Ustawi wa Kidijitali

Somo 1: Sifa ya Mtandaoni

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Nani Anajua Siri Zako?

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Una siri gani inayokuhusu wewe? Weka siri hii akilini mwako. Hutakiwi kumwambia yeyote siri hii au kuiandika.

Sasa jibu maswali haya akilini mwako — usiyaseme majibu yako kwa sauti au kuyaandika:

 • Ni watu wangapi katika chumba hiki wanaoijua siri hii?
 • Ni majirani zako wangapi wanaoijua siri hii?
 • Ni watu wangapi ambao hujawahi kukutana nao ana kwa ana lakini wanaijua siri hii?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hebu fikiria kwamba ungelazimika kuandika siri hiyo kwenye karatasi kisha mtu yeyote katika kundi hili aisome.

Haya hapa ni maswali zaidi — kwa mara nyingine, yajibu tu akilini mwako, siyo kwa kuyatamka au kuyaandika. Baada ya juma moja kupita:

 • Ni watu wangapi katika chumba hiki ambao sasa wangeijua siri hii?
 • Ni watu wangapi katika majirani zako ambao sasa wangeijua siri hii?
 • Ni watu wangapi ambao hujawahi kukutana nao ana kwa ana ambao sasa wangeijua siri hii?

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Fikirieni watu ambao wanaweza kuona siri au taarifa nyingine zinazokuhusu kama "walengwa" wa taarifa hizo. Kuwa na uelewa mzuri wa walengwa wa maudhui yako kunaweza kukusaidia kujua kwa urahisi taarifa ambazo unahisi sio tatizo kuzisambaza na zile ambazo hufai kuzisambaza kwa wengine.

Walengwa wa maudhui ni mtu au kundi la watu ambao wanaweza kupata taarifa fulani. Huku kukiwa na teknolojia mpya zilizopo leo, walengwa wa maudhui wanaweza kuongezeka kwa kasi sana. Kwa sababu ya uwezekano huu wa kuongezeka kwa kwa kasi kwa walengwa wa maudhui, ni vigumu — au hata haiwezekani — kwako kufahamu au kudhibiti walengwa wa taarifa na shughuli zako za mtandaoni. Ingawa ni vizuri kwamba walengwa wa maudhui wanaweza kuongezeka kwa kasi unapotaka kuonesha watu wengi kazi yako, si jambo zuri hili litokee kwa taarifa ambazo unataka ziwe za siri.

Cha kusikitisha ni kwamba, taarifa za siri — hasusan taarifa za kuaibisha — mara nyingi husisimua watu wanapoziona, kwa hiyo baada ya taarifa za aina hii kufika mtandaoni tu, inaweza kuwa changamoto kudhibiti atakayeziona.

Kila unaposambaza taarifa mtandaoni (hata ikiwa unazituma moja kwa moja au kwa mtu binafsi, kama vile kupitia ujumbe binafsi), jiweke tayari ya kuwepo kwa uwezekano wa taarifa hizo kuenea kwa watu wengine mbali na walengwa uliowakusudia wafikiwe na taarifa hizo.

Sehemu ya 3

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Unapochapisha taarifa za matukio ya sasa, picha au taarifa nyingine katika mitandao ya kijamii, unataka nani azione?
 • Je, inategemea mitandao ya kijamii unayotumia? Au muktadha?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Inategemea na mipangilio yako binafsi pamoja na mitandao ya kijamii utakayochagua, lakini walengwa wa maudhui yako wanaweza kujumuisha marafiki zako wa karibu zaidi/wafuasi/watu ulio na mahusiano nao kwenye mtandao au kuwa kundi kubwa zaidi linalojumuisha mtu yeyote anayetumia mitandao hiyo ya kijamii au mtu yeyote atakayekutafuta mtandaoni. Lakini bila kujali walengwa wa maudhui akina nani, taarifa zinaweza kunakiliwa na kuchapishwa pahali pengine, mtu anaweza kupiga picha/kuchukua picha ya skrini inayoonesha maudhui hayo au taarifa zinaweza kusambazwa kupitia mawasiliano ya mtu na mtu na ya mtandaoni.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Je, unapochapisha kitu katika mitandao ya kijamii, ni akina nani unawalenga?
 • Ni akina nani unawalenga kwa mfano, unapochapisha kwenye ukurasa wa Facebook wa mtu mwingine au unapoweka maudhui kwenye akaunti ya mtu mwingine katika mitandao ya kijamii (mfano, kwa kuweka maoni katika moja ya picha zake au kumshirikisha katika chapisho au picha)?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hii itategemea mipangilio yako binafsi na pia ya rafiki yako, lakini mara nyingi maudhui hayo yataonwa na marafiki/wafuasi/watu ulio na mahusiano nao katika mtandao huo, ambao ni pamoja na watu usiowafahamu — hii inaweza kuwa ni pamoja na watu wa familia yake au wasimamizi au walimu wa shule yake.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Unapotuma ujumbe (mfano, ujumbe, barua pepe, ujumbe binafsi/moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii), ni akina nani unawalenga?
WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Mlengwa wa ujumbe huo ni mtu unayemtumia, lakini kuwa mwangalifu — watu wengine wanaweza pia kuuona.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ujumbe wako unaweza vipi kuwafikia watu wengine mbali na mtu uliyemtumia? Njia zinazoweza kutumika ni pamoja na kupiga picha/picha za skrini, kutuma ujumbe huo kwa watu wengine na kutuma ujumbe huo kwa mtu binafsi kwa kupitia simu.
 • Ni katika hali gani kuwafikia walengwa wengi kunaweza kuwa na manufaa? Mifano inaweza kuwa kama wakati unakusudia kusambaza ujumbe kwa watu wengi au kuhamasisha watu.
 • Ni katika hali gani ambapo kuwafikia walengwa wengi zaidi ya wale uliowakusudia linaweza kuwa ni tatizo? Kusambaza maudhui kwa wasiokuwa walengwa kunaweza kukuweka hatarini, kukusababishia aibu na kukuharibia sifa.
 • Je ni zipi baadhi ya hali ambapo udumishaji wa sifa ya mtandaoni kunaweza kuwa muhimu? Mifano inaweza kujumuisha wakati wa kuomba nafasi katika shule/chuo/chuo kikuu, kuomba nafasi za kazi na kujenga urafiki na watu wapya.

Kutafiti Kuhusu Sifa Yako

Sehemu ya 1

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Mwalimu achague mtu mashuhuri (mfano, mtu aliye katika tasnia ya muziki, filamu, televisheni, mwanasiasa, kiongozi wa kibiashara) ambaye anajulikana kwa wanafunzi. Tafuta jina la mtu huyo katika injini ya utafutaji ya mtandaoni. Kisha pamoja na wanafunzi, tathmini baadhi ya mambo yatakayojitokeza (tafadhali onesha matokeo ya utafutaji kwenye skrini).

Pia chunguzeni uwepo wa mtu huyo mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii. Baada ya kutumia dakika chache kuchunguza, waombe wanafunzi wawili waigize uhusiano wa kubuniwa kati ya mtu huyo mashuhuri na shabiki wake.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Je, unapata hisia gani unapokutana na mtu mwenye taarifa nyingi sana kuhusu wewe?
 • Je, utapata hisia gani endapo taarifa hizo sio sahihi?
 • Ni watu wangapi wanaoweza kuzipata taarifa hizo?
 • Unawezaje kudhibiti taarifa zako ambazo zinaweza kupatikana mtandaoni?

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Watu unaokutana nao watatumia injini za utafutaji ili kupata taarifa zaidi kuhusu wewe. Habari watakazopata, ziwe nzuri au mbaya, zitachangia kile wanachofikiria juu yako. Ikiwa unataka kudhibiti jinsi wanavyokuchukulia ni muhimu ufahamu taarifa ambazo wanaweza kuzipata mtandaoni.

Watu hawa ni pamoja na waajiri wako wa baadaye na maafisa udahili katika shule, vyuo au vyuo vikuu. Maafisa udahili huenda wasiwaambie waombaji ikiwa walitafuta au hawakutafuta taarifa zao mtandaoni na/au walitumia taarifa hizo kufanya maamuzi yao.

Sehemu ya 3

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Fikirieni kuhusu mambo matatu ambayo mngetaka yaonekane mtu anapotafuta majina yenu mtandaoni. Je, mnadhani ni kwa vipi mambo hayo ndiyo yatakayotokea katika matokeo ya utafutaji? Jadiliana na mwenzako.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Wewe na mwenzako mmepata majibu gani?
 • Inua mkono kama umetafuta jina lako mtandaoni. Umeona nini? Ni picha gani zilizotokea? Je, umeweza kupata taarifa zinazokuhusu wewe, au kuna watu wengine duniani wenye jina sawa na lako?
DONDOO ZA MWALIMU

Ikiwa wana majina sawa, omba wanafunzi waongeze taarifa zaidi kwenye utafutaji wao, kama vile mji wanaotoka ama jina la shule yao.
Pia unaweza kuwaomba wanafunzi watafute majina yao katika Google/mtandaoni wakati wa zoezi hili ikiwa kuna kompyuta au simu za mkononi zilizo unganishwa na intaneti.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Wakati wa kutafuta jina lako mtandaoni, uliza maswali haya manne:
  • Ni yapi matokeo machache ya kwanza?
  • Unaridhika na taarifa hizo?
  • Yale matokeo mengine yanapendekeza kwamba wewe ni mtu wa aina gani? Kama mwanafunzi? Kama muajiriwa?
  • Mtu asiyekufahamu anaweza kukuchukulia vipi baada ya kuziona taarifa hizo? Atapata taswira gani kuhusu wewe ikiwa atabofya na kusoma taarifa zilizo katika matokeo machache ya kwanza?Kushughulikia Taarifa Changamano
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi hati ya "Unatakiwa kufanya nini?". Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili. Waambie wanafunzi wajadili matukio yaliyo kwenye hati hii kisha wabuni mikakati/masuluhisho mawili kwa kila tukio na wafikirie kuhusu mambo yanayoweza kusababishwa na hatua watakazochukua. Wape dakika 15 kulikamilisha zoezi hilo.

DONDOO KWA MWALIMU

Vitini hivyo vinalenga kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kutafakari kwa kina kuhusu tabia zao za mtandaoni na namna wanavyowatendea watu wengine. Majina na mifano iliyopo kwenye vitini inaweza kuwa ya kawaida ili iendane na majina ya watu yanayotumika sana na shughuli za kawaida katika eneo unalofundisha. Kwa mfano:

 • Ethiopia: Samira, Meskerem, Hiwot na Lidya
 • Kenya: Chebet
 • Zambia: Yonah na Abigail

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Unatakiwa kufanya nini pindi mtu anapochapisha maudhui kuhusu wewe ambayo hupendi na/au hupendezwi nayo kwa muktadha uliotumika?
 • Unatakiwa ufikirie nini kabla ya kuchapisha maudhui kuhusu mtu mwingine?

Kuzijibu Taarifa Mbaya

Sehemu ya 1

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
 • Ikiwa utapata taarifa mbaya kuhusu wewe baada ya kutafuta jina lako mtandaoni (mfano; kupitia injini ya utafutaji au mitandao ya kijamii). Je, unaweza kuifanya lolote?
 • Kuna mifano gani ya maudhui ambayo usingependa watu wengine wayaone?

Sehemu ya 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Kuna mitazamo tofauti kuhusu kile unachoweza kukifanya ikiwa utaona maudhui mtandaoni yanayokuhusu ambayo hupendi, kulingana na muktadha na aina ya maudhui hayo.

Mtazamo wa kwanza ni "kubadili maudhui" yaani kwa kuyabadili maudhui usiyopenda kwa kuonesha/kutoa mambo mazuri yanayokuhusu kwa kutengeneza na kusimamia maudhui yanayoonesha sifa zako nzuri. Kwa mfano, unaweza kufanya hivi kwa kutengeneza maudhui na shughuli zako katika mitandao ya kijamii wakati unaofaa, kuanzisha blogu au kusajili tovuti inayotumia jina lako.

Mtazamo wa pili ni kutumia njia tofauti za kuondoa maudhui mabaya mtandaoni yanayokuhusu. Kwa mfano, ukiona maudhui ambayo hupendi (mfano; picha yako), unaweza kujaribu kuwasiliana moja kwa moja na mtu aliyeichapisha (hususan kupitia mitandao ya kijamii/programu za kutuma ujumbe) na kumuomba ayatoe maudhui hayo.
Mitandao mingi pia hukupa uwezo wa kutambua taarifa zinazokukera au maudhui yasiyokufurahisha (mfano; picha, video, machapisho yenye maandishi) ambayo yanatoa taswira mbaya; maudhui ambayo hayafai kuwa kwenye mtandao huo (mfano; yanaudhi, yanaonesha vurugu au ni marufuku); pamoja na maudhui yanayoonekana kuwa ya udanganyifu. Kisha tovuti hiyo inalinganisha ripoti hiyo na masharti yake ya matumizi pamoja na kanuni za kijamii.

Katika hali zingine, huenda ukataka kuchukua hatua za kisheria kwa mfano, unaweza kupeleka mashtaka mahakamani, kulingana na mamlaka na sheria inayotumika (mfano; katika visa vingine vya uvujaji wa siri au kutoa madai ya uongo yanayoharibu sifa ya mtu). Nchi zingine zina sheria mahususi ambazo zinazitaka tovuti kuondoa aina nyingine za maudhui ambayo siyo ya kweli baada ya kuarifiwa (mfano; Sheria ya Taarifa na Mawasiliano ya Kenya (Marekebisho ya 2019)).

Dondoo kwa Mwalimu

Mfano huu unalenga kuwafundisha wanafunzi kuhusu sheria zinazosimamia mitandao ya kijamii na data katika nchi yao. Sheria zinazosimamia mitandao ya kijamii na ulinzi wa data zinaweza kurekebishwa zaidi ili kuendana na maudhui ya mazingira ya wanafunzi katika eneo unalofundisha. Kwa mfano:

 • Kenya: Sheria ya Taarifa na Mawasiliano ya Kenya (Marekebisho ya 2019) husimamia matumizi ya mitandao ya kijamii.
 • Nigeria: Nchini Nigeria, kila raia ana haki ya kupata siri ya data zake, kwa mujibu wa Kifungu cha 37 cha Katiba ya 1999. Hili lipo katika haki, unaweza kupeleka mashtaka mahakamani kama haki hii itavunjwa.
 • Zambia: Nchini Zambia, Sheria ya Usalama wa Mtandao na Uhalifu wa Mtandaoni, 2021.

Tafadhali pia kumbuka kwamba wakati mwingine, kujaribu kukandamiza/kuondoa/kurekebisha maudhui kunaweza kuwavutia watu zaidi, kinyume na unavyotaka.

Sehemu ya 3

DONDOO KWA MWALIMU

Katika Sehemu ya 3, jadili sheria na kanuni zozote za ulinzi wa data katika nchi au eneo lako ambazo zinaweza kuwa zinaendana na wanafunzi wako. Mfano huu unalenga kuwafundisha wanafunzi kuhusu sheria zinazosimamia mitandao ya kijamii na data katika nchi yao, ili wawe raia wa kidijitali wenye maarifa zaidi. Kwa mfano:

 • Kenya: Sheria ya kwanza ya ulinzi wa data ya Kenya ilianza kutumika mnamo Novemba 25, 2019. Sheria hii inawezesha utekelezaji wa Kifungu cha 31(c) na (d) cha Katiba ya Kenya ya 2010 inayotoa haki ya kuwa na siri. Sheria hii inampa mtu anayetambulishwa na data hizo haki ya kurekebisha data zenye makosa au za kupotosha, kufuta data zenye makosa au za kupotosha, na kusahihisha data zake, sawa na sheria ya GDPR ya Muungano wa Ulaya. Mtu anayedhibiti au kuchakata data ana wajibu wa kutoa njia ambazo mtu anayetambulishwa na data anaweza kuwasilisha maombi ya kurekebishwa kwa data hizo. Maelezo yaliyo katika Sehemu za 26, 27, 29, na 30 ni muhimu ili kutoa ridhaa ya ufahamu kabla ya kuchakatwa kwa data. Mtu anayetambulishwa na data anafaa kujulishwa kwamba data zake zinakusanywa, na wahusika wote ambao data hizo zimetumwa au zitatumwa kwao, pamoja na maelezo kuhusu mikakati iliyowekwa ya kudumisha usalama wa data. Sera ya kitaifa ya ulinzi wa data ya nchi ya Kenya hutoa maelezo kuhusu usimamizi wa data binafsi katika hatua zote za kuchakatwa kwa taarifa hizo na jinsi Serikali ya Kenya ilivyojitolea kulinda data binafsi, pamoja na data nyeti za siri.
 • Nigeria: Kuna sheria ya ulinzi wa data nchini Nigeria inayojulikana kama Sheria ya Ulinzi wa Data ya Nigeria (NDPR) iliyotolewa na Wakala wa Taifa wa Maendeleo ya Habari na Teknolojia (NITDA) mnamo Januari 2019 ili kudhibiti jinsi data za raia na wakazi wa Nigeria zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa. Sheria hii pia hutumika kwa watu wote wanaotambulika kisheria ambao wanaishi nchini Nigeria au wanaishi nje ya Nigeria ila wana asili ya Nigeria. Ijapokuwa sheria ya NDPR haina orodha ya hali ambapo sheria hii haitatumika, haki yako ya kuwa na siri kwa mujibu wa Katiba ya Nigeria ya 1999 inaweza kuondolewa kwa ajili ya maslahi ya umma, usalama wa taifa, afya ya umma na katika utetezi wa mashtaka ya kisheria. Kwa hiyo, ingawa Sehemu ya 37 ya Katiba inasema kwamba siri za raia, nyumba zao, barua na mawasiliano ya simu inahakikishwa na kulindwa, Sehemu ya 45 ya Katiba inasema kuwa haki ya mtu ya kuwa na maisha ya siri inaweza kuondolewa kwa sababu ya kulinda maslahi ya umma na kulinda haki na uhuru wa watu wengine. Pia kuna vipengele vingine vya sheria vyenye sehemu mbalimbali ambavyo vinazungumzia ulinzi wa data wa raia wa Nigeria. Mfano ni Sehemu ya 8 ya Sheria ya Haki za Watoto ya 2003 na Sheria ya Ulinzi wa Wateja ya 2016. Sheria hizi zote zinalenga kuhakikisha kwamba haki ya kuhifadhiwa kwa data zako kwa njia salama, kwamba data zako zitatumiwa kwa njia halali, kupata maelezo kuhusu jinsi data zako zitakavyotumika na haki ya kurekebisha/kufuta data binafsi zinaheshimiwa.
 • Zambia: Nchini Zambia, tuna haki zetu zinazosema kuwa tuna haki ya kutoruhusu data zetu kuhifadhiwa mtandaoni na tuna haki ya kuomba data hizo zifutwe.

Zoezi

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa kwa kuwa tumejifunza kuhusu jinsi ambavyo taarifa zinazopatikana kwa umma zinavyoweza kuchangia maoni kuhusu watu wengine, hebu sasa tutumie maarifa ambayo mmejifunza hivi sasa. Katika muda wa dakika 30 zijazo, ukiwa peke yako, fanya zoezi lifuatalo.

Chagua mtu mashuhuri (mfano, mtu aliye katika tasnia ya muziki, filamu, televisheni, mwanasiasa, kiongozi wa kibiashara). Tafuta taarifa zinazopatikana kwa umma mtandaoni kuhusu mtu huyo na kwa mistari michache, eleza jinsi ambavyo taarifa hizo zimekusaidia kupata mtazamo kuhusu mtu huyo.

Kama ungeweza kumpa mtu huyu mapendekezo manne kuhusu jinsi maudhui kuhusu yeye yanavyoweza kupatikana mtandaoni kwa njia tofauti (mfano, kwa kubadilisha mipangilio binafsi, kubadilisha walengwa wa maudhui yake, kubadilisha kipengele fulani cha maudhui hayo) na/au maudhui yake yasiweze kupatikana kabisa (mfano, yafutwe au yaondolewe) ili kuboresha taswira ambayo mtu huyu anaonesha/jinsi watu wengine wanavyomchukulia mtandaoni, ungependekeza nini?

Wape wanafunzi dakika 30 ili wakamilishe zoezi hili.

End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy