Ustawi wa Kidijitali

Somo 2: Mitandao ya Kijamii na Usambazaji Taarifa

Kabla ya kuanza somo, hakikisha umesoma muhtasari wa somo na matayarisho ya somo. Mwongozo wa Muwezeshaji unaweza pia kukusaidia kujitayarisha.

Muhtasari wa Somo


Matayarisho ya Somo


Begin Lesson

Tayari?
Anza Somo

Matumizi ya Mitandao ya Kijamii

DONDOO ZA MWALIMU

Kabla ya zoezi hili, bandika vibao vya NINAKUBALI na SIKUBALI katika pande zinazoelekeana za chumba.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Wafahamishe wanafunzi kwamba baada ya kusoma kila kauli, wanafaa kusimama karibu na upande mmoja au wa pili kulingana na maoni waliyo nayo; wanafunzi wanaweza pia kusimama katikati mwa vibao hivyo viwili ikiwa hawana uhakika/hawajaamua.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Kati ya kauli moja na nyingine, waombe wanafunzi waelezee maoni yao na uendeshe mijadala mifupi kwenye kundi kuhusu kila mada.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Nitasoma kauli fulani. Kama unakubaliana nayo kwa asilimia 100, nenda kwenye kibao cha "NINAKUBALI". Kama hukubaliani nayo kabisa, nenda kwenye kibao cha "SIKUBALI". Ikiwa huna uhakika au hukubaliani nayo/huipingi kabisa, nenda katikati na usimame katika sehemu inayowakilisha msimamo wako vizuri zaidi.

  • Nina akaunti katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Snapchat au Instagram.
  • Ninatumia mitandao ya kijamii kila siku.
  • Wasifu wangu wa mitandao ya kijamii — kwenye mitandao ya kijamii ninayotumia zaidi — uko wazi kwa umma.
  • Nina marafiki/wafuasi/mtandao (yaani watu wa aina tofauti wanaopokea maudhui yangu) katika mitandao tofauti ya kijamii ninayotumia.
  • Watu wa umri wangu wana njia tofauti ya kufikiria kuhusu taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii ikilinganishwa na watu wazima.
  • Ninatumia mitandao tofauti ya kijamii ili kuchapisha aina mahususi za maudhui.

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Mitandao ya kijamii ni mifumo ya mtandaoni inayoweza kutumika kukutanisha na watu na kuwasiliana nao.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Ni mitandao gani ya kijamii ambayo mmeisikia?

Sehemu ya 2

DONDOO KWA MWALIMU

Kabla ya zoezi lifuatalo, bandika vibao vya NINAKUBALI na SIKUBALI katika pande zinazoelekeana za chumba.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wafahamishe wanafunzi kwamba baada ya kusoma kila kauli, wasimame karibu na upande mmoja au wa pili kulingana na maoni waliyo nayo. Wanafunzi wanaweza pia kusimama katikati ya vibao hivyo ikiwa hawana uhakika/hawajaamua. Kati ya kauli moja na nyingine, endesha majadiliano mafupi ukitumia maswali yaliyo chini ya kila kauli.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Nitasoma kauli fulani. Kama unakubaliana nayo kwa asilimia 100, nenda kwenye kibao cha "NINAKUBALI". Kama hukubaliani nayo kabisa, nenda kwenye kibao cha "SIKUBALI". Ikiwa huna uhakika au hukubaliani nayo/huipingi kabisa, nenda katikati na usimame katika sehemu inayowakilisha msimamo wako vizuri zaidi.

Katika zoezi hili, fikiria kuhusu mitandao ya kijamii unayotumia zaidi.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Mitandao yangu ya kijamii iko wazi kwa umma.
    • Je, hii inabadilisha namna ambavyo unachapisha maudhui mtandaoni? Kivipi? Au kama siyo, kwa nini siyo?
  • Mitandao yangu ya kijamii ni kwa ajili ya mawasiliano na marafiki/watu ninaofahamu vizuri sana tu.
    • Ni kwanini ulifanya uamuzi huu?
    • Je, ungechapisha maudhui tofauti kama kila mtu angeweza kuyaona? Ni maudhui ya aina gani?
  • Nina rafiki/mfuasi/mtu niliye na urafiki naye katika mitandao ya kijamii ambaye sijawahi kukutana naye ana kwa ana.
    • Kwa nini ukawa rafiki/mfuasi/uhusiano wa mtandaoni na mtu huyu? Je, ni mtu ambaye ulikutana naye mtandaoni au hamjawahi kuwa na mawasiliano yoyote hapo kabla?
    • Unawezaje kueleza uhusiano huo?
    • Kwa kuwa mnawasiliana mtandaoni tu, je, hii inaathiri jinsi mnavyowasiliana? Ni yapi baadhi ya manufaa ya mawasiliano ya aina hii? Ni changamoto zipi zinazoweza kujitokeza?
  • Ninakubali kila ombi la rafiki/mfuasi/mtandao ninalopata.
    • Ni yapi manufaa ya mtazamo huu? Ni changamoto zipi zinazoweza kujitokeza?
    • Je, maombi ya marafiki/wafuasi/wahusiani wa mtandaoni yana athari yoyote katika siri zako? Kama ndiyo, kwa namna gani? Kama siyo, kwa nini siyo?
  • Kila ninapokutana na watu wapya, ninawatumia ombi la urafiki/mfuasi/mahusiano ya mtandaoni.
    • Kwa nini hili ni wazo zuri/baya?
WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Katika mtandao, mimi ni rafiki na mfuasi wa mtandaoni wa wazazi/walezi au walimu wangu.
    • Je, hii inabadilisha maudhui unayoposti?
    • Je, watu wazima hutoa maoni kuhusu mambo unayochapisha mtandaoni?
    • Kuna manufaa na/au changamoto zipi zinazoweza kutokea kutokana na kuwa na urafiki/wafuasi/wahusiani na wazazi/walezi au walimu wako?
  • Nimewahi kufuta watu kama marafiki/wafuasi/wahusiani wa mtandaoni.
    • Ni kwanini ulifanya uamuzi huu?
  • Mambo mengine kwenye wasifu wangu yanaweza kuonwa na marafiki wa marafiki zangu/watu ambao sina mahusiano nao ya moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.
    • Ni mambo gani?
  • Nimeangalia na/au kubadilisha mipangilio yangu binafsi.
    • Kwa nini au kwa nini siyo?
    • Mipangilio hii binafsi ilikuwa rahisi au inachanganya? Ni nini kinachoweza kurahisisha kutazama/kubadilisha mipangilio hii?

Mtandao Wako ni Mkubwa Kiasi Gani?

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa tuzungumzie idadi ya watu wanaoweza kufikiwa na maudhui yako katika mitandao ya kijamii. Kuna njia mbili kuu za kusambaza maudhui (mfano, picha, video, chapisho la maandishi) ili kufikia walengwa. Maudhui yanaweza kusambazwa kwa walengwa halisi, ambao wanaweza kuwa marafiki/wafuasi/watu ulio na mahusiano nao kwenye tovuti fulani au pia inaweza kujumuisha marafiki wa marafiki zako. Pia, walengwa wa mwanzo wa maudhui yako wanaweza kusambaza maudhui hayo kwa marafiki/wafuasi/watu walio na mahusiano nao kwenye tovuti fulani.

Pengine utapendelea kuchagua walengwa wako wa moja kwa moja, lakini ni vigumu zaidi kudhibiti watu ambao walengwa wa maudhui yako watasambaza tena/watachapisha tena tena maudhui hayo.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Chukulia kwamba unasambaza maudhui yako na marafiki/wafuasi/watu ulio na mahusiano nao kwenye tovuti fulani kisha maudhui hayo hayo pia yanasambazwa na walengwa wako na marafiki/wafuasi/watu walio na mahusiano nao kwenye tovuti fulani. Unadhani ni watu wangapi unaowasambazia maudhui yako?

Sehemu ya 2

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Andika milinganyo/matokeo yafuatayo kwenye ubao.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Hebu tufanye hesabu. Kwa mfano, ikiwa una marafiki/wafuasi/watu wawili ulio na mahusiano nao kwenye mitandao ya kijamii na kila mmoja wao ana marafiki/wafuasi/watu watatu walio na mahusiano nao kwenye tovuti hiyo. Basi ni watu wangapi, kwa ukadiriaji wa juu zaidi (marafiki/wafuasi/watu wengine wenye mahusiano nao kwenye tovuti hiyo huenda wakajirudia) wanaweza kuona maudhui uliyosambaza kwenye mitandao hiyo ya kijamii?

  • Jibu: 2 + 2 x 3 = 8

Ikiwa una marafiki/wafuasi/watu 10 ulio na urafiki nao kwenye mtandao ya kijamii na kila mmoja wao ana marafiki/wafuasi/watu 10 alio na urafiki nao. Basi kwa ukadiriaji wa juu zaidi ni watu wangapi wanaoweza kuona maudhui uliyosambaza kwenye mitandao hiyo ya kijamii?

  • Jibu: 10 + 10 x 10 = 110

Ikiwa una marafiki/wafuasi/watu 300 ulio na mahusiano nao kwenye mtandao wa kijamii na kila mmoja wao ana marafiki/wafuasi/watu 300 walio na mahusiano nao, basi kwa ukadiriaji wa juu zaidi, ni watu wangapi wanaoweza kuona maudhui uliyosambaza kwenye mtandao huo wa kijamii?

  • Jibu: 300 + 300 x 300 = 90,300

Hesabu hizo zimefanywa huku ikichukuliwa kwamba walengwa wa moja kwa moja wa maudhui yako huyasambaza kwa walengwa wao wa moja kwa moja. Lakini maudhui hayo hayasambazwi tena baada ya hapo. Hata hivyo, katika hali nyingi, maudhui yanaweza kusambazwa na watu zaidi mbali na makundi hayo mawili ya walengwa wa kwanza.

Sehemu ya 3

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Mtazamao wako ukoje juu ya uwezekano kwamba watu wengi sana ambao pengine huwajui (labda unajua baadhi ya marafiki wa marafiki zako) wanaweza kufahamu kwa urahisi sana kuhusu unayofanya mtandaoni? Jambo hili linaweza kuwa na athari gani mbaya na/au nzuri?
  • Kwa nini suala hili ni muhimu?
  • Je, suala hili linabadili jinsi unavyofikiria kuhusu kusambaza maudhui mtandaoni? Kwa nini au kwa nini siyo?

Kusambaza Maudhui Mtandaoni

Mjadala wa 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Unaweza kusambaza maudhui mtandaoni ukilenga yawafikie walengwa mahususi. Hata hivyo, ukifanya maudhui hayo yaweze kuonekana na kila mtu, huenda yakawafikia watu ambao hukutarajia. Maudhui yaliyosambazwa mtandaoni yanaweza kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, huku yakinakiliwa jinsi ulivyoyachapisha au pengine yakifanyiwa mabadiliko.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kuna mtu yeyote anayeweza kufikiria kuhusu maudhui yaliyosambaa sana?
  • Kama siyo, waulize kuhusu kichekesho, nyimbo/video zilizofanyiwa mabadiliko, au video maarufu ambazo wameona na/au kusambaza kwa marafiki zao.
MAZUNGUMZO YA DARASANI

Onesha mfano wa hivi sasa unaoendana na mazingira yako/mazingira ya wanafunzi wako/mazingira ya ukanda wako ili kueleza wazo hili zaidi.

DONDOO KWA MWALIMU

Mfano huo wa maudhui yaliyosambaa sana unaweza kurekebishwa ili kuendana na maudhui ya mazingira ya wanafunzi katika eneo unalofundisha. Mfano huu unalenga kuwaonesha wanafunzi maudhui yaliyosambaa sana mtandaoni ili kuwafundisha kwamba baada ya maudhui kuingia mtandaoni, huenda ikawa vigumu kudhibiti watu watakaoyaona. Kwa mfano:

  • Ghana: #WasichanaWaTakoradi, kisa maarufu sana kuhusu kutekwa nyara kwa wasichana watatu.
  • Kenya: Msanii wa nchi hiyo anayefahamika kama Embarambamba alichapisha video alipokuwa akijivingirisha kwenye matope na kufanya vitendo vya kushangaza. Kwa kuwa matendo haya yalikuwa ya kipekee sana, video zake zilisambaa sana na hata akapata fursa ya kuhojiwa katika kipindi cha televisheni nchini Kenya kinachojulikana kama "The Trend."
  • Nigeria: Picha hii maarufu iliyochapishwa kwenye Twitter ilisambaa sana. Ilianza tu kama chapisho la mtumiaji wa Twitter ambaye hakufahamu kwamba ingesambaa sana.
  • Zambia: Video ya Kevin Hart bandia ilisambaa sana nchini Zambia.

Mjadala wa 2

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Maudhui yanayosambaa sana yanaweza kuwa na manufaa ikiwa unataka watu waifahamu kazi yako. Hata hivyo, taarifa zikiwafikia watu usiowakusudia zinaweza kusababisha unyanyasaji na dhuluma ya mtandaoni. Video ya siri ikivuja au kusambazwa bila ruhusa yako inaweza kukuharibia sifa.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Kuna njia zipi ambazo maudhui yaliyo mtandaoni yanayokuhusu yanaweza kusambazwa mbali na walengwa uliowalenga na hali hii inaweza kukuathiri vipi wewe na/au sifa yako?

Machaguo ya Siri ya Mitandao ya Kijamii

Sehemu ya 1

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa kwa kuwa tumezungumzia baadhi ya sababu za kutopendelea kila unachofanya mtandaoni kiweze kuwa wazi kwa umma, basi tuzungumzie jinsi tunavyoweza kusimamia siri zetu mtandaoni.

Sehemu ya 2

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Kati ya swali moja na lingine, toa ufafanuzi wa mjadala ukitumia kauli zinazofuata kila swali.

WAULIZE WANAFUNZI WAKO
  • Je, ni muhimu kuwa na mipangilio tofauti binafsi kwa ajili ya taarifa za aina tofauti? Huenda ukachukulia kwamba taarifa tofauti zina viwango tofauti vya siri. Pengine ungetaka kuchapisha picha yenye uso wako, kuhusu mitazamo yako ya kisiasa au kidini, au kisa kuhusu video ya kuchekesha ili kuwafikia walengwa tofauti.
  • Vipi kuhusu mipangilio binafsi tofauti kwa ajili ya watu tofauti? Kwa mfano, je, wazazi/walezi wako na marafiki zako huona maudhui sawa kwenye akaunti zako za mitandao ya kijamii? Pengine wanafunzi hawatataka jamaa zao waweze kuona machapisho yao lakini wangetaka marafiki zao watoe maoni kuhusu machapisho hayo.
  • Je, unaweza kurudi nyuma na kupitia maudhui yote ambayo umeshirikishwa? Kwa nini au kwa nini siyo? Pengine utataka kuondoa maudhui yoyote ya kuaibisha (mfano, picha ambayo nywele zako hazipendezi au chapisho linalokuhusu ambalo hutaki lisambazwe). Katika mitandao mingine ya kijamii, kama vile Facebook, unaweza kubadilisha mipangilio yako ili kuweza kuidhinisha maudhui fulani kabla ya kuonekane kwenye wasifu wako. Unadhani hilo ni wazo zuri? Kwa nini au kwa nini siyo? Mifano ni kama kukusaidia kuepuka kuwa na maudhui ya aibu kwenye akaunti yako ya mitandao ya kijamii. Hata hivyo, kufanya hivyo hakuzuii mtu anayechapisha maudhui hayo asiyachapishe kwenye akaunti yake ili kuonekana na marafiki/wafuasi/watu alio na mahusiano nao kwenye mtandao huo wa kijamii.
  • Kwa nini mtu angetaka kudhibiti watu wanaoweza kutazama taarifa zake? Unaweza kutoa mfano? Pengine hutaki watu wageni/watu usiowafahamu vizuri wawe marafiki/wafuasi/wahusiani wako katika mitandao ya kijamii au wakutumie ujumbe ambao hutaki.
  • Je, wewe ni rafiki ya wafuasi/wahusiani wa wazazi/walezi wako katika mitandao ya kijamii? Walimu? Watu wengine wazima? Je, hali hii inabadilisha aina ya maudhui unayosambaza au watu unaoshiriki nao maudhui hayo? Je, wazazi/walezi au walimu wanahitaji kuwa marafiki za/ wafuasi wa/kuwa na mahusiano nawe katika mitandao ya kijamii ili kuona wasifu wako?
    • Wanafunzi wanatakiwa kuzingatia ikiwa mipangilio yao binafsi inaruhusu watu wote kuona wasifu wao wa mitandao ya kijamii. Wasaidie kufikiria kuhusu njia nyingine ambazo wazazi/walezi au walimu wanaweza kuona wasifu wao.
  • Vipi kuhusu kutumia mipangilio binafsi tofauti katika mitandao tofauti ya kijamii? Katika Twitter, machapisho yako huwa wazi kwa umma au ni ya siri? Ni watu wangapi wanaoweza kuona machapisho yako ya Snapchat?
  • Ni watu wangapi wanaoweza kuona kile ulichoweka katika Instagram? Je, watu wengine wanaweza kutazama video zako katika YouTube? Mbali na picha ya wasifu wako, watu wanaweza kuona picha zako zingine katika Facebook? Ikiwa wanafunzi hawajui, waambie kuna mipangilio binafsi kwa ajili ya hayo yote.
  • Unapochapisha maudhui katika Twitter, unatumia jina lako halisi au bandia? Kwa nini? Wanafunzi pengine hawataki watu wote wajue majina yao halisi. Katika hali hii, huenda wakatumia majina bandia.

Sehemu ya 3

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wapange wanafunzi katika makundi ya watu wawili wawili.

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Tunafahamu kwamba mipangilio binafsi inaweza kuwa na utata. Katika makundi yenu ya watu wawili wawili, tumieni dakika chache kubuni swali au maoni kuhusu mipangilio binafsi.

MAZUNGUMZO YA DARASANI

Wape wanafunzi dakika tano ili wabuni swali au maoni kuhusu mipangilio binafsi. Waombe walishirikishe kundi zima kuhusu mambo waliyopata na kujibu kila swali walilotunga. Omba majibu kutoka kwa wanafunzi wengine kabla ya kutoa jibu lako. Ikiwa mna kompyuta au simu za mkononi zilizounganishwa kwenye intaneti, waoneshe jinsi ya kuthibiti mipangilio binafsi mtandaoni.

Zoezi

WAAMBIE WANAFUNZI WAKO

Sasa kwa kuwa tumezungumzia siri katika mitandao ya kijamii, hebu tuendeleze somo hilo kwa kubuni mwongozo unaoweza kutumika kuwasaidia wengine kujifunza mambo ambayo mmejifunza sasa hivi.

Katika muda wa dakika 30 zijazo, ukiwa peke yako, tengeneza mwongozo mfupi wa kuwasaidia wengine:

  • Fikiria kuhusu walengwa wa machapisho yao katika mitandao ya kijamii.
  • Wafikirie kuhusu mambo ambayo wangependa yaonekane kwa umma na yale ambayo wangependa yawe ya siri na kwa sababu gani.
  • Zingatia sababu ambazo huenda zikawafanya kukagua na/au kubadilisha mipangilio yao binafsi katika mitandao ya kijamii.
  • Fikiria kuhusu jinsi wanavyoweza kuweka mipangilio binafsi tofauti kwa ajili ya maudhui tofauti na kwa nini wangetaka kufanya hivyo.

Mwongozo huu unaweza kuchukua muundo wowote unaotaka. Unaweza kuandika mwongozo wa maandishi wa hatua kwa hatua, na kuutengeneza kama "mwongozo wa mtumiaji", ukijumuisha picha au chati ya mtiririko wa hatua, au utumie mbinu nyingine yoyote ambayo unafikiria inaweza kuwasaidia wengine kujifunza mambo haya; una uhuru wa kuwa mbunifu!

Katika mwongozo huo, pia hakikisha kwamba:

  • Unawaonesha wasomaji jinsi ya kukagua na kubadilisha mipangilio binafsi katika mitandao ya kijamii.
  • Unatoa jibu la swali kuhusu la mipangilio binafsi ambalo unafikiria kwamba ni muhimu, ukizingatia mjadala wa kundi uliopita.
DONDOO KWA MWALIMU

Wahimize wanafunzi wachague mitandao tofauti ya kijamii ili kwa pamoja, wagusie mitandao mingi ya kijamii. Wape wanafunzi dakika 30 ili wakamilishe zoezi hili.


End Lesson

Hongera!
Umekamilisha Somo


Chanzo:
Maudhui haya yanahifadhiwa na Meta na hivi sasa yanajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa shirika la Youth and Media katika Kituo cha Berkman Klein cha Intaneti na Jamii katika Chuo Kikuu cha Harvard chini ya leseni ya Kimataifa ya Creative Commons Attribution-ShareAlike 4.0. Unaweza kuyatumia maudhui hayo, ikiwa ni pamoja na kuyanakili na kuandaa kazi zinazotokana na maudhui hayo, kwa madhumuni ya kibiashara au la, ilimradi utataja mradi wa Youth and Media kama chanzo cha asili na kufuata masharti mengine ya leseni hiyo, kushirikisha kazi zingine zozote za ziada chini ya masharti hayo.

To help personalize content, tailor and measure ads and provide a safer experience, we use cookies. By clicking or navigating the site, you agree to allow our collection of information on and off Facebook through cookies. Learn more, including about available controls: Cookie Policy