kumbukumbu zako kuu zaidi ni wakati ulipofanikiwa kucheza wimbo uliokuwa mgumu sana. Au pengine familia yako ni muhimu sana kwako na mojawapo ya kumbukumbu zako kuu zaidi ni likizo ambayo mlisherehekea kwa furaha ulipokuwa mdogo.
Wakati mwingine, kumbukumbu zetu kuu ni za furaha. Au, zinaweza kuwa za huzuni, kipuuzi au zisizohitaji mzaha — au hata mchanganyiko wa hisia hizi!
Bila kujali hali za matukio haya, yametusababisha tuuone ulimwengu kwa namna za kipekee.
DONDOO KWA MWALIMU
Mifano iliyoko hapo juu inaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Mifano hii inalenga kuwaonesha wanafunzi maana ya kumbukumbu kuu na jinsi inavyojenga sifa ya mtu.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sasa, ningependa mchague angalau moja ya matukio mnayokumbuka zaidi mliyopitia na kuyajadili katika makundi ya watu wawili wawili. Kwa nini unalikumbuka jambo hilo sana? Kumbukumbu hiyo imechangia vipi kukutengeneza wewe ulivyo sasa? Fikiria kuhusu
"Muonekano wa Haiba" katika video. Je, kumbukumbu hii imesaidia kutengeneza moja (au zaidi) ya muonekano wako (yaani kufafanua sehemu ya haiba yako)? Kama ndiyo, kwa njia gani? Una dakika 10 za kulijadili na mwenzako.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Wagawe washiriki katika makundi ya watu wawili wawili. Wape washiriki dakika 10 za kujadili maswali haya.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna yeyote anayetaka kuzungumzia mojawapo ya matukio aliyopitia yenye kukumbukwa zaidi?
- Baada ya kutafakari kuhusu namna matukio haya yalivyochangia kuifafanua haiba yako, je, kuna yeyote aliyejifunza jambo jipya au la kushangaza kujihusu?
Kutengeneza Matukio Mapya
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sote tuna kumbukumbu tofauti ambazo zinatupa njia ya kipekee ya kutazama na kuamiliana na ulimwengu.
Baadhi ya kumbukumbu hizi zina upekee fulani kwetu — kumbukumbu kuu — na zinasaidia kufafanua sisi ni watu wa aina gani.
Ikiwa tayari umekamilisha Sehemu ya 1: Jinsi Matukio Tuliyopitia Yanavyotufanya Kuwa Watu wa Kipekee, unaweza kutotilia maanani mifano ifuatayo.
Kwa mfano, tuseme kwamba unapenda sana kusoma na kuandika mashairi — upendo wako wa ushairi ni sehemu ya mambo yanayokufanya wewe kuwa wewe kama wewe! Pengine mojawapo ya kumbukumbu zako kuu ni mtu wa familia yako akikusomea mashairi ulipokuwa mdogo. Au pengine una ari ya kusafiri na kuzuru maeneo mapya ulimwenguni. Pengine mojawapo ya kumbukumbu zako kuu ni safari ya kupendeza ya nje ya nchi uliyosafiri ulipokuwa mdogo.
Ijapokuwa matukio tuliyopitia huko nyuma huathiri utambulisho wetu, tunaweza kutengeneza matukio mapya ya kukumbukwa na yenye kusisimua — kushuhudia matukio mapya na kutengeneza mahusiano mapya na watu na maeneo mbalimbali.
Mara nyingi, kulingana na machaguo tunayofanya, tuna uwezo wa kujitengenezea kumbukumbu mpya.
Baadhi ya machaguo hayo yanaweza kuonekana kuwa madogo. Lakini hata kufanya mabadiliko madogo katika maamuzi yetu ya kila siku kunaweza kuwa na athari itakayodumu kwa muda mrefu.
Kwa mfano, chukulia kwamba unataka sana kujifunza kucheza gitaa, lakini una wasiwasi kwamba huna wakati, kwa sababu ya kazi za shuleni na shughuli zingine za nje ya shule. Wakati wa juma, unaweza kupata muda usiokuwa na shughuli wa takriban saa moja tu na wewe hutumia muda huo kwa kupumzika na kutazama televisheni. Ni muhimu sana kufanya mambo yanayotutuliza, lakini itakuwaje kama ukitumia dakika 15 tu za saa hiyo moja kufanya mazoezi ya kupiga gitaa kila siku? Baada ya muda, kufanya hivyo kutakusaidia kuboresha ustadi na ujasiri wako wa kupiga gitaa!
DONDOO KWA MWALIMU
Mifano iliyoko hapo juu inaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu. Mifano iliyoko hapo juu inalenga kuonesha jinsi mambo tuliyopitia yanavyoathiri utambulisho wetu, lakini mambo mapya tutakayopitia pia yanaweza kuchangia kutujenga.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Leo, kila mmoja wenu atachagua lengo la kiwango cha wastani (yaani, lengo unalohisi kuwa litakuchukua angalau majuma kadhaa kulitimiza) ambalo daima umetaka kulitimiza lakini unahisi kuwa ni gumu sana na kisha ufikirie namna unavyoweza kulitimiza. Hili linaweza kuwa jambo lolote kama kuwa makini zaidi kufanya mazoezi mara nyingi, kujifunza kuhusu uwanja mpya wa kitaaluma ambao daima umetamani kuuelewa (kama vile upigaji picha au kipindi fulani katika historia).
Tuanze kwa kutumia dakika 15 zinazofuata kwa kukamilisha maswali yatakayowasaidia kufikiria kuhusu malengo mnayotaka kutimiza na mikakati mnayoweza kutumia ili kuyatimiza.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Sambaza kitini cha "Kuanza Jitihada Mpya" pamoja na kalamu za wino au penseli. Wape washiriki dakika 15 za kukamilisha kitini hicho.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Hebu tukusanyike pamoja.
Kwanza, unapokabiliana na changamoto mpya, ni muhimu sana ufikirie kuhusu mambo yanayokupa msukumo. Lengo letu hutusaidia kusonga mbele tunapokumbana na vizuizi katika jitihada zetu za kutimiza malengo yetu.
Pia ni muhimu kufikiria kuhusu matukio uliyopitia huko nyuma. Muhimu zaidi, tilia maanani malengo yenye changamoto ambayo umeyatimiza huko nyuma na jinsi ulivyotimiza malengo hayo. Je, kuna mikakati fulani uliyotumia — pengine ukizingatia mambo uliyokuwa umeyapitia hapo nyuma — ambayo yalikuwa na ufanisi mkubwa?
Kwa mfano, chukulia kwamba una lengo la kufanya mazoezi mara nyingi zaidi. Pengine mkakati mmoja uliotumia hapo nyuma ulikuwa kufanya mazoezi katika wakati wa siku unaokufaa zaidi — tuseme kama jambo la kwanza asubuhi. Au, kwa mujibu wa mambo uliyopitia hapo nyuma, unafahamu kuwa unafurahia kufanya mambo unapoyafanya na rafiki yako. Kama lengo lako ni kufanya mazoezi mara nyingi zaidi, mkakati mmoja unaoweza kutumia ni kufanya mazoezi pamoja na rafiki yako.
DONDOO KWA MWALIMU
Mifano iliyoko hapo juu inaweza kurekebishwa ili kuendana na mambo ambayo wanafunzi wako wanafahamu na pia muktadha wa eneo lenu.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna mmoja wenu ambaye angependa kuzungumzia wakati alipokumbana na lengo gumu huko nyuma na jinsi alivyolitimiza? Je, mambo uliyoyapitia huko nyuma yalichangia jinsi ulivyoikabili changamoto hiyo?
- Andika baadhi ya majibu ya washiriki kwenye chati ya mtiririko wa hatua/bango au ubao. Mawazo mengine huenda yakawapa wengine msukumo.
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Vizuri sana! Asanteni kwa kutoa majibu haya!
Unapofikiria kuhusu kujaribu kitu kipya, wakati mwingine unaweza kuzuiwa na woga — woga wa kutofanya au kutosema mambo yanayofaa au kutowaridhisha wengine au mwishowe kukosa kufanikiwa.
Lakini, kuna njia za kushinda woga huu. Kwa mfano, kuweza kuona hali fulani katika namna iliyo wazi zaidi kunaweza kukusaidia kubadilisha jinsi unavyokitazama kisa hicho ili namna zingine za kufikiria (kama vile, "Sina uzoefu wa kutosha wa kufanya jambo fulani!") zisikuzuie kutimiza malengo yako.
Kuna njia chache unazoweza kubuni za kupata mtazamo ulio wazi zaidi wa kufikiria kuhusu changamoto mpya.
Njia mojawapo ya kufanya hivyo ni kwa kufikiria kuhusu kile ambacho mtu mwingine angekwambia kama ungemwambia jambo ambalo unakusudia kulitimiza. Kwa mfano, kama utamwambia mmoja wa marafiki zako kuhusu changamoto mpya unayotaka kuikabili, unadhani atasema nini? Ni kwa namna gani atakusaidia?
Njia nyingine ni kwa kumuomba rafiki yako — au mtu mwingine unayemuamini, kama vile mwanafamilia, mkufunzi au mshauri — akupe ushauri moja kwa moja.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, umejaribu kitu chochote huko nyuma ambacho kilikusaidia kuliona lengo au tatizo fulani kwa mtazamo tofauti na hatimaye kukusaidia kuona suluhisho la changamoto hiyo kwa njia iliyo wazi zaidi?
Zoezi
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Sasa, hebu turudi kwenye changamoto unayotaka kuitatua ambayo uliandika kwenye kitini chako cha "Kukabiliana na Changamoto Mpya."
Unapoanza kufanya jambo jipya linaloonekana kuwa gumu, itakuwa vizuri kufikiria kuhusu mambo matatu muhimu tuliyojadili leo:
- Kwanza, ni lengo letu na mambo yanayotupa motisha.
- Pili, ni njia ambazo tumezitumia kuzikabili hali ngumu huko nyuma na mambo tuliyojifunza kutoka kwa mambo hayo tuliyopitia.
- Na la tatu, ni njia tunazoweza kutumia kupata mtazamo mpya kuhusu changamoto fulani.
Andika njia hizi katika chati mgeuzo/kipeperushi au ubao.
Hebu tuchukue mambo tuliyojifunza kisha tuyatumie kwa kubuni hatua halisi za kwanza unazoweza kutumia kutimiza lengo lako!
Nitawapa kielelezo cha kupanga shughuli za majuma manne ambapo ningetaka muandike, kwa kila wiki, angalau mambo mawili mnayoweza kufanya ili kulifikia lengo mnalotaka kutimiza. Hayatakiwi kuwa mambo makubwa — ni mambo yanayoweza kuchukua dakika 10 hadi 15 tu kwa kila juma! Fikiria kuhusu jinsi ambavyo, kama inatumika, mambo uliyopitia huko nyuma yalivyochangia hatua unazopanga kuchukua kisha uandike mawazo hayo katika safu ya tatu ya kitini chako. Mtatumia dakika 10 zijazo ili kukamilisha zoezi hili.
MAZUNGUMZO YA DARASANI
Sambaza kitini cha “Mpango wa Kutimiza Lengo Langu". Wape washiriki dakika 10 za kukamilisha kitini hicho.
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
- Je, kuna mtu anayetaka kuzungumzia baadhi ya hatua atakazozichukua ili kujaribu kutimiza lengo lake?
- Je, mambo uliyopitia huko nyuma yamechangia hatua unazokusudia kuchukua? Kama ndiyo, kwa njia gani?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO
Asanteni kwa kuzungumzia njia hizi nzuri mtakazotumia kutimiza malengo yenu!
Leo, tumejifunza kuwa ingawa matukio ya nyuma yamechangia kukujenga na kuwa kama ulivyo hivi sasa, unaweza kutengeneza matukio mapya, yenye changamoto na ya kusisimua, hata kwa kupiga hatua ndogo tu.
Katika siku zijazo, ningependa mfanye jitihada za kutimiza malengo yenu mkitumia hatua mlizoandika. Mjisikie huru kuwajulisha marafiki na jamaa zenu kuhusu mnavyoendelea!
Hongera!
Umekamilisha Somo
Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.